Na Penina Malundo
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt.Doto Biteko, amesema kuwa,Tanzania inachukulia mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika – Misheni 300 kama kichocheo cha utekelezaji wa Sera yake ya Taifa ya Nishati inayolenga kuendeleza nishati endelevu,uhifadhi na ufanisi.
Pia amesema maazimio ya nishati yaliyotayarishwa na nchi 14 yatakuwa ni maazimio ya majaribio ambayo yatakuwa yanatoa mfumo wa utekelezaji wa hatua zilizoratibiwa ili kufungua uwekezaji zaidi.
Ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam,wakati akifungua Mkutano huo wa siku mbili ambao utatoa fursa ya kufanya majadiliano kati ya ngazi ya mawaziri na wadau wa masuala ya nishati na fedha na kesho.
Dkt. Biteko amesema kupitia mkutano huo utakuwa na manufaa kwa kupata umeme wa uhakika na kujadili mambo mbalimbali yanayohusu upatikanaji wa nishati na ufumbuzi wake.
Amesema pamoja na maendeleo ya nishati yaliyopo nchini ,bado nchi inahitaji uwekezaji zaidi katika sekta ya nishati kwani matarajio yake ni kukuza shughuli za kiuchumi hususan katika sekta za viwanda, madini na huduma za ukarimu jambo ambalo linahitaji uwekezaji wa kimkakati zaidi katika sekta ya nishati. Â
“Sera hiyo pia inalenga kuongeza upatikanaji wa huduma za kisasa za nishati na kuongeza mchango wa nishati mbadala katika mchanganyiko wa uzalishaji ili kuimarisha upatikanaji, uhakika na usalama wa nishati,” amesema Dkt. Biteko.
Amesema kuwa, Rais wa Tanzania, Dkt. Samia, Â amekuwa mstari wa mbele kukuza upatikanaji wa suluhisho la nishati safi ya kupikia barani Afrika, jitihada ambazo zimeungwa mkono na mkakati wa kitaifa na kujumuishwa katika Azimio litakalotiwa saini katika mkutano huu, huku akitoa wito wa ahadi na ushirikiano zaidi katika kuboresha upatikanaji wa suluhisho la nishati safi ya kupikia barani mwetu. Â
Aidha, amesisitiza kuwa ifikapo mwisho wa mwaka 2025, uwezo wa Tanzania kuzalisha umeme utaongezeka hadi megawati 4,000, nishati inayotoka kwenye vyanzo safi na mbadala inavyonufaisha wakazi wa vijijini na mijini, huku miundombinu ya umeme ikifikia vijiji vyote 12,318 nchini.

Pia, amesema Tanzania inaimarisha muunganiko wa Afrika kwa kuwa na miundombinu ya umeme inayounganisha nchi za Kenya, Burundi, Rwanda, na Uganda, huku miundombinu ya kuunganisha Zambia ikiwa inaendelea. Â
Ametaja miongoni mwa mambo mengine yatakayofanyika katika mkutano huo kuwa ni kushirikishana uzoefu; kupata ahadi muhimu za kisiasa; kutumia ushirikiano ili kufungua uwekezaji wa sekta binafsi; kuanzisha ushirikiano wa kufadhili miundombinu ya nishati; na kukubaliana mfumo wa ufuatiliaji ikiwa ni pamoja na kuanzisha Kiashiria cha Ufuatiliaji wa Maazimio ili kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa ahadi zilizotolewa kwenye Mkutano huo. Â

Ametoa rai kwa viongozi walioshiriki mkutano huo kutumia fursa hiyo kuhitimisha Maazimio yanayoendana na matarajio ya bara la Afrika ya nishati na kuimarisha ushirikiano unaohitajika katika kuyatekeleza.
“Ni matarajio yangu kwamba, mamlaka zinazohusika za nishati katika kila nchi ya majaribio zitajitahidi kuhakikisha maazimio ya nishati yanafanikishwa kupitia malengo na mipango ya hatua zinazolenga kuongeza kiwango cha upatikanaji wa umeme, matumizi ya nishati safi ya kupikia, nishati mbadala na mchango wa mtaji wa sekta binafsi katika kufanikisha upatikanaji wa nishati”,amesisisitiza Dkt. Biteko. Â
Kwa upande wake Rais wa Benki ya Dunia(WB),Ajay Banga amesema kuwa bara la Afrika linaweza kubadilisha sura ya Afrika kwa kuwa na juhudi za pamoja za kuunganisha rasilimali zilizopo kuhakikisha nishati ya umeme inawafikia wananchi wengi zaidi Afrika ifikapo 2030.
Nae Rais wa Benki ya Afrika (AfDB), Dkt. Akinumwi Adesina ameipongeza nchi ya Tanzania kwa kuwa mfano wa kuigwa kwa kufanya vizuri katika uwekezaji wa miundombinu ya umeme kwa kuwafikishia nishati ya umeme wananchi katika vijijini vyote 12,318.
Mkutano huo umewakutanisha Mawaziri wa Nishati, Viongozi wa Taasisi za Kimataifa za Kifedha, Wataalam na Wadau wa Mashirika ya Kiraia ambao watapata fursa ya kujadili na kukubaliana malengo, vipaumbele vya sera, suluhisho, na ahadi za jinsi ya kutekeleza Mpango wa Mission 300.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba amesema hadi kufikia mwaka 2030 Watanzania wote watakuwa tayari wamefikiwa na umeme kutokana na mipango madhubuti iliyopangwa na Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Amesema kutoka na kampeni ya Rais Samia Suluhu Hassan ya Watanzania kutumia nishati safi ya kupikia kufanikiwa, hivyo suala la umeme pia litafanikiwa kwa kila mtanzania.
Amesema mpaka kufikia mwaka 2030 Serikali ya Tanzania imekusudia kuhakikisha zaidi ya asilimia 75 ya watanzania watakuwa wamepata nishati safi ya kupikia.
Mramba amesema mkutano huu kufanyika hapa ni kama namna nyingine kutambua kazi kubwa ambayo nchi ya Tanzania imeweza kufanya.
”Ni uongozi wa Rais Samia katika nishati ya kupikia ambapo Rais Samia ametambulika Duniani kama ni Champion katika eneo hili la nishati ya kupikia na Tanzania tupo mstari wa mbele katika utekelezaji wa jambo hili.
”Ambapo sisi tumeonekana kuwa miongoni mwa nchi chache tumeonesha mfano ambapo Tanzania tayari imetengeneza mkakati wa utekelezaji wa nishati safi ya kupikia ambapo mkakati unaotoa miaka hadi 2034 kuweza kuwaamisha watanzania wote kutoka katika nishati isiyokuwa safi na kutumia nishati safi,”alisema.
Aidha alisema pia suala la Tanzania kuondokana na mgao wa umeme hili ni suala lingine ambalo Tanzania limetoa ujumbe kwa mataifa mengi ya Afrika juu ya uwezo na dhamira ya serikali ya Tanzania ya kuweza kuwafikishia wananchi wake umeme wa uhakika na kuondokana na matatizo ya changamoto nyingi za umeme.
”Mkutano huu unatuhakikishia mwaka 2030 Watanzania asilimia 100 wataweza kufikiwa na miundombinu ya umeme na wataweza kupata umeme na katika kipindi hicho watanzania ambao umeme umeingia katika nyumba zao wasiwe chini ya asilimia 75,pia katika kipindi hicho tunataka chini ya asilimia 75 wawe tayari wamepata nishati safi ya kupikia,”amesema.
Amesema mkutano huu utawaachia Watanzania wakiwa wametengeneza mahusiano makubwa na wadau mbalimbali sekta binafsi,washirika maendeleo,mabenki pamoja na watafiti.
Mramba amesema katika mpango huu serikali ya Tanzania imekusudia kuunganisha mita mpya milioni8.5 katika miaka mitano ijayo.
More Stories
Tuzo za EAGMA zazinduliwa rasmi
Katibu Mkuu Nishati aipongeza Sweden kufadhili miradi ya umeme nchini
RAS Seneda akabidhi msaada wa Mablanketi kwa wazee na yatima