Na Penina Malundo, Timesmajira
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO, Lazaro Twange amefanya ziara ya kikazi kwa kuitembelea Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC) ambayo ni Kampuni Tanzu ya shirika hilo kwa lengo la kuzifahamu taasisi zilizo chini ya shirika analolisimamia.
Akiongea leo mei 15,2025 na Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti pamoja na watumishi akiwa katika ofisi za TGDC makao makuu, Mkurugenzi Twange ameeleza kufurahishwa kwake na wale walioanzisha wazo hadi uwepo wa taasisi hii iliyoanzishwa mwaka 2013 kwa lengo la kuendeleza rasilimali ya jotoardhi nchini ili kuzalisha umeme.
Pia, ameipongeza TGDC kwa ujumla kwa utendaji kazi nzuri akitambua kuwa uanzishwaji wa jambo mpaka kuleta matokeo huchukua mda mrefu lakini hatua ni nzuri na kusisitiza kuwa Watanzania wanahitaji umeme.

“Ninamshuruku Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuniamini na kunipa nafasi ya kuwa mtumishi wa TANESCO na niwapongeze sana walioanzisha wazo mpaka leo tunayo TGDC.
” Pia niwapongeze wote kuanzia Bodi ya Wakurugenzi mpaka wafanyakazi kwa utekelezaji mzuri wa kazi”amesema.
Amesema , Watanzania wanahitaji kuuona umeme wa jotoardhi,hivyo TGDC inatakiwa kujitahidi kuhakikisha wananchi wanauona umeme huu.

Mkurugenzi Twange alimaliza kwa kusema kuwa atafurahi kuwa sehemu ya shuhuda wakati wa upatikanaji wa umeme huu na yupo tayari kufanya kazi na kila mmoja wao,.”Nitawapa ushirikiano na ninafurahi kwamba, kazi nyingi zimefanywa na wazawa. Ninatamani mjue yakwamba, watu wanataka kuridhika na kuridhika kwao ni kuupata umeme wa jotoardhi,”amesema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TGDC ,Prof. Shubi Kaijage alimkaribisha na kumpongeza kwa kuteuliwa, lakini pia kwa kufika na kuwasalimu wafanyakazi.

Amemuhakikishia Mkurugenzi huyo kuwa, maelekezo aliyotoa wameyachukua na kuyafanyia kazi na menejimenti inaendelea kutekeleza majukumu yake ipasavyo ili kuleta matokeo.
Awali akitoa maelezo utekelezaji wa shughuli mbalimbali ndani ya taasisi, Meneja Mkuu wa Kampuni ya TGDC ,Mhandisi Mathew Mwangomba ameeleza kuwa, TGDC inaamini kuwa, umeme wa jotoardhi utakapozalishwa, Tanzania itakuwa imeondokana na changamoto ya upatikanaji wa umeme kwa kiasi kikubwa kupitia vyanzo msteto na kusema kuwa, ndani ya muda mfupi anaamini watatoa matokeo chanya wakitarajia kuanza kuchimba visima vya uhakiki wa mradi wa Jotoardhi Ngozi kwa lengo la kuzalisha umeme.

Mhandisi Mwangomba ameongeza kuwa, utafutaji wa rasilimali ya jotoardhi unahitaji uwekezaji mkubwa na teknolojia ya hali ya juu, jambo linalopelekea TGDC kuendelea kuomba ushirikiano wa karibu kutoka kwa viongozi wake mbalimbali akiwemo MD Twange ili kuweza kufanikisha azma yake na kuhitimisha kwa kusema, kila mtumishi wa TGDC anadaiwa Megawati 1 ambayo inapatikana kwa kila mmoja kutekeleza jukumu lake na kwamba wafanyakazi wana ari ya kazi na watatoa matokeo.
TGDC ni kampuni tanzu ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ambayo inamilikiwa na serikali ya Tanzania kwa asilimia 100 iliyoundwa tarehe 19 Desemba 2013 kwa lengo la kuendeleza rasilimali ya jotoardhi (geothermal) nchini na kuanza rasmi tarehe 1 Julai, 2014. Kazi yake ni kufanya utafiti, maendeleo, na uendeshaji wa miradi ya nishati ya jotoardhi. Hadi hivi leo, TGDC imekwisha kuainisha maeneo takribani 52 katika mikoa 16 ya Tanzania bara yenye viashiria vya nishati ya jotoardhi ambavyo vyote kwa pamoja vinakadiriwa kuzalisha Megawati 5000 za umeme na Megawati 15,000 za joto kwa matumizi mengineyo.
More Stories
Serikali yawezesha miradi 80 kwa utaratibu wa PPP
Mpogolo akabidhi Cheti kwa wahitimu
Gavu asisitiza kuimarisha ushirikiano Tanzania na China