a Mwandishi wetu,Timesmajira
Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 14 wa Baraza la Usimamizi wa Mkataba wa Lusaka (14TH Governing Council Meeting of Parties to the Lusaka Agreement) utakaofanyika jijini Arusha katika Hoteli ya Gran Melia kuanzia Mei 8,2025.
Hayo yamesemwa leo Mei 7,2025 jijini Arusha na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt.Pindi Chana wakati akizungumza na wanahabari.
“Tumekutana hapa hii leo kwa lengo la kuwaomba kutumia vyombo vya habari mnavyoviwakilisha kufikisha ujumbe kwa Watanzania kuhusu mkutano mkubwa na wa kipekee wa masuala ya Uhifadhi wa Wanyamapori na Misitu unaoatarajiwa kufanyika hapa nchini kwetu hususani katika Jiji hili la Utalii la Arusha.”
Amesema,mkutano huu hufanyika mara moja kila baada ya miaka miwili ambapo kwa mara ya mwisho ulifanyika nchini Zambia mwezi Machi, 2022.
Balozi Dkt.Chana amesema,Baraza la Usimamizi wa Mkataba wa Lusaka, ulianzishwa mwaka 1994 kwa lengo la kuziwezesha nchi za Afrika kusaidiana katika kukabiliana na ujangili na biashara haramu ya nyara yakiwemo mazao ya misitu inayovuka mipaka ya nchi.

Tanzania ilijiunga na Mkataba huu mwaka 1999 na imekuwa ikiutekeleza kwa kushirikiana na nchi wanachama ambazo ni pamoja na Congo-Brazzaville, Kenya, Lesotho, Liberia, na Zambia.
“Kupitia Mkataba huu, Tanzania imenufaika katika nyanja mbalimbali ikiwemo kubadilishana taarifa za uhalifu wa makosa yanayohusu wanyamapori na misitu.”amesema.
Mafanikio mengine amesema ni kufuatilia na kukabiliana na mitandao ya ujangili wa wanyamapori na misitu,kufanya operesheni na doria na mafunzo ya kukabiliana na vitendo vya uhalifu.

“Katika mkutano huu wa 14 ambao utafanyika hapa nchini kwetu katika Jiji hili la Arusha, pamoja na mambo mengine utapokea taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya Mkutano wa 13 wa Baraza na utaidhinisha Mpango Mkakati wa Mkataba wa Miaka mitano (2025-20230).”
Aidha, amesema Tanzania kupitia Waziri wa Maliasili na Utalii, itapokea nafasi ya Urais wa Baraza la Usimamizi wa Mkataba kwa kipindi cha miaka miwili ijayo kutoka kwa Waziri wa Maliaisili wa Kenya.

Waziri Chana amesema, kufanyika kwa mkutano huu katika jiji la Arusha ni fursa ya kutangaza utalii, kufanya biashara na kushiriki katika juhudi za kikanda na kimataifa za kukabiliana na ujangili na biashara haramu ya wanyamapori na mazao ya misitu.
Kwa mujibu wa Kanuni za Uendeshaji wa Mikutano ya Baraza, mkutano huo unatarajiwa kuhudhuriwa na takribani Mawaziri 19 wanaoshughulikia masuala ya Maliasili na Mazingira kutoka katika nchi 19 za Afrika.
Sambamba na wawakilishi kutoka katika Mashirika ya Umoja wa Mataifa (UNEP, UNODC, UNDP, INTERPOL WCWG) na Katibu Mkuu wa Mkataba wa Kimataifa wa Biashara ya Wanyamapori na Mimea Iliyohatarini kutoweka (CITES).
Aidha, kwa Tanzania,Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na taasisi zake zinazounda Wakala wa Utekelezaji wa Mkataba (National Bureau) zitashiriki.
More Stories
Kikundi cha Mwanamke Shujaa chamchangia Fedha ya kuchukua Fomu Rais Samia
Magugu maji yatajwa changamoto ya uzalishaji umeme maporomoko Rusumo
Wataalam Maendeleo ya Jamii waaswa kutoruhusu tamaduni potofu