Na Steven Augustino, TimesMajira Online, Tunduru
MKUU wa Wilayani Tunduru, mkoani Ruvuma, Julius Mtatiro (Pichani kushoto) ametoa ufafanuzi kuhusu kifo cha mkulima wa Kijiji cha Namasalau Kata ya Tuwemacho aliyefariki dunia aprili 19 ambapo inadaiwa ni mmoja wa wadaiwa sugu wa ambapo alikopa mifuko miwili ya sulpher yenye dhamani ya shilingi 64,000.
Akitoa maelezo wakati akitoa salam za serikali katika kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani, Mtatiro amemtaja mkulima huyo kuwa ni Shaibu Mandiwele kuwa inadaiwa alikuwa anawakimbia polisi waliodaiwa kwenda katika Kijiji cha Tuwemacho ili kuwakamata wadaiwa sugu wa pembejeo za kilimo zilizotolewa na Serikali.
Kikao hicho kilichoketi katika ukumbi wa Klasta, Tarafa ya Milingoti iliripotiwa kuwa mkulima huyo aliamua kukimbia kwa utashi wake, bila kutishwa, wala kukimbizwa na bila sababu za msingi, jambo ambalo ni la kusikitisha.
“Ni kwamba, wakulima wa Tunduru hawajalipa zaidi ya shilingi milioni 500 za pembejeo, matokeo yake Wilaya yetu haikopesheki katika msimu ujao wa korosho, na matokeo yake ni kuashuka kwa uzalishaji wa korosho jambo ambalo litasababisha umasikini” amefafanua Dc, Mtatiro.
Ili kuhakikisha ufuatiliaji na kukusanya madeni hayo, iliundwa kamati maalumu ya kuwafuatilia wakulima wanaodaiwa (wadaiwa sugu) jambo ambalo litaifanya wilaya hiyo ikidhi vigezo ili wakulima wa Tunduru waendelea kukopeshwa katika msimu ujao
“Tuliunda kamati hii baada ya jitihada za AMCOS na viongozi wa vijiji katika kufuatilia madeni hayo kugonga mwamba” amesisitiza Mtatiro.
Mtatiro ameleza kuwa Kamati hiyo haikuwa inapita kuwakamata wakulima mitaani, bali wakulima wanaitwa katika ofisi za Vijiji na Kata kwa wito maalum, wale wanaoweka jitihada ya kulipa wanapewa utaratibu, wale ambao wana mashaka na madeni yao au wana sababu maalum wanajieleza ili kushauriwa namna bora ya kutatua tatizo lao.
Kamati hiyo inaundwa na wajumbe kutoka katika taasisi mbalimbali ikiwemo TAMCU, Bodi ya Korosho, AMCOS na vyombo vya Ulinzi. Ambapo taarifa za madeni wanazipata kutoka katika Ofisi ya Mtendaji wa Kijiji.
Hata hivyo wakiwa ndani ya ofisi hiyo wa wadaiwa wote walioitikia wito walikuwa nje ya ofisi hiyo bila ulinzi wowote ambapo inadaiwa ghafla mtu mmoja alianza kukimbia huku akiwahamasisha wenzake akiwaeleza kuwa “kule ndani walikuwa na mkakati wa kutukamata na kutuweka LOCKUP” ameeleza Mtatiro
Amesema hata hivyo wadaiwa wengine waliendelea kusubiri nje ya ofisi wakisubiri maelekezo ya kamati na hawakumfuata na kwa sababu nje hakukuwa na mtu au chombo chochote kilichokuwa na nia ya kumfukuza au kumkimbiza, mkulima huyo aliendelea kukimbia, nadhani lengo lake lilikuwa ni kwenda na kujificha kwa utashi wake mwenyewe.
Amesema baada ya mazungumzo ya Kamati na Mtendaji, Kamati iliondoka na wadaiwa wote na kufanya nao kikao kazi katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ambapo taarifa za madeni yao zilihakikiwa na wameahidi kulipa madeni hayo kwa tarehe zilizokubaliwa na pande zote mbili, kisha wakulima wadaiwa sugu waliruhusiwa kuelekea majumbani mwao.
Wakati kamati ikiendelea na kikao, taarifa zikafika katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya kuwa yule mkulima mdaiwa aliyekimbia, alizidiwa na baadaye nduguze wakaomba msaada wa gari na kumkimbiza hospitali ambako alifariki muda mfupi uliofuatia.
“Wito wangu kwa wakulima wote wadaiwa sugu wa pembejeo wilayani Tunduru, kuipa kamati yetu ushirikiano ili kukamilisha uhakiki na ufuatiliaji wa madeni kwa njia nzuri inazotumia” amesistiza Mtatiro.
More Stories
Wizara ya madini yakusanya bil.521 nusu ya kwanza mwaka wa fedha 2024/25
Meya awafunda wenyeviti Serikali za Mitaa
Mgeja aipongeza CCM kwa uteuzi Wagombea Urais