Na Lubango Mleka, TimesMajira Online,Musoma Vijijini.
Serikali imetoa zaidi ya milioni 573 kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari Wanyere Jimbo la Musoma Vijijini ili kupanua wigo na kuongeza ubora wa utoaji elimu jimboni humo.
Wakizungumza wakati mkutano wa hadhara uliofanywa na Mbunge wa jimbo hilo Prof.Sospter Muhongo alipofanya ziara ya kukagua miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi katika Kata ya Suguti baadhi ya wananchi wamebainisha kuwa ujenzi wa shule hiyo mpya utatua tatizo la wanafunzi kutembea umbali mrefu kufuata elimu.
Mmoja wa wananchi hao Mwijarubi Charles, ameeleza kuwa wanafunzi wa kijiji cha Wanyere wanalazimika kutembea zaidi ya kilometa 30 kwenda na kurudi kutoka masomoni kwenye sekondari ya Kata, huku baadhi ya wanafunzi wakiwa wamepanga vyumba na wanajipikia karibu na eneo la shule.
“Tunaishukuru serikali kwa kutupatia fedha za ujenzi wa shule hii mpya ambayo itakuwa mkombozi kwa watoto wetu ,” amesema Mwijarubi.
Kuunga mkono juhudi za serikali za kutatua changamoto katika sekta ya elimu nchini, Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Prof.Muhongo ameendesha harambe ya kuanza ujenzi huo na michango iliyotolewa ni fedha taslimu takribani milioni 2.5.
Saruji mifuko 30 imetolewa na kijiji jirani cha Kataryo Kata ya Tegeruka ambao watoto wao wanasoma katika kijiji cha Wanyere, Wanakijiji wa Wanyere wameanza kuchangia nguvu kazi za kusomba mchanga, mawe, maji na kuchimba msingi wa jengo moja la madarasa mawili na ofisi moja ya walimu.
“Kwanza kabisa niwapongeze wananchi wote kwa ujumla kwa kujitoa kwa hali na mali kujenga shule yenu hapa kijijini Wanyere,nimepokea kero zenu na ninaanza kuzitatua kwa kuwapatia saruji mifuko 100,niiombe na Halmashauri yetu iunge juhudi za Rais Samia kwa kutoa michango kwa ajili ya kutatua changamoto katika sekta ya elimu,” amesema Prof.Muhongo.
Hata hivyo lengo la michango hiyo ya wananchi ni kupunguza mrundikano wa wanafunzi darasani,ukosefu wa maabara za masomo ya sayansi, ukosefu wa maktaba na upungufu mkubwa wa walimu hasa wa masomo ya sayansi na lugha.
Kata ya Suguti inaundwa na vijiji vinne vya Chirorwe, Kusenyi, Suguti na Wanyere ambavyo vinategemea sekondari moja iliyoko kijijini Suguti.
Kwa kuona hilo Serikali Kuu kupitia TAMISEMI katika bajeti ya mwaka 2023/2024, itatoa kiasi cha milioni 573 kupitia mradi wake wa SEQUIP kwa ajili ya ujenzi wa sekondari mpya kijijini Wanyere na itakuwa sekondari ya pili ya Kata ya Suguti.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu