November 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mil. 7 zawakwamisha Failuna, Geay World Half Marathon

Na Mwandishi Wetu

NYOTA wa timu ya Taifa ya Riadha Failuna Abdi na Gabriel Geay ambao walitakiwa kwenda kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya Dunia ya riadha ya ‘World Half Marathon’ yatakayofanyika Oktoba 17, Gdynia nchini Poland wameshindwa kufanya usajili wa mwisho baada ya kutofikia makubaliano baina ya Mameneja wa nje ya nchi wa wanaridha hao na Shirikisho la Riadha nchini (RT).

Safari hiyo imeyeyuka huku ikiwa tayari walishafanya usajili na kwanza na walikuwa wanasubiri kukalimika kwa mchakato wa tiketi ili waweze kuthibitisha ushiriki wao katika mashindano hayo juzi Septemba 28.

Lakini pia tayari walishaanza maandaliz kwa kushiriki mashindano kadhaa ya hapa ndani ili kuimarisha viwango vyao na kuweza kufanya vizuri.

Moja ya mashindano ambayo waliyatumia kama sehemu ya maandalizi ni mbio za Ngorongoro ambapo katika mashindano hayo Geay aliibuka kinara kwa upande wa wanaume akitumia saa 1: 4 : 42 na kuvunja rekodi iliyowekwa mwaka jana na Abraham Too kutoka Kenya, aliyetumia saa 1: 5: 59 na kumshinda Herman Sule kutoka Mbulu aliyetumia 1: 6: 10 na Josephat Joshua kutoka Polisi Tanzania aliyetumia saa 1: 6: 57.

Kwa upande wa wanawake, mshindi wa jumla alikuwa Failuna kutoka klabu ya Talent ya Arusha aliyetumia saa 1: 16: 3 akimpuki mshindi wa mwaka jana Esther Chesang kutoka Kenya aliyetumia saa 1:16:49 huku nafasi ya pili Natalia Sule kutoka klabu hiyo akitumia saa 1:16:43.

Sababu kubwa zilizofanya mchakato huo kushindwa kukamilika inasemekana ni makato ya Shilingi milioni 7 ambazo mawakala hao walieleza kuwa zinapaswa kukatwa kutoka katika malipo ya wanariadha yao.

Fedha hizo zilikuwa ni kwa ajili ya tiketi za kwenda na kurudi lakini pia kulipaswa kuwa na makato mengine ya fedha za kujikimu kwa wanariadha hao.

Kocha wa nyota wa kike Failuna Matanga, Thomas Tlanka ameumbia Mtandao huu kuwa, sababu zilizowakwamisha wanariadha hao kuiwakilisha nchi katika mashindano hayo ya dunia ni RT kushindwa kuwapa fedha kwa ajili ya tiketi.

Amesema kuwa, tayari walikuwa wameshakamilisha kila timu ikiwemo usajili wa awali lakini dakika za mwisho walishindwa kuthibitisha kutokana na kukosa tiketi hizo.

Kocha huyo amesema kuwa, ndoto kubwa ya wanariadha hao ilikuwa ni kuiwakilisha nchi katika mashindano hayo ya Dunia na tayari walishaanza maandalizi ili kuhakikisha wanafanikiwa kurudi hapa nyumbani na medali.

Amesema, baada ya kushindwa kwenda kwenye mashindano hayo, mipango iliyopo sasa ni kuendelea na maandalizi ya mbio za kilometa 15 zitakazofanyika wiki mbili kutoka sasa nchini Netherland.

Mbali na mbio hizo lakini poa Failuna atashiriki mashindano ya Valencia Half Marathon yatakayofanyika mwezi ujao ambapo tayari meneja wame ameshaanza kushughulikia tiketi.

Akitoa ufafanuzi wa jambo hilo, Msemaji wa RT, Tullo Chambo amesema kuwa, baada ya kufuatilia kwa viongozi wa juu kuhusu jambo hilo alichoelezwa ni kutofikiwa kwa makubaliano baina ya pande hizo mbili.

Amesema kuwa, mara walipopata taarifa za Failuna na Geay walianza kushughulikia Viza zao lakini pia kulikuwa na mazungum zo yaliyokuwa wakiendelea na mameneja wao.

Tullo amesema, makubaliano yaliyokuwepo ni wanaridha hao kukatwa kiashi cha Sh. milioni 7 kwa ajili ya tiketi na bado fedha zao za kujikimu jambo ambalo ni kinyume na taratibu.

Amesema, baada ya kuona hivyo hata wanaridha wenyewe hawakuwa tayari kutakwa fedha hizo kwani kiuhalisia isingewalipa.

“Maombi ya wanaridha hawa kwenda kushiriki mashindano hayo ya Dunia yalikuja kupitia Mameneja wao wa nje ambao ndio tulikuwa tukijadiliana nao hivyo kutokana na muda mfupi uliokuwepo wa kuthibitisha ushiriki na masuala ya tiketi walijikuta hadi mda wa usajili wa pili unafungwa bado suala la tiketi lilikuwa halijakamilika, ” amesema Tullo.