January 4, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mitambo ya kutengeneza barabara,magari ya kuzolea taka kupunguza gharama kwenye halmashauri

Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza

MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Wakili Kiomoni Kibamba amesema uamuzi wa kununua mitambo ya kutengeneza barabara na magari ya kuzoa taka utapunguza gharama za uendeshaji wa halmashauri.

Pia Halmashauri hiyo imetenga bajeti ya milioni 198 kukamilisha Hospitali ya Wilaya hiyo ili ianze kuwahudumia wananchi ifikapo Desemba mwaka huu baada ya miundombinu mbalimbali kukamilika.

Wakili Kibamba ametoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela baada ya kuwasilisha taarifa ya makusanyo na utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika kikao cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2023/24.

Amesema Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kununua na kumiliki mitambo yake inalenga kutengeneza na kuboresha barabara zake za vumbi na kupunguza gharama inazowalipa wakandarasi,inatafuta mzabuni wa kuleta mitambo hiyo itakayogharimu zaidi ya bilioni 4 fedha kutoka mapato ya ndani.

Pia,Wakili Kibamba amesema halmashauri hiyo inatumia kiasi cha milioni 581 kwa mwaka kumlipa mzabuni wa kuzoa taka katika maeneo mbalimbali ya manispaa hiyo,hivyo watanunua malori ya kukusanya taka ili fedha nyingine zikatumike kufanya maendeleo ya wananchi.

Mkurugenzi huyo wa Ilemela amesema kuwa mapato halisi bila mauzo ya viwanja ni bilioni 8 na asilimia 60 ya fedha hizo ndizo zinakwenda katika maendeleo, kwa kuwa maendeleo ni mchakato changamoto bajeti ya mwaka huu ni fedha wamekumbana na viporo vya miradi ya miaka ya nyuma.

“Nataka tufanye maendeleo ya haraka sana lakini hoja ya kuongeza vyanzo vya mapato bajeti haikuwa na uhalisia,mfano eneo la stendi ya Nyamhongolo yalikuwa juu wakati makusanyo ni milioni 40,”amesema.

Pia Halmashauri hiyo itaendelea kuboresha sekta ya elimu ambapo Septemba 30, mwaka huu,ilipokea vitabu 30,364 vyenye thamani ya milioni 118.1 kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) ili kuweka uwiano wa kitabu kimoja kwa mwanafunzi mmoja wa shule za sekondari.

Kwa mujibu wa Wakili Kibamba tawi la Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) kitajengwa Kata ya Kiseke,kupitia mradi wa Higher Education for Economic Transformation-HEET) utakaogharimu takribani bilioni 4.77 za mkopo kutoka Benki ya Dunia.