November 16, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkurugenzi Paradise Mission awataka vijana kutumia fedha kwa utaratibu

Na Esther Macha, Timesmajira,Online ,Mbeya

VIJANA jijini Mbeya wametakiwa kutumia fedha kwa utaratibu ili kuweza kufikia malengo waliojiwekea ili kujikwamua kiuchumi badala ya kuweka tamaa mbele ambazo zinaweza kuvuruga mikakati yao ya kusonga mbele .

Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi wa Paradise Mission Pre&Primary School iliyopo katika Mji Mdogo wa Mbalizi jijini hapa, Ndele Mwaselela wakati akizungumza na  waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu jinsi vijana wanavyoweza kutoka hatua moja kwenda nyingine .

Mwaselela amesema vijana wanatakiwa kutimiza malengo yao kwa hatua na kwa utulivu, wasiende haraka.

“Ni lazima wafanye kila kitu kwa hatua ili kufanikisa kile wanachohitaji ikiwa ni pamoja na kutenga muda wa kujituma kufanya kazi,” amesema.

Hata hivyo amesema inawezekana vijana kujiwekeza vizuri kikubwa ni kujipanga na kutia nia ya kitu wanachohitaji kufanya.”Mfano mimi nimetoka familia ya maskini baba yangu alikuwa mlinzi na mama yangu mama lishe wala sijachakachua maisha,“amesema Mwaselela.

“Tuache kushangaa tufanye kwa vitendo leo hii nimeona kuna vijana wanawekeza kwenye madini wilayani Chunya kesho watakuwa matajiri  na isitoshe hawa vijana wameanza na mitaji midogo sana, kesho utawaambia wakope hawawezi kukopa watakopa pale watakapohitaji kufanya jambo kubwa tofauti na hilo huwezi kukopa pasipo na malengo na ndio chanzo cha kutumia fedha vibaya katika umri mdogo sababu unachukua fedha isiyo kuwa na utaratibu ,miradi hii inaenda kwa utaratibu lazima muipe muda Paradise mission ifanye kazi na ione faida zake na changamoto zake,”amesema Mkurugenzi Mwaselela .

Mkurugenzi wa Paradise Mission,Ndele Mwaselela akizungumza na waandishi wa habari (Hawapo pichani)

Akifafanua zaidi amesema mtu anapoenda kukopa fedha kwenye taasisi za kifedha mfano benki kunakuwa na tatizo la majanga lakini huna janga lolote unaenda kukopa ndio mwanzo wa kuwa matumizi mabaya ya fedha .

Aidha, Mwaselela ameleeza kuwa mpaka kufikia hatua hiyo ya kumiliki shule amekuwa kijana wa kwanza katika Mkoa wa Mbeya kuwekeza mradi mkubwa kama huo bila kugusa mkopo wowote na  inawezekana kuwa watu wengine wamefanikiwa kutoka maeneo tofauti ikiwemo familia tajiri, lakini kwake imekuwa tofauti kubwa kutokana na kutoka familia ya kimaskini.

Mwaselela amesema hiyo ni fursa kwa vijana wa Mkoa wa Mbeya kikubwa  ni kujiwekea ratiba vizuri na kwamba kila kitu kina kiasi na hakuna kinachoshindikana kikubwa ni kujipanga na kuheshimu wanachotaka kufanya na kuweka malengo .