March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mixx by Yas yaja na Kampeni ‘Kila hatua Mixx’

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

MIXX by Yas, imezindua rasmi Kampeni maalum iitwayo ‘Kila Hatua Mixx’, inayolenga kutoa suluhisho la utatuzi wa changamoto mbalimbali za kifedha ili kuhakikisha wote wanafikia malengo bila ya kikwazo cha fedha.

Kampeni hiyo inahamasisha Watanzania kugeuza kila hatua ya matumaini kuwa hatua ya maendeleo. Ni hadithi ya mshikamano, uvumilivu na mafanikio, wakisafiri pamoja kutoka kwenye ndoto hadi ukweli.

Akizungumza katika hafla fupi ya uzinduzi wa Kampeni hiyo, iliyofanyika jana katika Hotel ya Serena, jijini Dar es Salaam, Afisa Mtendaji Mkuu wa Mixx by Yas, Angelica Pesha amesema ni historia kubwa wameandika katika safari ya Mixx kuchochea ujumuishwaji wa kifedha hapa nchini.

“Tangu safari yetu ya utoaji huduma za kibunifu na zinazozingatia mahitaji ya watanzania ianze mwaka 2010 mpaka leo, tunajivunia mchango mkubwa na alama tunayoendelea kuiweka kwenye sekta ya fedha ikiwemo kuchochea Uchumi wa kidigitali.

“Tunawezesha watanzania zaidi ya milioni 20 kufanya miamala mbalimbali ya kifedha ya takribani shilingi trilioni 6 kwa mwezi.

“Kupitia fursa za uwakala wa huduma za kifedha tunatoa ajira zisizo za moja kwa moja kwa mawakala zaidi ya 200,000 nchi nzima,” amesema Pesha.

Vile vile, amesema mifumo yao ya kifedha inawezesha wafanyabiasha zaidi ya 500,000 kupokea malipo ya bidhaa na huduma kidigitali.

Pia, makampuni binafsi Pamoja na taasisi za umma zaidi 3,000 kukusanya na kufanya malipo ya mkupuo kwa wabia/suppliers na wafanyakazi wao.

Aidha, amesema wamewezesha wateja zaidi ya milioni 6 kupata huduma za mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 1 hivyo kufanya malengo yao kutimia.

Aliongeza kuwa, kuchochea utamaduni wa kuweka akiba miongoni mwao wamewezesha watanzania kuweka akiba zenye thamani ya zaidi ya bilioni 600.

“Haya yote yamewezeshwa na maono, mikakati na nia yetu ya dhati ya kuchochea ujumuishwaji wa kifedha kwa watanzania wote.

“Tunawashukuru wateja, washirika wetu na wadau mbali mbali wa sekta ya fedha na mawasiliano ambao wamekuwa nasi katika safari hii iliyojaa mafanikio na mchango chanya kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla,” amesema.

Hata hivyo amesema, Mixx wamejipanga kuendelea kubuni mikakati ambayo itachochea upatikanaji na utumiaji wa huduma za kifedha ikiwemo huduma za Mikopo, kuweka akiba, bima, uwekezaji n.k ili kuhakikisha kuwa wanakuwa na Tanzania ambayo kila mtu anafikia malengo yake bila kuwa na kikwazo cha kifedha.

Mixx by Yas wanaamini teknolojia ni nguzo muhimu ya kufikisha huduma za kifedha maeneo mengi hapa nchini ikiwemo kuyafikia makundi maalumu kama vijana na wanawake.