November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkutano wa kamati wa SADC wafunguliwa

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Mkutano wa Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ( SADC) umefunguliwa jana tarehe 13 March 2023 jijini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ambapo ujumbe wa Tanzania unaongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Shaaban.

Wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Makatibu Wakuu, Mwenyekiti wa Mkutano huo ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mtangamano wa Kikanda wa DRC, Balozi Songhu Kayumba alisisitiza umuhimu wa wajumbe kushiriki kikamilifu kwa kutoa maoni yatakayolenga kufanikisha utekelezaji wa agenda zitakazojadiliwa.

Makatibu Wakuu wanajadili agenda mbalimbali ambazo ni pamoja na hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa Maamuzi ya Wakuu wa Nchi na Serikali waliyotoa katika Mikutano iliyopita.

Tanzania inashiriki kikamilifu kwenye Mkutano huo na imejipanga kusukuma utekelezaji wa agenda ilizoziibua au kuziunga mkono katika mikutano iliyopita.

Agenda hizo ni pamoja na: ujenzi wa sanamu la Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambalo litasimikwa kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Afrika (AU); Tafsiri ya Nyaraka muhimu za SADC katika lugha ya Kiswahili ambayo ni hatua muhimu ya utekelezaji wa matumizi ya lugha ya Kiswahili kwenye Jumuiya; Mpango wa Kanda wa Ununuzi wa Pamoja wa Bidhaa za Afya unaoratibiwa na Bohari Kuu ya Dawa (MSD); na Mkakati wa pamoja wa Kanda wa Kusimamia Sekta ya Mbolea.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena L. Tax (Mb) anatarajiwa kuongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Baraza la Mawaziri utakaofanyika kuanzia tarehe 18 hadi 20 Machi 2023 baada ya Mkutano wa Makatibu Wakuu kukamilika.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab na Katibu Mkuu Idara ya Uhusiano wa Kimataifa ya Afrika Kusini, Bw. Zane Dangor wakifafanua juu ya utaratibu wa mkutano huo ambapo walieleza kuwa majadiliano ya mkutano yanafanyika katika makundi manne ambayo ni; Siasa na Diplomasia; Ulinzi na Usalama; Fedha na Uchumi, na Huduma za kijamii.