December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

‘Miongozo na sera za wenye ulemvau haijitoshelezi’

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee, na Watoto, Abeida Rashid Abdallah, amesema kuwa miongozo na sera zinazohusu Watu Wenye Ulemavu kwa sasa hazitoshelezi. Hivyo, kuna haja ya kuangalia upya sera na sheria nyingine ili kuhakikisha kwamba hakuna kundi linaloachwa nyuma katika jamii.

Abeida alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita wakati akifungua mkutano wa programu ya Kimataifa ya Haki za Watu Wenye Ulemavu, uliofanyika katika ukumbi wa Golden Tulip, Uwanja wa Ndege, Unguja. Amesema kuwa Sera ya mwaka 2004 inayohusu Watu Wenye Ulemavu haitoshelezi, hivyo kuna umuhimu wa kupitia upya sera na sheria zingine ili kuhakikisha zinawajumuisha ipasavyo Watu Wenye Ulemavu. Alisisitiza kuwa, kama kuna mapungufu, basi Watu Wenye Ulemavu wanapaswa kupaza sauti zao na kuiambia jamii kuhusu changamoto zinazowakabili kutokana na upungufu uliopo katika sera na sheria za sasa.

“Miongozo na sera ya 2004 inayowahusu Watu Wenye Ulemavu ipo, na kupitia programu hii ya kikao cha leo, inaangaliwa upya. Hili ni jambo la kushukuru, lakini pale tunapoona mapungufu, lazima tuwaoneshe wenzetu nini tunahitaji,” alisemaAbeida.

Aidha,Abeida alisema kuwa muda sio mrefu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto itazindua Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kupambana na Vitendo vya Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto, ambapo mpango huo utazingatia pia masuala ya Watu Wenye Ulemavu.

Pia, aliwasihi Watu Wenye Ulemavu kuweka takwimu zao vizuri, ingawa Serikali inaweka takwimu hizo, lakini ni muhimu kwao wenyewe kuwa na takwimu sahihi ili ziweze kuwasaidia wakati wa kutoa maoni yao.

Mwisho,Abeida alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa uongozi wao na kwa kuzingatia masuala ya Usawa wa Kijinsia na haki za Watu Wenye Ulemavu.

Mapema, akizungumza Mtaalamu wa Ushauri wa Masuala ya Usawa wa Kijinsia,Maja Hansen, alisema kuwa mkutano huo wa Haki za Watu Wenye Ulemavu unalenga kujadili ajenda nne muhimu: Ushiriki na Ushirikishaji, Ulinzi dhidi ya vitendo vya ukatili kwa Watu Wenye Ulemavu, Maboresho ya Sera, na Masuala ya Takwimu. Anaamini mkutano huo utaleta tija.

Kwa upande wake, mmoja wa washiriki wa mkutano huo, Ali Omar Makame kutoka Shirikisho la Jumuiya ya Watu Wenye Ulemavu Zanzibar (SHIJUWAZA), alisema amefurahishwa na hatua ya waandaaji wa mkutano huo kuwashirikisha Watu Wenye Ulemavu. Hii itawapa nafasi ya kueleza changamoto zinazowakabili, ikiwemo ukosefu wa vyoo rafiki kwa baadhi ya majengo ya Serikali na binafsi.