January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Miili nane yaopolewa,ajali ya mtumbwi Ziwa Victoria

Judith Ferdinand, Timesmajira Online,Mwanza

Takribani siku nne,zimepita tangu kupinduka kwa mtumbwi uliokuwa umebeba watu na mizigo,kugonga mwamba eneo la Bwiru,wilayani Ilemela mkoani Mwanza na kusababisha majeraha kwa watu takaribani 28 pamoja na vifo,ajali iliotokea Septemba 25,2024.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza,kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama pamoja na wananchi,wamefanikiwa kuopoa miili ya watu 8,waliopoteza maisha,baada ya mtumbwi waliokuwa wakisafiria,kugonga mwamba eneo la Bwiru wilayani Ilemela na kupinduka ukiwa na watu pamoja na mizigo.Mtubwi huo wa MV.Sea Falcon ulikuwa unatokea Mwalo wa Kirumba, wilayani Ilemela kwenda kisiwa cha Goziba, Wilaya ya Muleba,Mkoa wa Kagera.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa, Septemba 28,2024,ameeleza kuwa baada ya tukio hilo, Septemba 26,2024, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza,kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama pamoja na wananchi,waliendelea kuwatafuta watu wengine ambao huenda walikuwa hawajaopolewa kwenye ajali hiyo sambamba na kutafuta namna ya kunasua
mtumbwi ambao ulikuwa umezama kwenye maji.

“Jitihada hizo ziliendelea, kufanywa na Jeshi la Polisi kupitia kikosi cha wanamaji,
wakishirikiana na askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na wananchi hususani wavuvi wanaofanya shughuli zao ndani ya ziwa Victoria,kwenye fukwe za Wilaya ya Ilemela,”ameeleza Mutafungwa na kuongeza:

“Ilipofika Septemba 27,2024, tulifanikiwa kuopoa mwili wa mtu mmoja,
aliyetambuliwa kwa jina la Benene Boaz(57), mvuvi na mkazi wa Kata ya Bugogwa, wilaya ya Ilemela.Na Septemba 28,2024,tumefanikiwa
kuopoa miili ya watu saba na kufanya jumla ya watu nane waliopolewa ambao
wote ni jinsia ya kiume,na miili hiyo
imefikishwa katika hospitali Rufaa ya Mkoa wa
Sekou- Toure kwa ajili ya uchunguzi wa kitaalamu, hifadhi na utambuzi,”.

Ametaja,majina ya miili iliotambuliwa na tayari imekabidhiwa ndugu kwa
taratibu za mazishi ni,Kelvine Bigamana(20),mkazi wa Sengerema,Furaha Luhemeja(19) mkazi wa Sengerema,Rashid Salala,(33),mkazi wa Ibanda-Kirumba.Huku
miili mingine minne yote jinsia ya kiume bado haijatambuliwa na imehifadhiwa katika hospitali hiyo ya Mkoa.

Pia ametoa wito kwa wananchi ambao wanandugu waliosafiri katika mtumbwi huo kufika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekou-Toure kwa ajili ya kutambua miili iliyosalia.

Aidha,amesema,jitihada zinaendelea za kunasua mtumbwi huo kwenye maji,huku akiwakumbusha wananchi wote kuendelea kuzingatia maelekezo yote, yanayotolea na Serikali ya kupanda vyombo vya usafiri
majini, ambavyo vimesajiliwa rasmi kwa taratibu zilizowekwa na mamlaka
husika.
Pia,imewataka watoa huduma za usafirishaji Ziwa Victoria,kufanya kazi kulingana na leseni zao, kwa sabababu kutofanya hivyo
ni uvunjifu wa sheria na kuhatarisha usalama wa watu na mali zao.