Na Fresha Kinasa,TimesMajiraOnline,Mara.
MJUMBE wa Baraza kuu la Umoja wa Wanawake Tanzania(UWT)Taifa, Mkoa wa Mara ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) Mkoa huo Rhobi Samwelly,amewataka Wananchi wa Wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara Kuwachagua Wenyeviti wa mitaa,Vijiji na Vitongoji wanaotokana na CCM kwani wanayo sehemu sahihi ya kupeleka changamoto za Wananchi na zikatatuliwa kikamilifu.
Ameyasema hayo Novemba 23,2024, Wakati wa uzinduzi wa Kampeni za kuwanadi wagombea wa nafasi za Uenyekiti wa Vitongoji vya kata ya Morotonga Wilayani humo.
Amesema serikali iliyopo madarakani inaongozwa na CCM ambayo imekuwa ikitoa fedha nyingi za Maendeleo kwa wananchi. Hivyo Kuwachagua Viongozi wanaotokana na Chama hicho ni kuongeza ufanisi wa Serikali kuwahudumia Wananchi kutokana na muunganiko bora kuanzia ngazi za juu hadi chini.
“Tusichanganye kuchagua Viongozi ambao hawana muunganiko na Serikali, watakuwa hawawezi kuwafuata hata Viongozi waliochaguliwa kupitia CCM wakiwemo madiwani na Mbunge ambao wanatokana na CCM kufikisha kero za Wananchi zilizopo katika Vijiji vyao.” amesema Rhobi.
Pia, Rhobi amewataka wanaccm na vyama vyote Kuiamini na kuiunga mkono Serikali ya CCM kwa asilimia 100 kwani imefanya maendeleo makubwa katika nyanja za kiuchumi na kijamii maeneo ya vijijini na mijini.
Pia,amewahimiza kudumisha amani wakati wote wa kampeni kwa kunadi sera na kutotumia lugha chafu kama ambavyo baadhi ya wagombea wa upinzani wanafanya.
Kwa upande wake Katibu Mwenezi wa CCM Wilaya ya Serengeti Robert Chacha amesema kuwa Wilaya hiyo inajumla ya Vijiji 78, ambapo Kati ya Vijiji hivyo ni Vijiji 9 pekee ambavyo vyama vya upinzani vimesimamisha wagombea na matarajio kwa CCM ni kushinda Vijiji vyote na vitongoji.
“Vijiji 69 tayari hatuna upinzani, tunakwenda kuchuana katika Vijiji 9 pekee na vyama vingine, kutokana na maendeleo yaliyofanywa na Serikali tunao uhakika wa kushinda kwa kishindo cha msingi tushikamane na kuwapigia wagombea wa Chama cha Mapinduzi siku ya tarehe 27, Novemba 2024.”amesema Chacha.
Naye Justine Abwao Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Serengeti amewataka wagombea ambao kura zao hazikutosha katika uchaguzi wa kura za maoni za kuwapata wagombea ndani ya Chama Cha Mapinduzi, washikamane na waliochaguliwa ili kurahisha ushindi wa kishindo.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato