January 7, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkurugenzi Nsimbo atakiwa kugawa eneo kwa wananchi

Na George Mwigulu, Timesmajira Online,Nsimbo.

MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Nsimbo Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi ametakiwa kugawa eneo la hekari 5996.45 kwa wakulima wa Kata za Kapalala,Nsimbo na Uruwila ili kuondoa kero iliyopo kwa wananchi ambao wameshindwa kufanya shughuli za uzalishaji wa mazao ya kilimo katika eneo hilo.

Ombi hilo limetolewa Februari 28, mwaka huu na Mbunge wa Jimbo la Nsimbo, Anna Lupembe akiwa kwenye ziara yake ya kikazi ya kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua katika kijiji cha Kapalala jimboni humo.

Mbunge wa Jimbo la Nsimbo Mkoa wa KataviAnna Lupembe akiwahutubia wananchi wa kijiji cha Kapalala

Wakati akisikiliza kero za wananchi Mbunge huyo aliulizwa na Costatino Nkunda mkazi wa kijiji hicho kuwa Halmashauri ya Nsimbo ni lini itawapatia eneo la Msaginya Forest la zaidi ya hekari 13000 huku akilalamikia halmashauri hiyo kumpatia eneo mwekezaji wasiye mfahamu.

Lupembe akijibu swali hilo ameeleza kuwa anataarifa nalo kupitia vikao vya ndani vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Kapalala ambapo baada ya kuelezwa aliwasilina na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo kwa njia ya simu na kukiri kuwa suala hilo analifahamu na kunakitalu namba 148 ambacho kipo eneo la wafugaji wamempatia mwekezaji.

“Lakini lile eneo ambalo mlilopangiwa ninyi wananchi liko vilevile …nikauliza kwanini hadi hivi sasa hujawagawia wananchi?,nikamwagiza Mkurugenzi na kumuomba kukutana na wenyekiti wote wa serikali za vijiji na Madiwani wa Kata husika,nendeni site mkawape maeneo hayo wananchi waendelee kufanya kazi zao za kilimo,”amesema.

Mbunge huyo amewaomba wananchi kuondoa hofu kwa kuwa eneo hilo watapatiwa haraka iwezekanavyo na kama kutakuwa na ucheleweshwaji wa aina yoyote amewasihi kuwasiliana naye ili aweze kuchukua hatua zaidi.

Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Kapalala, Enock Kapele amesema kuwa wananchi hawana sababu ya kuwa na hofu kwani kama viongozi wa serikali ya kijiji wameshirikishwa kwa kila hatua kuhusu eneo hilo lililopo Msanginya forest.

Kapele amefafanua kuwa serikali iligawa eneo hilo kwenye sehemu mbili kwa maana ya eneo la wafugaji na wakulima hivyo wanapaswa kutambua kuwa hakuna eneo lililomilki yao ambalo amepatiwa mwekezaji yeyote.

“Wananchi wenzangu tambueni kuwa eneo hilo limegawiwa kwenye sehemu mbili kuna eneo hekari 5996.45 ni sehemu ya wakulima na hekari 7520.12 kwa wafugaji ambapo eneo lililotolewa kwa mwekezaji ni la wafugaji,”amesema Kapele.

Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Kapalala wameshukuru Mbunge huyo kwa kuweza kuwasiliana na Mkurugenzi kwa wajili ya kutafuta ufumbuzi wa kero yao ambapo wanadai kuwa ni muda wa mwaka mmoja umepita bila mafanikio yoyote ya kugawiwa ardhi.

Stella Fred,Mkazi wa kijiji cha Kapalala amesema kuwa Halmashauri hiyo kushindwa kuwagawia eneo hilo kwa muda muafaka ni chanzo cha baadhi ya wakulima wengine kukosa maeneo ya kutosha kwa ajili ya kufanya kilimo.

Costatino Nkunda.Mkazi wa kijiji cha Kapalala akitoa kero yake kwa Mbunge wa Jimbo la Nsimbo Anna Lupembe

Amesema kuwa uchumi wao kwa kiasi kikubwa unategemea kilimo ambapo kukosa maeneo makubwa kwa ajili ya uzalishaji wa mazao ya kilimo utazorotesha ukuaji wa uchumi wao.