Na Mwandishi wetu, Timesmajira
Dhamira ya Serikali ya kuwasaidia wachimbaji Wadogo wa Madini nchini kwa kuwawezesha kupata taarifa sahihi za miamba kupitia Mitambo ya Uchorongaji (drilling rigs) ili wachimbe kwa tija imetimia baada ya huduma hiyo kuanza kuwanufaisha baadhi ya wachimbaji walioanza kuitumia.
Serikali kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ilinunua jumla ya mitambo mitano (5) kwa ajili ya wachimbaji wadogo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 9.1 ambayo ilizinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan Oktoba 21, 2023 Jijini Dodoma. Mitambo hiyo ilinunuliwa kwa ajili ya shughuli za utafiti wa madini kwa wachimbaji wadogo inayowasaidia kupata taarifa sahihi na za kina ili wachimbe kwa uhakika pasipo kubahatisha.
Akizungumza na Maafisa Habari kutoka Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Madini waliowatembelea hivi karibuni na waliotaka kujua manufaa ya mashine hizo kwenye shughuli za uchimbaji mdogo, mnufaika wa huduma za uchorongaji kwa kutumia mashine hizo, Mhandisi Rodgers Sezinga amesema ujio wa Rig hizo umesadia wachimbaji ikiwemo yeye mwenyewe kupata taarifa za uwepo wa madini katika maeneo yao kwa kutambua umbali na kiwango cha madini kilichopo katika eneo husika na hivyo kupelekea kuzalisha kwa tija.
‘’Ninatoa wito kwa Serikali kuongeza mashine nyingine aina ya Reverse Circulation (RC) ambayo ina kasi zaidi ili kuwafikia wachimbaji wengi kwa muda mfupi kuliko ilivyo sasa. Lakini pia ninaiomba Serikali iwasogezee wachimbaji vifaa vya Jiofizikia ili kubaini muelekeo wa miamba yenye viashiria vya madini kabla ya kuchoronga ili kuepusha epotevu wa mitaji kwa wachimbaji wadogo,’’ amesema Mhandisi Senziga.
Naye, Mwenyekiti Mstaafu wa Wachimbaji Wadogo wa Mkoa wa Geita Christopher Kadeo ameipongeza Serikali ya awamu ya Sita kwa kuona umuhimu wa kuwasaidia wachimbaji wadogo kwa kupeleka huduma hiyo ambayo inaepusha upotevu wa mitaji na kuwasaidia wachimbaji wadogo kuchimba kwa uhakika.
Kadeo ametoa wito kwa Serikali kuongeza mashine hizo kwa wingi katika maeneo mbalimbali ya uchimbaji madini nchini kwa lengo la kuwasaidia wachimbaji wadogo kupata taarifa za uwepo na mwelekea wa miamba ya madini katika maeneo yao ili kuchimba kwa uhakika.
Kwa upande wake, Msimamizi wa timu ya uchorongaji Lwamgasa kutoka STAMICO Mjiolojia Nachindala Kazingumbe, amesema mitambo hiyo ni kwa ajili ya kuchoronga na kuchukua sampuli chini ya ardhi na kuzipima ili kubaini kama kuna viashiria vya madini, ambazo zinatoa taarifa za kiaalamu kuliko zile za jadi.
Kazingumbe ameongeza kwamba, mitambo hiyo ina uwezo wa kuchimba mita 400 ambapo hutumia takriban siku sita kutegemea aina ya Mwamba katika eneo la uchorongaji na ametoa wito kwa wachimbaji wadogo kutumia huduma za uchorongaji kwa ajili ya kubaini uwepo wa madini katika maeneo yao ya uchimbaji kabla hawajaanza shughuli hiyo kwa lengo la kuepusha upotevu wa mitaji.
“Serikali inatoa huduma za uchorongaji bure kabisa, isipokuwa mchimbaji au mnufaika atalazimika kulipa gharama za uendeshaji ikiwemo mafuta na posho ya wafanyakazi ambayo inakadiwa kwa mita 100 ni shilingi milioni 10.8,’’ amesema Mjiolojia Kazingumbe.
Hadi sasa wachimbaji wadogo 23 wamefanyiwa uchorongaji na zaidi ya mita Elfu Sita Mia Tisa Ishirini na Tisa zimechimbwa. (6,929). Gharama inayotozwa na STAMICO ni nafuu ikitoa fursa zaidi kwa wachimbaji kutumia huduma hiyo. Kwa sasa wachimbaji wadogo wanatozwa wastani wa shilingi Milioni 10,801,252.12 kwa mita 100 badala ya shilingi Milioni 22,758,750 ambayo ni bei ya Soko. Punguzo hilo ni sawa na punguzo la zaidi ya asilimia 50.
Aidha, mbali na mitambo hiyo, STAMICO ipo mbioni kuongeza tena mitambo mingine 10 ya uchorongaji ambayo muda wowote itawasili nchini huku baadhi ikitengwa kwa ajili ya wanawake na vijana. Huduma hizi zitawasaidia kuongeza tija na kupunguza hasara zisizo za lazima.
More Stories
Benki ya NMB yahudhuria Mkutano wa CSSC
Upungufu wa viti,meza vyamnyima usingizi Diwani
PPP kuibua miradi ndani ya Mikoa 12