November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mloganzila yatoa matibabu ya uhakika upasuaji ubongo

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Dar

HOSPITALI ya ​Taifa Muhimbili-Mloganzila imeendelea kutoa huduma za Kibingwa na Bobezi za Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Upasuaji Hospitali ya Muhimbili/Mloganzila Dkt. Godlove Mfuko alipokuwa akizungumza na kikundi cha Twiga House cha Hoteli ya Kilimanjaro Hyatt Regency kilichofika Hospitalini hapo kutoa misaada mbalimbali kwa watoto wenye changamoto za mgongo wazi na vichwa vikubwa wanaohitaji upasuaji.

“Mloganzila kuna mazingira tulivu, mashine za kisasa za uchunguzi, watalaam bobezi kabisa nchini wa upasuaji wa ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu pamoja na watalaam wa kada zingine ambao wanashirikiana katika kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma stahiki kwa wakati” amesema Dkt. Mfuko.

Dkt. Mfuko ameongeza kuwa hospitali inapokea watoto wengi wenye changamoto ya vichwa vikubwa na mgongo wazi na gharama za matibabu yake ni kubwa kwa watu wengi kuzimudu hivyo kuwaomba wadau kuendelea kujitokeza kuwasaidia watoto hao ili kurudisha tabasamu lao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kikundi cha ‘Twiga House’ Hoteli ya Hyatt Regency Said Mbaga amesema wao kama kikundi wameguswa kuja Mloganzila kutoa msaada kwa watoto wenye changamoto ya mgongo wazi na vichwa vikubwa ikiwa ni sehemu ya utaratibu wao waliojiwekea wa kurudisha kwa jamii.

Hospitali ya Taifa Muhimbili Mloganzila imeendelea kutumia tekonojia katika kutoa huduma za kibingwa ambapo mpaka mwezi Machi, 2024 imeshafanya upasuaji wa kutoa uvimbe kwenye sakafu ya ubongo (Transphenoidal hypophysectomy) kwa zaidi ya wagonjwa sita.