January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkakati wa usimamizi wahitajika kukuza ukuaji wa Tehama

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

SERIKALI imesema misingi ya Tehama ina nafasi kubwa katika maendeleo na ukuaji wa kitaifa hivyo kunahitajika mikakati na usimamizi madhubuti ili nchi iweze kufaidika na ukuaji huo.

Hayo yamesemwa Jijini Dar es salaam mapema Leo hii na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Tehama Mhandisi Samson Mwela katika hafla ya utiaji saini wa makubalino Kati ya Taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation ambayo inajishughulisha na masuala ya kijamii kwa niaba ya kampuni ya Vodacom Tanzania pamoja Taasisi ya African Child projects (ACP) kwa lengo la kuunganisha shule 50 nchini kwenye mtandao wa intaneti pamoja na kuzipatia vifaa vya kujisomea kidijitali ikiwemo kompyuta.

Amesema katika mazingira ya sasa ya uchumi unaotegemea TEHAMA, ni muhimu kwa sekta zote zinazoendeshwa na TEHAMA ili kuweza kumudu mabadiliko yanayotokea nchini na duniani kwa ujumla.

“Ni furaha kubwa kuona sekta binafsi ikishirikiana na AZAKI kutimiza malengo na sera za kitaifa Tunapongeza jitihada hizo.”amesema

Mwela amesema nia ya serikali ya Tanzania kuleta elimu ya kiwango bora iwezekanavyo kwa wananchi.

“Katika ulimwengu wa sasa, upatikanaji wa huduma kidijitali unazidi kuwa muhimu katika utoaji wa maudhui ya elimu tutaendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika upanuaji wa mitandao haswa katika maeneo ya vijijini ili kuhakikisha tunatimiza malengo yetu na hivyo kuwanufaisha watanzania wote kwa matunda ya maisha ya kidijitali.”

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Vodacom Foundation Tanzania Rosalynn Mworia, amesema dhamira ya kampuni hiyo ni kuipeleka Tanzania katika ulimwengu wa kidijitali kupitia teknolojia.

Amesema makubaliano hayo yanalenga kuunganisha shule 50 ambazo ziko katika mikoa 10 nchini na kuonyesha njia endelevu kitaifa ya kuunganisha shule kidijitali.

“Mradi huu umebuniwa ili kuchangia jitihada za kutambua shule zenye uhitaji pamoja na kuziunganisha shule hizo na intaneti ili kupata suluhisho kwa wahitaji katika mazingira ambayo rasilmali ni finyu”amesema

Na kuongeza kuwa

“Tuko tayari kutimiza wajibu wetu kwa kushirikiana na serikali na wadau wote wanaohusika ili kujenga mazingira wezeshi pamoja na kuwekeza kwenye miundombinu ili kutimiza malengo yetu ya kujenga jamii ya kidijitali nchini.”amesema

Aliongeza kuwa uwepo wa mradi huo utasaidia nchi kwa kiwango kikubwa kufikia lengo la tisa endelevu la maendeleo (SDG9) ambalo linalenga kuongeza kwa kiwango kikubwa upatikanaji wa TEHAMA na kujitahidi kuleta upatikanaji wa huduma za intaneti kwa gharama nafuu kwa nchi zinazoendelea.

Amesema chini ya mkataba huu, Vodacom Tanzania Foundation kwa kushirikiana, na taasisi ya Vodafone Foundation, itagawa kompyuta 186, tablet 246 pamoja na uunganishwaji kwenye mtandao wa intaneti kwa mwaka mmoja kwa shule 50 nchini.

Aliongeza kuwa Shule hizo ziko katika mikoa ya Kilimanjaro, Mara, Tabora, Katavi, Morogoro, Iringa, Ruvuma, Njombe, Kigoma na Tanga.

Hata hivyo amesema lengo kuu la mradi huu ni kuunganisha shule hizo na kuleta upatikanaji wa maudhui ya elimu bila gharama yeyote.

“Mradi huu unaendana kikamilifu na malengo ya Vodacom Tanzania Foundation katika kuunganisha watanzania, kupata elimu na kujenga uwezo wa kidijitali kwa vizazi vijavyo Zaidi, mradi huu utafungua jukwaa la elimu la Vodacom kwa shule 50 na wanafunzi takribani 42,291 pamoja na waalimu wao”amesema

Pia amesema wanafunzi watanufaika na maudhui ya bure yanayopatikana kupitia mfumo wa E-Fahamu unaoendeshwa na Vodacom Tanzania Foundation na ambao maudhui yake yamepitishwa ili kuendana na mitaala ya kitaifa kwa shule za msingi na sekondari.

Alibainisha kuwa Jukwaa la E-Fahamu hadi sasa lina zaidi ya vitabu 80 vya kiada na zaidi ya vitabu 1,000 vya masomo ya ziada pamoja na katuni na video kadhaa za elimu.

Naye mkurungezi Mtendano wa African Child Projects Catherine Kimambo, alisema Mlipuko wa Covid-19 ulionesha haja ya ushirikishwaji kidijitali na kuongeza kasi ya uunganishwaji kwa njia kadhaa ambazo hazikutegemewa.

Hata hivyo, tofauti kati ya waliounganishwa na ambao hawajaunganishwa imeongezeka, kwani waliokuwa wanapata mawasiliano ya intaneti ya kasi waliweza kuendelea na masomo na shughuli za kikazi wakiwa mbali, wakati wale wasiokuwa na mawasiliano hayo wakiwa wameachwa nyuma.

“Ni nia yetu ACP kujitahidi kupunguza hali hii kwa kiwango kikubwa iwezekanavyo katika sekta ya elimu mafaniko ya mradi huu yatapunguza gharama za uunganishwaji kwa mashule na wakati huo huo, kuonyesha umuhimu wa mawasiliano ya intaneti katika kuboresha mifumo ya elimu nchini na hivyo kushinkiza uwekezaji kwenye elimu ya kidijitali katika mitaala ya taifa”alisisitiza

Kutoka kushoto Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Foundation Rosalynn Mworia pamoja na Mkurugenzi wa African Child Projects, Catherine Kimambo baaada ya kusaini mkataba wa makubaliano baina ya mashirika hayo mawili kushirikiana katika mradi wa ‘Scale Up!’ wenye lengo la kuongeza ufaulu wa wanafunzi mashuleni kwa kupunguza changamoto zilizopo katika nyenzo za ufundishaji kama ukosefu wa vifaa vya kisasa vya kidigitali, uhaba wa walimu.
Kutoka kushoto Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Foundation Rosalynn Mworia, anayefatia ni Mkurugenzi mkuu wa Tume ya Tehama, Mhandisi Samson mwela (mwenyesuti nyeusi) anayefatia ni Mkurugenzi wa African Child Projects, Catherine Kimambo baaada ya kusaini mkataba wa makubaliano baina ya mashirika hayo mawili kushirikiana katika mradi wa ‘Scale Up!’ wenye lengo la kuongeza ufaulu wa wanafunzi mashuleni kwa kupunguza changamoto zilizopo katika nyenzo za ufundishaji kama ukosefu wa vifaa vya kisasa vya kidigitali, uhaba wa walimu.