November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Milioni 135 kugharamia AFCON ya walemavu

Na Penina Malundo,timesmajira,Online

KATIBU Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi, amesema Serikali tayari imetenga zaidi ya shilingi milioni 135 kugharamia Michuano ya Mpira wa Miguu kwa Watu wenye Ulemavu Afrika inayotarajiwa kufanyika Novemba 25 hadi Disemba 5 mwaka huu kwenye iwanja mbalimbali nchini ikiwemo wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Dkt. Abbasi amesema hayo leo Novemba 10, 2021 baada ya kukutana na Kamati ya maandalizi ya michuano hiyo katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Amesema fedha hizo ni maalum kwa ajili ya kugharamia malazi, chakula pamoja na usafiri ikiwa ni juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha michezo yote inaguswa.

“Nchi yetu imekuwa ikipata bahati ya kuwa mwenyeji wa mashindano makubwa makubwa, na hivi karibuni Tanzania ilikuwa mwenyeji wa Mashindano ya ulimbwende na Utanashati kwa viziwi ambayo yalifana sana, hivyo huu ni muendelezo wa Tanzania kutambulika Kimataifa” alisema Dkt. Abbasi.

Dkt. Abbasi ameitakia Kila la heri timu ya Tembo Warriors ambayo inaiwakilisha Tanzania katika michuano hiyo na kuihakikishia Serikali ipo pamoja nao katika kipindi chote cha mashindano.

Michuano hiyo itatumika kutafuta timu nane zitakazowakilisha Afrika kwenye michuano ya kombe la dunia mwakani yatakayofanyika nchini Uturuki.

Amewataka wadau kujitokeza kusaidia timu hiyo vifaa na uratibu wa mashindano hayo kwani walemavu pia wana vipaji na vipawa vinavyohitaji kuendelezwa.