Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
MKUU wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt Batilda Burian amewataka vijana wote wa Mkoa huo kuchangamkia fursa mbalimbali za kuwaingizia kipato ili kujikwamua kiuchumi.
Ametoa rai hiyo juzi alipokuwa akizindua kampeni ya ‘Kijana Zungumza na Mkuu wa Mkoa” yenye lengo la kuwapa mbinu za kutumia fursa za kiuchumi zilizoko mbele yao iliyohudhuriwa na mamia ya vijana wa Mkoa huo.
RC alisisitiza kuwa vijana wana uwezo mkubwa wa kufanya kazi ila wengi wao wanasubiri ajira tu huku kukiwa na fursa lukuki za kujiajiri.
Alibainisha kuwa wameanzisha Kampeni hiyo ili kuondoa kasumba ya kusubiri ajira za serikali au taasisi binafsi pekee na kutumia muda mwingi kulalamika wakati fursa za kujiajiri zipo nyingi.
Alifafanua baadhi ya fursa zilizopo kuwa ni uwekezaji katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, ufugaji, uvuvi, ujasiriamali na nyinginezo.
Aliongeza kuwa fursa hizi hazihitaji nguvu kubwa ya uanzishwaji na kama watahitaji mtaji, serikali imeweka utaratibu wa kuwezesha makundi ya kijamii kupitia mikopo nafuu isiyo na riba ya asilimia 10.
Balozi Batilda alieleza dhamira yake kuwa ni kuona vijana wote wa Mkoa huo wakianzisha shughuli mbalimbali za kuwaingizia kipato ili kujiepusha na tabia zisizofaa.
‘Nataka ndani ya miezi mitatu mabadiliko yaanze kuonekana kwa vijana na jamii kwa ujumla kupitia kampeni hiyo’, alisema.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Viva Promotion inayojishughulisha na uchapishaji, Sylvester Geneli alisema Kampeni hii ni fursa muhimu sana kwa kila kijana kuamua hatma ya maisha yake kwa kuanzisha mradi wa kiuchumi.
Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Madam Vai Investment, Vailet Lusana, alieleza kuwa yeye ni mfano wa kuigwa kwani licha ya kuajiriwa ameanzisha kampuni yake ambayo inamlipa zaidi kuliko hata ajira aliyonayo.
More Stories
RC Mrindoko:Ufyekaji wa mahindi Tanganyika si maelekezo ya serikali
Walimu S/ Sekondari Ilala wafundwa juu ya maadili ya wanafunzi
Dkt. Samia afungua skuli ya sekondari Misufini, Bumbwini