December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkurugenzi MWAUWASA apewa maua yake kwa ubunifu

Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza

MKURUGENZI Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA),amepongezwa kwa ubunifu na utekelezaji wa miradi ya uondoshaji na kutibu majitaka na matokeo ya haraka.


Pongezi hizo zimetolewa na Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Nyamagana,leo ilipotembelea na kukagua miradi iliyotekelezwa na mamkala hiyo.

Akitoa pongezi hizo, Katibu wa CCM Wilaya ya Nyamagana, Geofrey Kavenga amesema kwa kipindi kifupi MWAUWASA chini ya Mkurugenzi Mtendaji, Neli Msuya imefanya mambo makubwa ya kuhakikisha wananchi wa Jiji la Mwanza, wanapata maji safi na salama kwa matumizi ya kibinadamu.

Amesema utekelezaji wa mradi wa kuondosha na kutibu majitaka utaboresha usafi na mazingira na kuimarisha afya za wafungwa na watumishi wa Gereza Kuu la Butimba ikiwemo kuboresha maji ya Ziwa Victoria ambalo ni chanzo kikuu cha maji jijini Mwanza.

Amewataka wanufaika kutunza miundombinu ya mradi ili itumike muda mrefu kwa sababu Nyamagana imependelewa kwa miradi ya kimkakati inayoonekana kwa macho na thamani yake ambapo Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ametoa fedha hizo kuboresha mazingira na maji.

Diwani wa Butimba (CCM),Marwa Mbusiro amesema mazingira ya Gereza la Butimba hayakuwa rafiki kutokana na kuharibika kwa miundombinu ya vyoo,hivyo mradi huo utabadilisha mazingira na madhari ya gereza na kuleta tija kwa jamii ya wafungwa.

Naye Mwenyekiti wa CCM Kata ya Butimba,Faustine Ntonja amesema gereza hilo lilikuwa kero kwa kutirisha maji sababu ya uchakavu wa miundombinu iliyojengwa kwa miaka mingi,hivyo alimpongeza Rais Dk.Samia kwa kuleta fedha nyingi za maendeleo yanayohitajika na kuboresha mazingira.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa MWAUWASA Neli Msuya amesema mradi huo wa uboreshaji mfumo rahisi wa uondoshaji na kutibu majitaka ya Gereza la Butimba utasaidia kuboresha maji ya Ziwa Victoria na kuyafanya kuwa salama kwa watumiaji.

Meneja miradi wa MWAUWASA,Celestine Mahubi,akisoma taarifa ya mradi huo amesema umegharimu Euro 856,462.41 sawa na zaidi ya bilioni 1.9,kwa ufadhili wa Serikali na wabia a maendeleo Benki ya Uwekezaji ya Ulaya(EIB) na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD),umezingatia athari za mazingira.

Amesema mradi huo wa miundombinu ya majitaka utaboresha hali ya usafi na mazingira katika Gereza la Butimba ambapo utawanufaisha watu 4,000 wa jamii ya wafungwa na watumishi wa gereza,umekamilika na unatoa huduma ya kuondosha na kutibu majitaka eneo la gereza hilo.

Katika hatua nyingine Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Nyamagana,Peter Bega amesema maji ni agenda ya kwanza ya Chama Cha Mapinduzi kuhakikisha wananchi wanayapata.

Amekemea watumishi kero wa MWAUWASA wanaochelewesha wananchi kupata huduma ya maji na kuwataka wabadilike na kuhakikisha maji yanawafikia baada ya mradi wa Matokeo ya Haraka wa Luchelele kukamilika.

“Watumishi wote wakifanya kazi na kuwajibika hakuna sababu ya CCM kukosa kura,yote yakifanyika na kukamilika itakuwa na uhakika wa kupata ushindi wa asilimia 90 katika uchaguzi wa serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu wa Rais,Wabunge na Madiwani,”amesema Bega.

Aidha, Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Nyamagana,Witness Makale amesema Rais Samia ametoa fedha nyingi za miradi ya maji inayolenga kumtua mwanamke ndoo ya maji kichwani, hivyo miundombinu yake itunzwe ikiwemo kudhibiti wanaochezea koki kuchepusha maji kwani dhamira ya serikali ni kila mtu.