April 16, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mjumbe UWT Taifa awataka vijana kutokubali kutumika kuvuruga amani

Fresha Kinasa, TimesMajira Online Mara.

MJUMBE wa Baraza kuu la (UWT) Taifa Mkoa wa Mara Rhobi Samwelly, ametoa wito kwa Vijana nchini kujitambua na wasikubali  kutumika vibaya na watu wenye nia ovu kuvuruga amani  iliyopo nchini hasa kuelekea uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwaka huu.

Ameyasema hayo leo Aprili 9, 2025 wakati akizungumza katika Mahafali ya 54 ya Wahitimu wa kidato cha sita katika shule ya Ufundi ya Musoma. Ambapo Wazazi,  walezi na Viongozi mbalimbali wa serikali walihudhuria.

Rhobi amesema kuwa,Watanzania wameendelea kuishi kwa upendo,umoja,amani na mshikamano hivyo tunu hizo lazima ziendelezwe. Na vijana wakiwemo Wasomi  katika vyuo mbalimbali wanalojukumu la kuilinda amani isivurugwe kwani ndio Msingi wa Maendeleo yaliyopo hapa nchini.

“Taifa letu mwaka huu litafanya uchaguzi, niwaombe Vijana  mnaohitimu  msikubali kutumiwa na Wanasiasa  wenye nia ovu  kuvuruga amani kwa matakwa yao  binafsi mtakakokwenda.  Mmesoma kwa utulivu kwa sababu kuna amani, shughuli za maendeleo zinafanyika nchini  kwa sababu ya amani ambayo imelindwa na kuimarishwa kikamilifu.”amesema Rhobi. 

Pia amesema, jukumu la kutunza amani iliyopo nchini lazima liendelee kufanywa na Watanzania wote kama mboni ya jicho. Huku pia akiwaomba kuendelea kuiamini serikali inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani miradi mingi ya maendeleo imetekelezwa ikigusa huduma za Jamii na miradi ya Kimkakati kwa Maendeleo ya nchi.

Katika hatua nyingine, Rhobi amewahimiza  Wazazi na walezi kuwasomesha Watoto wa kike na watoto wa kiume kwa usawa kwani wote wana nafasi kubwa ya kuleta maendeleo katika Jamii.Huku akisema vitendo vya ukatili wa Kijinsia viendelee kukemewa kwani havifai katika Jamii.

“Wazazi  na walezi wasomesheni Watoto wote wa kike na wa kiume. Mila na desturi kandamizi ziachwe ukiwemo ukeketaji,  ndoa za utotoni na manyanyaso mengine hayafai” amesema Rhobi. 

Kwa upande wake Afisa Elimu  Sekondari Manispaa ya Musoma Avit Aveline Malya amesema anamatarajio kuwa, wanafunzi hao  wanaohitimu  watafanya  vizuri katika mitihani yao ya kuhitimu kidato cha sita. Huku pia  akishukuru Wazazi na  walezi wa Wanafunzi hao kuwasimamia na kuwapa mahitaji yao hadi kufika kidato cha Sita.

Pia, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kufanya ukarabati mkubwa na maboresho katika shule hiyo Jambo ambalo limesaidia kwa kiwango kikubwa kupunguza changamoto za miundombinu shuleni hapo. 

Akisoma risala ya shule  hiyo, Mkuu wa shule ya Musoma Ufundi Magita Nyangore  amesema kuwa, shule hiyo inajumla ya wanafunzi 1249, ambapo Kati yao  wanafunzi 474, ni wanaosoma kidato cha kwanza hadi cha nne, na wanafunzi 775 wanasoma  kidato cha Tano na Sita wakisoma Tahasusi mbalimbali. 

Pia amesema,  Wanafunzi 147 ni wenye ulemavu wa aina mbalimbali wakiwemo Walemavu wa  ngozi, usonji, uoni, huku akisema  Vijana wanaohitimu kidato cha sita mwaka huu ni  453 na  wameandaliwa vyema kitaaluma,kiroho, kiakili na pia watakuwa tegemeo kwa Taifa kwani wamepikwa vyema.