Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online,Simanjiro
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mhandisi Victor Seff, amemuagiza Meneja wa TARURA Mkoa wa Manyara kumuelekeza Mkandarasi Afritrust kurudi eneo la kazi ili kuendelea kutekeleza mradi kama mkataba wake alivyoingia.
Ambapo utekelezaji wa mradi huo ulianza mwaka wa fedha 2023/2024 kwa bajeti kutoka Serikali kuu na utekelezaji wake umefikia asilimia 60.
Mhandisi Seff ametoa maelekezo hayo wakati alipofanya ziara ya kukagua barabara ya Lengai-Lemkuna-Msitu wa Tembo yenye urefu wa kilomita 89 wilayani Simanjiro ili kujionea uharibifu wa barabara hiyo uliosababishwa na mafuriko.
Meneja wa TARURA Wilaya ya Simanjiro Mhandisi Naftal Chaula ametaja sababu kubwa za kuchelewa kukamilika kwa mradi huo ni kutokana na mafuriko yaliyoharibu kazi zilizokuwa zikifanyika na Mkandarasi hivyo kusababisha kufanya mapitio ya usanifu na kuonekana kuna ongezeko la makalavati manne(4) ili kuweza kudhibiti maji katika eneo la mradi.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Simanjiro Christopher Ole Sendeka amesema barabara hizo ni kiungo muhimu kati ya Makao Makuu ya Wilaya ya Simanjiro na Halmashauri ya Manispaa ya Moshi.
Pia barabara hiyo ni kiungo kiuchumi na imekua ikiingizia Halmashauri hiyo mapato makubwa kutokana na kusafirisha madini ya mchanga ambapo asilimia kubwa hutumiwa na wananchi wa Wilaya ya Moshi katika ujenzi wa nyumba.
Hata hivyo Mbunge huyo alimuomba Mtendaji Mkuu kuangalia uwezekano wa TARURA kufanya ujenzi wa barabara tatu za Msitu wa Tembo-Lemkinai-Langai Km. 25, Nabelela-Landanai-Lemkunae pamoja na ufunguzi wa barabara ya Msitu wa Tembo-Naisinyai Km. 20 ili kuweza kuchochea shughuli za kijamii.
Awali Diwani wa Kata ya Msitu wa Tembo Keliya Mollel ameeleza kuwa eneo hilo lilishakumbwa na mafuriko mengine ambapo mwaka 1998 yaliyofika hadi kwenye makazi hivyo ameomba makalavati zaidi yaongezwe kwenye barabara hiyo ili maji yaweze kutoka kwa urahisi.
More Stories
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â