November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Migongano ya binadamu na wanyamapori bado ni changamoto’

Na Penina Malundo, timesmajira

HALI ya migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori imekuwa ikiongezeka siku hadi siku kutokana na hali ya ukidhani kati ya binadamu na wanyamapori katika utumiaji wa rasilimali ikiwemo watu kujenga makazi katika njia za wanyamapori.

Uwepo wa ukidhani huo unapelekea madhara mbalimbali kutokea ikiwemo wanyama kuuwawa na binadamu au binadamu kuuwawa na wanyama kutokana na kugombania matumizi ya rasilimali ikiwemo maji.

Asilimia 80 ya migongano baina ya binadamu na wanyamapori nchini inahusisha mnyama tembo huku wengine kama simba,boko,nyati,fisi na mamba uchangia asilimia 20 ya migongano hiyo.

Licha ya kuwepo kwa changamoto hiyo serikali imekuwa mstari wa mbele kuboresha utendaji kazi kuleta mapinduzi katika utoaji huduma na utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya uhifadhi wa wanyamapori,utatuzi wa migongano baina na Wanyamapori.

Miongoni mwa maboresho hayo ni pamoja na mkakati wa kutekeleza sera ya wanyamapori ya mwaka 2023 -2033,Mkakati wa Kitaifa wa kupambana na Ujangili ya Mwaka 2020-2024 pamoja na mpango mkakati wa kuongoza shoroba wa mwaka 2022 – 2026 ambapo sera hizi zitaweza kusaidia kupunguza migongano hiyo kwa kiasi kikubwa.

Hayo yamebainishwa wakati wa mafunzo yaliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET)kwa ufadhili wa Mradi wa Kupunguza Migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori ulio chini ya Shirika la Maendeleo la Ujeruman (GIZ)kwa niaba ya Serikali ya Ujerumani (MBZ).

Ofisa Uhifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania(TAWA), anayesimamia udhibiti wa wanyamapori wakali na waharibifu,Isaack Chamba anasema changamoto ya migongano baina ya Binadamu na Wanyama haijaanza miaka ya hivi karibuni imekuwa ya muda mrefu ambapo sera ya wanyamapori ya mwaka 1998 na marudio yake ya 2017 inatambua changamoto hiyo.

Anasema migongano hiyo hata katika Sheria ya Hifadhi ya Wanyamapori sura ya 283 na yenye marejeo ya mwaka 2022 kupitia kifungu cha 19 inayozungumzia masuala ya uwepo wa changamoto hii ya binadamu na wanyamapori waharibifu.

Chamba anasema mwaka 2018,changamoto ya migongano baina ya Binadamu na Wanyama iliongezeka kuwa kubwa hususani matukio ya wanyamapori kusababisha madhara kwa binadamu na pia uwepo wa matukio ya wanyamapori kutoka katika maeneo ya hifadhi.

”Hali hiyo ikawa ndio chanzo cha kuzidi kuongezeka kwa migongano kwani wanyamapori wanakuwa wanatoka katika maeneo ya hifadhi na kuzunguka katika maeneo yaliyokaribu nao hivyo kuanza kusababisha hali ya migongano kuzidi,”anasema.

Anasema kutokana na changamoto hiyo kuzidi Wizara ya Maliasili na Utalii ilianzisha Mkakati wa Kitaifa kwaajili ya kukabiliana na changamoto hiyo,ujulikanao ”Mkakati wa Kitaifa wa Kusimamia utatuzi wa Migongano ya Binadamu na Wanyamapori” ambapo utekelezaji wake unachukua miaka mitano 2020-2024.

Chamba anasema mkakati huo utakapokamilika utawawezesha kufanya tathimini kuangalia namna gani utekelezaji wa mkakati ulivyofaikiwa kwa kiwango kipi na baada ya hapo wataweza kuangalia namna ya kuihisha na kuja na mkakati mwingine.

”Mkakati huu tuliuzindua rasmi mwezi October 5,2020 ambapo changamoto hii ilikuwa inafanyiwa na TAWA pekee yake ila baada ya kuzindua mkakati huu utekelezwaji unafanywa na wadau mbalimbali ikiwemo Jamii,”anasema Chamba anasema matukio ya migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori yamekuwa yakiongezeka ambapo takwimu zinaonyesha kuwa Mwaka 2016 hadi 2023,yameongezeka hadi kufikia wastani ya 23.76 kwa mwaka.

Anasema changamoto kubwa pamoja na madhara yanayotokea katika migongano hiyo ni uharibifu wa mazao ambapo takwimu inaonyesha kwa wastani wa 118.1 kwa mwaka.

”Katika kukabiliana na migongano hiyo mwaka 2022/2023 TAWA imeweza kuua wanyama 108 ambao wameweza kuleta madhara kwa binadamu,”anasema

Anasema kuna wilaya takribani 44 zinachangamoto ya migongano hiyo ikiwemo na wilaya ya Busega,Kilwa,Meatu,Nachingwea,Rufiji,Lindi Manispaa,Manyoni,Bunda na Itilima.

Kwa upande wake Mshauri wa Mradi wa Kupunguza Migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori nchini GIZ, Anna Kimambo anasema kutatua migogoro baina ya binadamu na wanyamapori sio jukumu la serikali pekee bali ni la Watanzania wote.

Anasema kupitia mradi huo utatekelezwa katika wilaya tatu za Namtumbo,Tunduru Mkoani Ruvuma pamoja na Liwale katika vijiji 30 ambavyo vimebainika kupata matukio hayo ya binadamu na wanyamapori.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Waadishi wa Habari za Mazingira (JET),Dkt. Ellen Otaru anasema mradi huo ni mahsusi kuibua mchakato yote inayofanywa migongano ya binadamu na wanyamapori katika nyanja za kusini.

Anasema lengo kuu kuhakikisha wanahabari wanapata uelewa mzuri wa masuala yote yanayohusu taarifa,kiwango kilichopo na kinachoendelea na namna ya kupunguza kwa njia nzuri sahihibila uharibifu masaula yote ya migongano ya binadamu na wanyama pori.