December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkutano wa CHADEMA mwanzo mzuri wa falsafa ya R4 za Rais Samia

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

JUMAMOSI ya Januari 21, mwaka huu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimezindua mikutano yake ya hadhara jijini Mwanza ikiwa ni mara ya kwanza tangu miktano hiyo kuzuiwa na Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano, Hayati John Magufuli.

Rais Samia Suluhu Hassan alitangaza kufuta zuio hilo alipozungumza na viongozi wa vyama vya siasa 19 vyenye usajili wa kudumu, Ikulu, jijini Dar es Salaam, Januari 4, mwaka huu.

Kufuatia kufutwa kwa zuio hilo, CHADEMA kimekuwa chama cha kwanza kuanza mikutano hiyo na kupitia mkutano wake wa Jumamosi imeonekana wazi kwamba Uamuzi huo umezidi kufungua ukurasa wa maridhiano ambalo limekuwa hitaji kubwa kwa Rais Samia tangu alipoingia madaraka.

Hatua ya Rais Samia kufuta zuio la mikutano ya wanasiasa ni wazi amewezesha wanasiasa kusahau yaliyopita na sasa kupitia mkutano wa CHADEMA Jumamosi, tumeshuhudia kauli zinazoaksi maridhiano ya kisiasa ambazo hatukuwahi kuziona tangu kuanzishwa tena mfumo wa vyama vingi nchini mwaka 1992.

Katika mkutano huo kinyume na ilivyozoeleka miaka ya nyuma, tumeshuhudia kauli za staa kutoka kwa kila mwanasiasa aliyepanda jukwaani, ambapo Rais Samia alipongeza kwa uongozi wake.

Aidha, baadhi wa nawasiasa walilipongeza Jeshi la Polisi kwa jinsi lilivyoimarisha ulinzi. Kivutio kikubwa kilikuwa ni kauli za hoja kutoka kwa baadhi ya wanasiasa ambao walimpongeza Rais Samia.

Miongoni mwa waliompongeza Rais Samia ni Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, huku akielezea kusikitishwa na baadhi ya wanachama wa chama hicho kumfikiria kuwa anasaliti Watanzania kwa kufanya maridhiano ya kisiasa na CCM. Mbowe alimshukuru Rais Samia kwa kukubali maridhiano na hoja za CHADEMA.

“Yawezekana baadhi yetu msinielewe, namshukuru sana Rais Samia nimekaa naye kwenye vikao vingi vya kutafuta maridhiano.”

“Yawezekana miongoni mwenu akanyanyuka yeyote kunikebehi, hatanipindisha msimamo wangu kwa sababu nachokisimamia kwa niaba ya nafsi yangu binafsi na kwa niaba ya Taifa hili, mnyonge mnyongeni,lakini haki yake mpeni.”

“Madam President alisimama kuiunga mkono hoja ya CHADEMA, halafu nakutana na wanachama wa CHADEMA wananiona nilikosea! This is madness (huu ni uendawazimu),” alisema.

Alisema hatowafurahisha watu wanaotaka amtukane Rais Samia akisema kwa neno la kiingereza “I will never do that!”.

Alisema wakati wanachama wakiona ugumu upande wa CCM kulikuwa na ugumu kuliko upande wa CHADEMA kwa sababu walijua maridhiano yoyote ya kisiasa wanakwenda kuiua na kuidumaza CCM.

“Nyinyi badala ya kunipongeza Mbowe mnakuja na mawazo ya kiharamia, Mbowe karamba asali hataki Katiba mpya hataki tume huru,” alisema.

Alisema walipoanza mazungumzo ya maridhiano moja ya misingi waliyokubaliana kuwa msingi wa mazungumzo hayo ni usiri, hivyo hata viongozi wa CHADEMA walimuona akiingia na kutoka Ikulu bila kutambua kinachoendelea.

Pamoja na kumpongeza Rais, Mbowe alisema hataacha kuikosoa Serikali yake na maridhiano yao hayamaanishi vyama hivyo vitaungana, bali CHADEMA itaendelea kuwa chama kikuu cha upinzani nchini na baadaye kuwa chama tawala.

Walichosema viongozi wengine

Viongozi wengi wa CHADEMA waliopanda jukwaani juzi walimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kuruhusu mikutano ya hadhara, huku wakimtaka kuwavumilia pindi watakapomkosoa kwa hoja na sio matusi.

Wakitoa salamu kwa wananchi waliofika kwenye uzinduzi wa mikutano ya hadhara wa chama hicho viwanja vya furahisha jijini Mwanza, viongozi hao pia walimpomgeza Rais Samia kuruhusu mikutano hiyo.

Aliyeanza kutoa salamu ni Spika Kivuli wa Bungela Wananchi Chadema, Suzan Lymo aliyesema kila mbunge na diwani kivuli atakwenda kuangalia kero katika eneo lake pamoja na kuishauri na kusimamia Serikali.

“Kwahiyo kwakufanya hivyo tunawatetea japo hatupo Dodoma,” alisema.

Mbunge wazamani wa Mbeya mjini,Joseph Mbilinyi (Sugu) alimpongeza Rais Samia kuruhusu mikutano ya hadhara akisema wanazo hoja za kuongea na wananchi.

“Ninayo furaha kuwa hapa na nampongeza Rais kwa kuwa na ujasiri wa kukubari kuondoa zuio haramu la mikutano ya hadhara kwa miaka saba.”

Alisema kupitia mikutano ya hadhara wataenda kila sehemu kuzungumzia changamoto za maji, umeme na hali ngumu ya maisha inayowakumba wananchi.

Naye Katibu wa Baraza la Wanawake CHADEMA Taifa, Catherine Ruge alisema licha ya kuwa katika kifungo cha kisiasa kwa miaka saba kimewaimarisha na kuwapa nguvu mpya.

“Kwetu sisi wanawake wa CHADEMA miaka saba imekuwa chuo cha mafunzo na ujasiri na sasa imetuimarisha, tumeimarika na tupo tayari kuwa msitari wa mbele kuongoza mapambano, jukumu la wanawake wa CHADEMA ni kuibua kero za wananchi wetu,” alisema.

Alisema wanatamani kuona jamii, wanawake na watoto wanapata huduma bora.Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Grace Kiwelu alimuhakikishia Rais Samia kuwa chama hicho hakitotumia majukwaa ya mikutano ya hadhara kutukana matusi badala yake watatoa hoja.

Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa CHADEMA , Hashimu Issa Juma alisema licha ya Rais Samia kuwaheshimisha wanawake wa Tanzania, lakini itambidi avumilie chama hicho kumkosoa.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema, John Pambalu ameiomba Serikali kukaa pamoja kupitia meza ya mazungumzo kuwarudisha wamachinga kufanya biashara zao.

Pongezi kwa Polisi

Katika mkutano huo chama hicho kimetoa pongezi kwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza kwa kukipa ushirikiano kufanikisha mkutano wa hadhara.

Akizungumza juzi Katibu wa CHADEMA Kanda ya Victoria, Zakaria Obadi alisema chama hicho kimepokea kwa furaha jinsi uongozi wa Jeshi la Polisi Wilaya za Nyamagana na Ilemela mkoani Mwanza ulivyosaidia kufanikisha mkutano huo.

“Kusema ukweli tunawapongeza na kuwashukuru Jeshi la Polisi Mwanza, wametoa ushirikiano unaostahili kwa mujibu wa sheria ikiwemo kuwapokea na kuwapa ulinzi viongozi wetu wa kitaifa wakiongozwa na Mwenyekiti wetu Freeman Mbowe,” alisema Obadi.

“Tunaamini viongozi wa Jeshi la Polisi katika mikoa mingine wataiga mfano bora uliooneshwa na wenzao wa Mwanza kwa kutimiza wajibu na jukumu la ulinzi na usalama katika mikutano na shughuli za kisasa za vyama vyote kwa haki na usawa kwa mujibu wa sheria,” alisema.

Jeshi la Polisi lilimarisha ulinzi kuanzia katika hoteli la kitalii iliyoko katikati ya jiji la Mwanza walikofikia viongozi wa kitaifa na makada wa Chadema.

Pamoja na ulinzi hotelini, askari polisi wakiwa katika magari matatu wameonekana wakiimarisha ulinzi katika msafara wa viongozi wa CHADEMA wakiongozwa na Mbowe uliokuwa ukielekea eneo la Buhongwa, nje kidogo la jiji la Mwanza yanakofanyika mapokezi rasmi kabla ya kwenda viwanja vya Furahisha kuhutubia mkutano wa hadhara.

Akizungumza na viongozi wa vyama hivyo, Samia alisema,

“Serikali inadhamiria kukwamua mchakato wa marekebisho ya katiba, kwa jinsi tutakavokuja kuelewana huko mbele.Wengine wanasema tuanze na katiba ya warionba, wengine tuanze na katiba pendekezwa, lakini kuna mambo ya ulimwengu yamebadilika.”

Alisema itaundwa kamati maalumu kwa ajili kutoa ushauri wa namna ya kwenda kupata katiba ‘si muda mrefu, tutakwenda kuanza na kamati itakayokuja kutushauri, nataka kusema katiba hii ni ya watanzania si ya vyama vya siasa’, alisema.

Ukiacha Katiba mpya, kwa muda mrefu kulikuwa na kilio kutoka kwa wanasiasa na jamii za kimataifa kuhusu haki ya kufanya siasa hasa mikutano ya siasa kuruhusiwa, ambayo ipo kisheria.

‘Hii ni haki kwa sheria zetu, ni haki kwa vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara’, uwepo wangu leo mbele yenu ni kuja kutangaza, lile tangazo la kuzuia mikutano ya hadhara sasa linaondoka’, alisema.

Akitangaza kufuta zuio hilo, Rais Samia alisema,

“Mikutano ya vyama vya siasa ni haki ya vyama vya siasa. Uwepo wangu hapa leo ni kuja kutangaza kuwa lile tangazo la kuzuia mikutano ya hadhara sasa linaondoshwa.”

Mikutano hiyo ilizuiwa muda mfupi baada ya aliyekuwa rais wa awamu ya tano, Hayati John Magufuli kuingia madarakani kupitia uchaguzi mkuu wa 2015.

“Lakini ndugu zangu tuna wajibu, wajibu wetu Serikali ni kulinda mikutano ya vyama vya siasa, wajibu wenu vyama vya siasa ni kufuata sheria na kanuni zinavyosema.Twendeni tukafanye siasa za kistaarabu, tukafanye siasa za kupevuka, tukafanyeni siasa za kujenga sio za kubomoa, si kurudi nyuma hapa tulipofika, ‘sisi ndani ya CCM tunaamini katika kukosolewa na kujikosoa.”

‘Wakati mnanikabidhi kuongoza nchi hii, busara zilinituma, kwamba jinsi nilivyolipokea Taifa hili, kuna haja ya kufanya taifa liwe kitu kitu kimoja, wote tuzungumze lugha moja.”Ili taifa lilwe moja, lazima tuwe na maridhiano, nikasema kwanza tuwe na mazungumzo kwenye vyama vya siasa’.

Kikosi kazi kilichoundwa kilileta maoni kwenye maeneo 9, ambapo makubwa matatu yaliyojitokeza ni kutaka kuruhusiwa kwa mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa, mchakato wa katiba mpya na marekebisho sheria mbalimbali.

Rais alisema tayari michakato ya marekebisho ya sheria imeanza na waziri husika atakuja kuleta taarifa ya muelekeo.

Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe akizungumza kuhusu uamuzi wa huo wa Rais kukwamua mchakato wa katiba na kuruhusu mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa alisema ‘ni hatua kubwa sie tuna furaha, amesimama kwenye maneno yake.