KATIKA siku za hivi karibuni Serikali imeanza kuja hadharani kuelezea mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu tano inayoongowa na Rais John Pombe Magufuli.
Awali mafanikio hayo yalianza kuelezwa na aliyekuwa Mkurugenzi wa Habari Nchini na Msemaji Mkuu wa Serikali ambaye kwa sasa ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abasi.
Dkt.Abasi alifafanua vizuri mafanikio na mipango ya Serikali ambapo aligusia mafanikio yaliyopatikana katika kila sekta ambapo alisema Serikaii imefanya kazi na mageuzi makubwa katika kuboresha huduma kwa wananchi wake.
Muda mfupi baadaye ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(OR-TAMISEMI) kupitia Waziri wake Seleimani Jafo ilitaja mafanikio makubwa sita yaliyopatikana kuwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu, mpango wa elimu bure,ukusanyaji wa mapato,ujenzi wa viwanda vidogo, ujenzi wa miradi mikakati, ujenzi wa miundombinu ya barabara na Mradi wa mabasi yaendayo kasi.
Aidha alibainisha kuwa Serikali pia imefanya vizuri kwenye ujenzi wa hospitali za wilaya na vituo vya afya pamoja kuboreka kwa huduma za afya
Alisema kabla ya uongozi wa Rais Magufuli kulikuwa na vituo vya afya 115 lakini kwa sasa Serikali imejenga vituo3 52 ambavyo vina uwezo wa kufanya upasuaji.
Pia zimejengwa hospitali za wilaya 69 na mwaka huu wa fedha zitajengwa zingine 27 kupitia utaratibu wa “force account” alisisitiza Waziri Jafo.
Alikwenda mbali zaidi ambapo alitolea mfano wa hospitali zilizopo mkoani singida kuwa zimekuwa zikitoa huduma bora zaidi katika kipindi cha sasa ukilinganisha na awali.
Mbali na Mkoa wa Singida kupongezwa kwa hospitali na vituo vya afya kutoa huduma bora kumekuwa na mikakati madhubuti ya kuboresha afya za wanachi ambayo imebuniwa katika ngazi ya Mkoa na kutekelezwa katika Halmashauri zote za wilaya katika mkoa huo ambayo imeleta mafanikio makubwa.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Rehema Nchimbi anasema baadhi ya mikakati iliyobuniwa na kutekeleza katika kipindi cha awamu hii ni pamoja na suala la lishe bora kwa watoto na utoaji wa elimu na taulo ya mtoto wa kike.
Anasema suala la lishe bora ni suala ni kipaumbele cha kwanza ambalo limewekewa mkakati madhubuti ili kuboresha afya za watoto na wananchi kwa ujumla.
Anaongeza kuwa kutokana na suala hilo kuwa kipaumbele tayari alishaweka utaratibu wa kusainiana mkataba kila mwanzo wa mwaka na kila Mkuu wa Wilaya kwenye Mkoa wake ambapo baada ya kumaliza mwaka tathimini inafanyika na hatua stahiki zinachukuliwa kulingana na utekelezaji.
Dkt.Nchimbi ambaye amekuwa maarufu kwa jina la mama lishe katika Mkoa wa Singida anasisitiza“Tumeamua kufanya hili kwa dhati na hatuna mchezo kabisa kwenye jambo hili kwa kuwa lishe ni kila kitu, lishe ndiyo inatupa utambulisho wa taifa letu ”
Anaelekeza watendaji wote wa Serikali katika Mkoa wa Singida kuwa wa kwanza kujitafakari kuhusu lishe kabla ya kuwaambia wananchi.
Anasema mkoa umekuwa ukishirikiana na wadau mbalimbali kwenye eneo la uboreshaji wa huduma za lishe kwa lengo la kuimarisha afya ya uzazi kwa mama na mtoto .
Anasema kuanzia mwaka 2016 mkoa kwa kushirikiana na Shirika la World Vision kupitia Mradi wa ENRICH wamefanya vizuri kwenye suala la lishe
Anasema mradi ulilenga kwenye uboreshaji huduma za lishe katika kuimarisha afya ya uzazi kwa mama na mtoto ili kuchangia kupunguza maradhi na vifo kwa mama na mtoto vinavyosababishwa na sababu za kilishe katika mkoa wa Singida na Shinyanga.
“Hii ni kwa njia ya utekelezaji wa hatua za gharama nafuu za lishe bora ambazo ni pamoja na kuimarisha mfumo wa afya, kuendeleza mazao yaliyorutubishwa kibailojia, kuhamasisha ushiriki wa wanaume na kushuhulikia moja kwa moja utapiamlo ndani ya siku 1000 za kwanza za maisha ya mtoto,” anaongeza Dkt.Nchimbi.
Kwa mujibu wa matokeo ya utafiti wa ENRICH kwenye vipengele vitatu vilivyofanyiwa utafiti ambavyo ni afya na lishe, jinsia na uchechemuaji na kilimo kupitia viashiria mbalimbali kumekuwa na ufanisi mkubwa ukilinganisha na awali kabla ya kuanza kwa mradi huo.
Kwa upande wa utoaji wa elimu ya jinsia na utoaji wa taulo za watoto wa kike shuleni Dkt.Nchimbi anasema mkoa kwa kushirikiana na Halmashauri zote umeanzisha kampeni maalum ili kuboresha afya na elimu kwa watoto wote katika Mkoa wa Singida.
Anasema tafiti mbalimbali zimeonyesha kuwa wanafunzi wa kike hapa nchini wamekuwa wakitoroka shuleni wanapokuwa kwenye hedhi na hivyo kushindwa kufaulu katika mitihani yao ya mwisho.
Kwa mujibu wa Mtandao wa Jinsia Tanzania(TGNP) wanafunzi wa kike wamekuwa wakitoroka shuleni kwa siku 60 ndani ya mwaka wanapokuwa kwenye hedhi.
Aidha utafiti wa mwaka 2010 wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) unaonyesha kuwa kati ya wanafunzi 10 Afrika, mwanafunzi 1 hutoroka shuleni katika kipindi cha hedhi.
Dkt.chimbi anasema katika kampeni hizo moja ya kifaa muhimu kinachopiganiwa zaidi katika kuhakikisha uwepo wa hedhi salama ni upatikanaji wa taulo zenye ubora za kike ambapo amesema mkoa wake umefanya ni kipaombeele kupitia kampeni yake ya “Mjali mtoto wa kike kwa maendeleo yake na taifa”
Katibu Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Angelina Lutambi anasema juhudi hizi za Serikali za kuboresha upatikanaji wa hedhi salama kwa kuwapatia watoto wa shule taulo bora za kike zinaenda sambamba na lengo namba 5 la malengo ya maendeleo endelevu (SDGs) kipengele cha 5.6 kinachohimiza afya ya uzazi, tendo la ndoa na haki za uzazi ambapo ni pamoja na masuala ya hedhi.
Akizindua kampeni maalum ya uchangishaji wa taulo za mtoto wa kike katika Mkoa wa Singida lililopewa jina la “Mjali mtoto wa kike kwa maendeleo yake na Taifa lake”wilayani Ikungi hivi karibuni Dkt.Nchimbi ametoa rai kwa wadau wote kushiriki kikamilifu katika kuwabaini na kutoa taarifa za wafanyabiashara watakaojaribu kuuza taulo zisizo na ubora ili kuwalinda watoto wa kike .
Aidha ametoa onyo kali kwa wawekezaji na wafanyabiasha wa kutengeneza na kuuza taulo za watoto wa kike kuacha mara moja tabia ya kutengeneza taulo sizizo na ubora kwa kuwa mkoa wake tayari umeanzisha msako wa kiintelijensia wa kuzisaka taulo zisizo na ubora ambapo atakayebainika sheria itachukua mkondo wake mara moja.
Anasema kutokana na juhudi za mageuzi makubwa ya kiuchumi yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli nchi yetu imekuwa katika mashindano ya kiuchumi duniani hivyo mikakati madhubuti ya kudhibiti ubora inahitajika katika kipindi hiki kuliko kipindi kingine chochote.
Anasema vyombo vya dola, viongozi wa dini na wazazi wanamchango mkubwa katika kumlinda mtoto wa kike kwa ustawi wa taifa letu.
“Ndiyo maana tunasema na tunamaanisha kuwa tunataka kujua mipango ya udhibiti wa ubora kwa watengenezaji hawa kwa kuwa majuto ni mjukuu, tusisubiri kufika huko,” anasisitiza Dkt.Nchimbi.
Anaongeza kuwa ubora wa taulo za kike ni ubora wa maisha yao hivyo ni muhimu kuchukua hatua za kudhibiti mnyororo mzima wa uzalishaji na usambazaji wa taulo sizizo kuwa na ubora.
Anatoa wito wa wajasiriamali kuja na andiko zuri la utengenezaji wa taulo bora za kisasa zitakazotengenezwa kwa kutumia malighafi za hapa nchini ambapo anasema atamzawadia tuzo la shilingi milioni moja.
Anawataka watoto wa kike kote nchini wajiamini kwa kuumbwa wanawake na kwamba hedhi ni kitu cha thamani kwa kuwa hedhi ni uhai ambapo alisisitiza elimu ya jinsia na mtoto wa kike kutambua mabadiliko ya miili kuendelea kutolewa ili kuwajenga watoto wa kike kujua thamani ambayo Mungu amewajalia kwa kuwaumba wakamilifu.
Wadau wote kuendelea kuchangia kwa kutambua thamani ya mtoto wa kike ambapo katika uzinduzi huo lengo lilikuwa ni kuchangia paketi 8000 za taulo za kike lakini zilipatikana jumla ya 9089 kulingana na fedha zilizotolewa.
Aidha malengo jumla kwa mwaka 2020 katika Wilaya ya Ikungi ni kuchangia taulo 192,000 kwa watoto wote wa kike kwenye shule 36 za Sekondari, na shule 131 za Msingi zenye jumla ya watoto wa kike 16,000
Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Dkt.Angelina Lutambi alisisitiza kuwa Serikali imeendelea kutoa kipaumbele katika huduma za afya zenye ubora na zinazowafikia wananchi wote ili kuboresha afya zao.
Dkt.Lutambi anasema Serikali inatambua umuhimu wa afya bora kwa wananchi wake kwani afya bora ni rasilimali muhimu kwa maendeleo. Maendeleo ya Taifa letu la Tanzania yataletwa na wananchi wenye afya na wenye uwezo wa kuzalisha mali. Katika kuhakikisha kuwa wananchi wana afya bora, Serikali imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kutoa huduma za afya kwa kuzingatia sera na miongozo iliyopo.
Dkt.Nchimbi alipongeza uongozi wa Halimashauri ya Wilaya ya Ikungi kwa kuratibu kwa ufanisi kampeni hiyo na kuhakikisha kuwa imeanza utekelezaji wake kwa umakini mkubwa ambapo anasema kufikia mwisho wa mwaka huu Halmashauri zote ziwe zimekamilisha utekelezaji wa Kampeni hii .
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Justice Kijazi alimshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kubuni wazo la kampeni hiyo na kutaka Halmashauri zote katika mkoa wa Singida kulitekeleza kwa vitendo.
Anasema kutoa elimu ya jinsia shuleni na kuwachangia watoto wa kike taulo jambo lenye manufaa kwa taifa kwa kuwa ukimuelimisha mtoto wa kike umeelimisha taifa zima ambapo alimhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa litakuwa endelevu.
“Nikuhakikishie Mkuu wa Mkoa kwa kushirikiana na wadau chini ya uongozi wako na Mkuu wangu wa Wilaya tunakwenda kuwakomboa watoto wa kike katika Wilaya yetu kwa kuwapa elimu hii” anasema Kijazi.
Kijazi anasema tayari Halmashauri yake ilishaanza utekelezaji wa kampeni hiyo kwa kutoa elimu za jinsia kwa watoto wa kike katika shule zote na kwamba elimu hiyo imewafanya watoto wa kike kujiamini na kuongeza ufaulu katika mitihani yao.
Alizitaja baadhi ya changamoto zinazowakabili watoto wa kike kuwa ni pamoja na mimba za utotoni,kubakwa,kuozeshwa katika umri mdogo na kufanyishwa kazi nyingi nyumbani ambapo amesema kwa kazi ambayo inaendelea changamoto hizo zinaendelea kupungua siku hadi siku.
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Edward Mpogolo aliwataka wadau mbalimbali wajitokezee kuchangia taulo za kike ili kuwahifadhi wanafunzi wa kike ili waweze kuhudhulia masomo yao kikamilifu.
“Ndugu zangu hima tujitokeze kuchangia taulo za watoto wa kike, kwani kwa sasa ni bidhaa kama zilivyo bidhaa nyingine sisi kama wazazi tuna wajibu wa kuwanunulia watoto wetu kama mahitaji mengine,” anasema.
Mratibu wa program hii ya uchangiaji wa taulo za mtoto wa kike ambaye pia ni Afisa Maendeleo wa jamii wilaya ya Ikungi Haika Massawe alipendekeza wazazi wahusishwe kikamilifu katika program hii.
Anasema vyombo vya Serikali kama Polisi na mahakama vitende haki katika kushughulikia haki za mtoto wa kike aidha wazazi wa wanafunzi wa kike mashuleni waelekezwe kutoa fedha maalum kwa ajili ya kununua taulo za watoto wao.
Akitoa ushuhuda kwa niaba ya wanafunzi wenzake wa jinsi ambavyo mtoto wa kike amekuwa akinyanyasika kwa kukosa huduma ya taulo za kike , Esther Chacha Mwanafunzi wa Sekondari ya Ikungi alisema wanafunzi wengi wamekuwa wakidhalilika wanapopatwaa na siku zao za hedhi wakiwa shuleni wakika hawajavaa taulo hizo na kuiomba serikali kuendelea kuwasaidia kwa kuwapa taulo hilo.
More Stories
Siri ya Rais Samia kutembea kifua mbelea kijivunia Mapinduzi Matukufu ya Z,bar
Rais Samia anavyotimiza ahadi yake ya kumtua ndoo ya maji mwanamke
Rais Samia anavyozidi kusogeza karibu watoto wa kike na kasi ukuaji teknolojia