Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Korogwe
UONGOZI wa shule ya Msingi Mkalamo iliyopo Kijiji cha Mkalamo, Kata ya Mkalamo wilayani Korogwe wamelia kwa Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga Mwantumu Zodo kuwa shule yao haina miradi ya madarasa mapya wala nyumba za walimu kwa miaka 20 sasa.
Wamesema shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 1945, mara ya mwisho kujengewa vyumba vya madarasa ni miaka 20 iliyopita, ambapo walijengewa vyumba viwili kupitia Mpango wa Maendeleo Elimu ya Msingi (MMEM).
Akitoa kilio hicho Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Mkalamo Erasmus Mrema wakati Mbunge huyo alipotembelea miradi Kata ya Mkalamo ambapo alifika hadi kwenye shule ya Msingi Mkalamo ambayo aliwai kufundisha katika shule hiyo ikiwa ni ajira yake ya kwanza serikalini mwaka 2006.
Ambapo amesema shule hiyo kushindwa kupata mradi kwa muda mrefu imejenga chuki kwa wananchi wa Kitongoji cha Masimbani na Mkalamo ambavyo vyote vipo kwenye Kijiji cha Mkalamo.
Ambao wanahoji kwanini Kitongoji cha Masimbani wanapewa miradi ya madarasa wakati shule mama iliyopo makao makuu ya kijiji hawana mradi wowote kwa muda mrefu.
“Shule yetu ina upungufu wa vyumba vya madarasa, wanafunzi wanapokezana kusoma,hivyo tunakuomba utupiganie tupate mradi wa vyumba vya madarasa kwani tuna zaidi ya miaka 20 hatujapata mradi,”amesema Mrema.
Mrema amesema shule hiyo kongwe pia ina nyumba tano za walimu, lakini kuanzia nyumba hizo pamoja na vyumba vya madarasa, vyote ni chakavu,hivyo wanaiomba serikali pamoja kuwajengea vyumba vingine vya madarasa pamoja nav kuwafanyia ukarabati wa majengo yao.
Kaimu Ofisa Elimu Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Nassoro Mshangama amesema ni kweli shule hiyo haijapelekewa mradi wowote kwa muda mrefu moja ya sababu ni kuimarisha shule ya Msingi Masimbani ambayo ipo kwenye Kijiji cha Mkalamo lakini wapo kwenye mpango wa kupeleka mradi wa Boost kwa ajili ya ujenzi wa madarasa.
Kwa upande wake Mbunge huyo wa Viti Maalumu Zodo amesema haiwezekani shule ikose mradi kwa miaka 20, hivyo ameiwataka halmashauri watafute fedha kwa njia yeyote ili shule hiyo iweze kupata vyumba vipya vya madarasa na vifanyiwe ukarabati.
“Shule hii ndiyo ilikuwa ajira yangu ya ualimu mwaka 2006, hivyo naijua kweli haijaongezwa chumba chochote cha darasa,serikali imekuwa ikitoa fedha kwa shule za msingi hapa nchini, lakini hii haijapangiwa kwa miaka 20 sasa,naagiza tafuteni fedha, iwe kwa mapato ya ndani ama Serikali Kuu muweze kuleta hapa muongeze vyumba vya madarasa,” amesema Zodo.
Katika ziara hiyo Zodo alikataa kukagua ujenzi wa zahanati ya Kijiji cha Pasilasi, Kata ya Mkalamo, ambayo Serikali imeshatoa kiasi cha milioni 50 ili kuunga mkono nguvu za wananchi, lakini bado haijakamilika.
Pia alitembelea zahanati ya Kweisewa ambayo imejengwa na TANAPA na imekamilika, na alitembelea shule ya msingi Masimbani kutembelea madarasa mapya.
Lakini alikagua daraja la kienyeji la matete na waya la watembea kwa miguu linalokatiza mto Pangani kutoka Kijiji cha Mkalamo kwenda vijiji vya Kweisewa, Pasilasi na Makayo, hivyo amesema jambo hilo amelichukua ili wananchi wajengewe daraja imara ama kupewa kivuko.
More Stories
Wakuu wa Wilaya,Wakurugenzi watakiwa kusimamia programu za chakula shuleni
Mbowe akuna wengi kuhusu maridhiano
Waziri Chana amuapisha Kamishna uhifadhi NCAA, ampa maagizo mazito