Na Penina Malundo,timesmajira
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema, amefanya ziara ya kukagua miradi ya kimkakati katika Halmashauri ya wilaya ya hiyo na kueleza kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Shule Mpya ya Sekondari ya Mmangu iliyopo Salawe wilayani humo.
Mjema amefanya ziara hiyo leo, akiwa ameambatana na Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Nice Munissy, Mwenyekiti wa Halmshauri Ngassa Mboje, wataalam, pamoja na viongozi wa Serikali na Chama Cha Mapinduzi CCM.
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa Madarasa Matatu katika Shule Mpya ya Sekondari Mmangu iliyopo Salawe wilayani humo, amesema hajafurahishwa na kasi ya ujenzi wake, ambapo kwa sasa ndiyo wanapima msingi, huku wakisaliwa na mwezi mmoja madarasa hayo yawe yameshakamilika.
“Nimefurahishwa na wananchi wa kijiji hiki cha Mmangu kujitoa kujenga Madarasa Sita kwa ajili ya kuanzisha shule mpya ya Sekondari, na sasa Rais Samia Suluhu Hassani ametoa Sh.milioni 60 kwa ajili ya ujenzi wa Madarasa matatu katika shule hii, ambayo yana takiwa Novemba 30 yawe yameshakamilika,”amesema Mjema
“Kasi ya ujenzi wa Madarasa haya sijaridhika nayo, ambapo nilitaka nije kuona tena maendeleo yake baada ya wiki mbili, lakini nitakuja baada ya wiki moja kuona hatua ilipofikia, ili kama kuna tatizo mahali tuongeze nguvu”ameongeza.
Aidha akiangalia maendeleo ya ujenzi wa kituo cha Afya Salawe, napo aliagiza kasi iongezeke, ili ujenzi huo ukamilike kwa wakati na kutoa huduma ya matibabu kwa wananchi, huku akimpongeza Rais Samia Suluhu Hassani kwa kutoa fedha za miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani humo kiasi cha zaidi ya Sh.bilioni 26.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Nice Munissy, amemwahidi mkuu huyo wa Mkoa, kuwa maelekezo yote ambayo ameyatoa atayafanyia kazi ili kuhakikisha ujenzi wa Majengo katika kituo hicho cha Afya Salawe na vyumba vya Madarasa shule ya Sekondari Mnangu unakamilika kwa wakati.
More Stories
Wanaoficha watoto wenye ulemavu kusakwa
Mawakili Tabora walaani kuziwa kutekeleza majukumu
RC Mrindoko:Ufyekaji wa mahindi Tanganyika si maelekezo ya serikali