Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
MSHINDI wa taji la Miss Tanzania 2020, Rose Manfere ameshiriki zoezi la kupanda miche milioni 1 ya miti lililoandandaliwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania – TFS kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza katika shamba la gereza la Wazo Hill jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuadhimisha sherehe za miaka 59 ya Uhuru .
Shughuli hiyo iliongozwa na Meneja Rasirimali Misitu Tanzania, Dkt Abel Masota pamoja mkuu wa gereza la Wazo Hill Ipyana Mwakyusa, wadau wa mazingira pamoja na waratibu wa Miss Tanzania.
Dkt. Masota amesema, Serikali imeagiza sherehe za Uhuru zitumike katika kufanya shughuli za kijamii na wao wameamua kupanda miche 1,300 kati ya hiyo 1,000 ya misaji ambayo inatoa mbao ngumu na iliyobaki ya matunda mbalimbali.
“Tukishirikiana na uongozi wa magereza, wadau wa mazingira na Kamati ya Miss Tanzania tumeamua kupanda miche hii ya misaji ili siku za usoni iende kuwasaidia wenzetu katika shughuli zao za ujenzi na hata biashara. Serikali ina mashamba mawili ya misaji ambayo huuza miti kwa njia ya mnada kila mwezi na sehemu kubwa ya wanunuzi wa mazao haya husafirisha nje ya nchi”.
“Thamani ya miche hii ikikuua ni kubwa sana tuna imani itawanufaisha jeshi la magereza. Tumeona magereza wana eneo kubwa kupanda miche hii na ni wajibu wao sasa kuitunza vizuri kwa manufaa ya baadaye, na ndio maana pia tumeamua kutoa elimu ya namna bora na hatua zinazotakiwa kufuatwa katika upandaji wa miche hadi kustawi ” amesema Dtk. Masota.
Kwa upande wake, Miss Tanzania, Rose amesema kuwa, kupitia shughuli hiyo amejifunza namna ya kupanda miti na hatua zinazotakiwa kufuatwa huku akiwataka wananchi kujenga utamduni wa kuithamini misitu.
“Somo nililolipata leo juu na namna bora ya upandaji miti na hatua zake ili kuifanya istawi nitakwenda kuiendeleza kwa jamii ili kutambua thamani ya miti na utunzaji wa mazingira lakini pia kuitumia kama biashara pale watakapoivuna na kujiongezea kipato,” amesema mlimbwende huyo ambaye aliambatana na Mratibu wa mashindano ya Miss Tanzania, Basila Mwanukuzi.
Kwa upande wake, mkuu wa gereza hilo, Mwakyusa amesema, kitendo cha uongozi wa TFS kupanda miche hiyo katika shamba lao ni fursa kubwa kwao na kuahidi kuitunza vyema ili iwaletee manufaa kwa siku za baadaye.
“Hapa tuna wataalamu wa kilimo na mifugo tutahakikisha tunaisimamia ipasavyo ikiwemo kuitunza na kuimwagilia lengo ni kuhakikisha inatusaidia kwa siku za usoni baada ya kukua,” amesema.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Kinondoni, Stellah Msophe amesema kuwa, katika miche 1300 iliyopandwa ana imani itakuwa sehemu kubwa ya kuboresha mazingira na kama Wilaya wataendelea kuwaunga mkono TFS kwenye uhamasishaji wa upandaji miti.
“Tunashukuru Miss wetu umefika hapa kupanda miti na sisi na hii ikawe chachu kwa vijana popote walipo wapande miti lakini niwataka magereza kuhakikisha miti hii inakuwa kwani nguvu kazi mnayo ili kesho tusione aibu kuwaomba TFS watusaidie tena na tena kuotesha miti,” amesema kiongozi huyo.
More Stories
Watumishi wa Fahari wafanya Bonanza
Rais Samia atia mkono mchezo wa masumbwi Tanzania
Chino bingwa mpya wa IBA Intercontinental Championship