May 18, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Misri yaonesha nia kuwekeza biashara ya nyama nchini

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Katika jitihada za kufungua biashara hususan ya nyama inayotoka Tanzania kwenda nchini Misri, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Kilimo kutoka nchini Misri, Mhe. El Sayed El Kosayer ili kuona uwezekano na kuweka mazingira wezeshi ya biashara hiyo baina ya nchi hizo mbili.

Waziri Ulega alifanya mazungumzo hayo na El Kosayer kando ya Mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Barani Afrika (AGRF) jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.

Pamoja na kujadiliana mambo mengine, suala la biashara ya nyama kutoka Tanzania kwenda kuuzwa nchini Misri lilijadiliwa kwa kina huku El Kosayer akiahidi kulifanyia kazi kwa haraka ili biashara hiyo iweze kuleta matunda kwa pande zote mbili.

Mapema wakati wa mazungumzo yao, Kosayer alimueleza Waziri Ulega kuwa lengo la kukutana kwao ni kuona namna wanavyoweza kuendelea kuimarisha ushirikiano katika kuendeleza sekta za mifugo na uvuvi ili ziweze kuwanufaisha wananchi wa pande zote mbili.