NEW YORK, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limesema kwamba mamia ya watoto na familia mjini Goma nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wako katika hatari kufuatia mlipuko wa volkano wa Mlima Nyiragongo.
Mwishoni mwa wiki, anga la Goma liligeuka kuwa jekundu na lava ya volcano ikatoka katika mlima na kusababisha maelfu kukimbia mji wenye wakazi takribani milioni mbili.
Ripoti za habari zinaonesha watu kadhaa wanaweza kuwa wamefariki dunia wakati wa uokoaji, na nyumba nyingine ziliripotiwa kuharibiwa kabisa Kaskazini mwa Goma.
UNICEF imesema kuwa, zaidi ya watoto 150 wametenganishwa na familia zao na zaidi ya watoto 170 wanahofiwa kutoweka.
“Zaidi ya watu 5,000 walivuka mpaka kuingia Rwanda kutoka Goma wakati lava inayokwenda polepole ilipokuwa ikisambaa kutoka kwenye mlima, na takribani watu 25,000 wamehama makazi yao huko Sake, kilomita 25 Kaskazini Magharibi mwa Goma.
“Hata hivyo, watu wengi taratibu wanarejea nyumbani kwani lava imeacha kutiririka,”imeeleza taarifa ya shirika hilo kwa kwa vyombo vya habari ikieleza kuhusu wasiwasi kuwa mamia wanarudi na kukuta nyumba zimeharibiwa, na usambazaji wa maji na umeme vimevurugika.
Aidha, bado haijafahamika ni kaya ngapi zimeathiriwa na mlipuko huo, inaeleza UNICEF na kwamba makundi ya watoto katika eneo karibu na uwanja wa ndege wa Goma wameachwa bila makao na maskini.
Timu ya UNICEF imepelekwa katika maeneo yaliyoathirika ya Sake, Buhene, Kibati na Kibumba ili kusughulikia mahitaji ya haraka, ambayo ni pamoja na kuweka vituo vya maji yenye dawa ndani na karibu na Sake ili kuzuia kuenea kwa kipindupindu.
Shirika hilo linaimarisha ufuatiliaji wa ugonjwa hatari unaosababishwa na maji, hasa huko Goma kufuatia kurudi kwa wakazi.
Vituo viwili vya muda vinaanzishwa kwa ajili ya watoto ambao hawajaambatana na yeyote au wametenganishwa na jamaa zao.
UNICEF inasema itashirikiana na wadau wake kushughulikia visa vyovyote vya unyanyasaji wa kijinsia au unyanyasaji mwingine, ili kutoa msaada wa kutosha wa matibabu na kisaikolojia.
Wakati huo huo, ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kulinda Amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (MONUSCO) uliandika katika Tweeter kwamba, helikopta kutoka katika ujumbe huo zilifanya safari juu ya kreta, na ilikuwa ikifuatilia kwa karibu hali hiyo.
Mara ya mwisho Nyiragongo kulipuka ilikuwa mwaka 2002, zaidi ya watu 100,000 walibaki bila makazi na karibu watu 250 waliripotiwa kufariki dunia. Ni moja ya volkano hai na zenye mlipuko mbaya zaidi duniani kwa sasa.
Mbali na hayo, uhaba mkubwa wa vyakula umeanza kushuhudiwa katika mji wa Goma wakati ambapo idadi kubwa ya wakazi wamepoteza nyumba zao kufuatia mlipuko wa volkano hiyo.
Hali hiyo ya ukosefu ya chakula ni baada ya barabara kutoka Butembo kuelekea katika mji huo ambayo imefunikwa na tope la volkano huku Gavana wa mkoa huo wa Kivu ya Kaskazini akitangaza pia kusitishwa kwa shughuli zote za shule katika maeneo hayo.
Magala na masoko ya vyakula katika maeneo kadhaa mjini Goma yameanza kushuhudia upungufu mkubwa wa vyakula tangu Jumapili, siku moja tu baada ya mlipuko wa volkeno milima ya Nyiragongo uliosababisha maelfu ya wananchi kuyatoroka makazi yao.
Hata hivyo, hali hiyo inayowatia wasiwasi mkubwa wakaazi wa Goma na raia wanaoishi katika Wilaya ya Nyiragongo iliyoteketea kwa asilimia kubwa na moto huo imetokana na kufunikwa kwa barabara muhimu inayosafirisha bidhaa kutoka Butembo hadi Goma.
More Stories
Elon Musk : Bill Gates atafilisika endapo…
Jay-Z aunganishwa na P Diddy kwa kumdhalilisha binti wa miaka 13
Samia avuna makubwa Mikutano ya Uwili G20