Ampa Lukuvi siku 7, awaweka kitimoto watendaji,
Mkurugenzi Kilosa aponea kwenye tundu la sindano, aomba msamaha kwa madudu aliyofanya
Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
MIGOGORO ya ardhi mkoani Morogoro imemchefua Rais John Magufuli, baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi maeneo mbalimbali mkoani humo aliyokuwa akipita mara baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa mahandaki kwenye mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) mkoani Morogoro.
Kutokana na hali hiyo, Rais Magufuli amempa siku saba Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, awe amemkabidhi hati ya shamba lenye ukubwa wa hekta 5,000 linalomilikiwa na raia wa kigeni wilayani Kilosa, mkoa wa Morogoro.
Mbali na kumpa Waziri Lukuvi siku saba, Rais Magufuli nusura amtumbue Mkurugenzi wa Wilaya ya Kilosa baada ya kutoridhishwa na uamuzi aliochukua wakati ukisubiriwa uamuzi wa timu ya Waziri Lukuvi ambayo ilikuwa inapeleka mapendekezo yake kwa Rais.
Rais Magufuli alitoa agizo hilo kwa Waziri Lukuvi jana baada ya kupokea malalamiko ya mgogoro wa ardhi kutoka kwa wananchi wa Kibamba, wilayani Kilosa na wale wa Kijiji cha Ironga.
Amemuagiza Waziri Lukuvi aliyekuwepo kwenye msafara wake kumkabidhi hati ya shamba hilo ili aligawe upya, kisha sehemu yake wapewe wananchi wa Kibamba kwa ajili ya kumaliza changamoto ya mgogoro wa ardhi.
Rais Magufuli amesema katika uongozi wake atahakikisha analinda maslahi ya wananchi wanyonge pamoja na kuwadhibiti wenye nguvu ambao wamekuwa wanadhurumu haki za wanyonge.
“Mnakodishiwa mashamba sababu hati ni za wakubwa, nataka nilale nao hao wakubwa, nimesema siku saba waziri pamoja na mkuu wa mkoa ataleta hati, yale mashamba yakufuta, sababu kwa mujibu wa sheria ardhi iko chini ya rais, na mimi nitaenda na watu wanyonge,” amesema Rais Magufuli.
Rais Magufuli aliwataka wananchi wa Kibamba kutumia vyema mashamba watakayopewa. “Naweza futa nusu au kutokana na mapendekezo nitakayopewa nitayagawa kwenu. Mjipange vizuri kugawiwa kwenu isije kuwa chanzo cha kupigana, mtumie uongozi mlio nao kila mmoja apate kipande, kutakuwa sehemu ya wafugaji na wakulima sababu wote tunategemeana,” amesema Rais Magufuli.
Wakati huo huo, Rais Magufuli nusura amtumbue Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Asajile Mwambambale, lakini amesema hawezi kufanya hivyo mbele ya Askofu.
Akizungumza kwenye uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa handaki kwenye njia ya reli ya treni ya kisasa (SGR), leo tarehe 29 Juni 2020 Kilosa mkoani Morogoro, Rais Magufuli amewataja wateule wake hao kwamba wanamakunyanzi kwenye utendaji wao.
Rais Magufuli amesema wateule wake katika uongozi wake hawawezi kuwa na furaha kwa kuwa hata yeye hana furaha kwani wanapaswa kuumiza kumaliza kero za wananchi.
Akizungumzia migogoro wilayani humo, Rais Magufuli amesema anazo taarifa kuwa watendaji wake wanafanyakazi kinyume na taratibu za kazi zao zinavyowaelekeza.
Miongoni mwa waliotajwa na Rais Magufuli kwenye mkutano huo kuwa ni Mkurugenzi na Mtendaji wa Wilaya ya Kilosa.
“Niwaambie katika kipindi changu hamtafurahi sana, hata mimi sipati raha. Ni lazima tuteseke kwa ajili ya kutatua kero za wananchi. Nimeambiwa Mkurugeni wa hapa ana matatizo, ajirekebishe.
“Siwezi nikamtumbua mbele ya askofu. Madhambi yake anayajua, ameuza eneo kule, kikao kikakaa siku hiyo hiyo na mkataba akasaini siku hiyo hiyo, kwa taarifa za pembeni zinasema aliingiziwa sh. milioni 400,” amesema Rais Magufuli.
Amesema pia Mkuu wa Wilaya ya Kilosa naye ana taarifa zake kuhusu utendaji wake na migogoro wilayani mwake. Amesema kama anaowateua lakini hawawezi kazi ni bora wakaacha kazi.
“Nawaomba viongozi badilikeni, mkiteuliwa mkiona hamuwezi acheni kazi. DC wa Kilosa nawe jirekebishe. DC umeenda Kimamba ukaanza kuwazuia watu kwenye mashamba tena yanamilikiwa na wageni, badala ya kuwatetea watu wako, unawatetea ambao hujui hata wamezaliwa kijiji gani,” amesema.
Amesema kumekuwa na wageni wanaomiliki ardhi kinyume na sheria za nchi, hivyo aliagiza ardhi irejeshwe kisha igawiwe kwa wananchi ili wanufaike nayo.
Rais Magufuli alionekana kukwerwa zaidi na Mkurugenzi wa Kilosa, baada ya kugawa ardhi ya Kijiji wakati bado yakisubiriwa maamuzi ya timu ya Waziri Lukuvi ya kushughulikia migogoro ya ardhi.
“Sitaki kumuonea mkurugenzi ni kijana mzuri, lakini hata mimi amenivunjia heshima, kwa sababu niliwaambia mapendekezo ninayapeleka kwa Rais ni haya na wananchi wasiondolewe,” amesema Lukuvi.
Ilielezwa kuwa tajiri huyo amepora wananchi hekta 400 za ardhi lakini wakati wa kugawa mkurugenzi aliamua kuwagawiwa wananchi hekari 140.
“Mimi nimeagiza Waziri Lukuvi na viongozi wengine, lakini wewe umewadharau, ukamuagiza Mtendaji wa Kata atekeleze maelekezo yako unayoyataka,” amesema Rais Magufuli.
Baada ya mkurugenzi huyo kuona amezidi kubanwa, aliaomba msamaha. “Mheshimiwa Rais naomba unisamehe kwa kosa ambalo nimelifanya,” amesema DED Mwambambale.
Wakati akiendelea kuomba msamaha, Rais Magufuli alimuuliza; “Unawaona wananchi hao, una muda gani hapa?” Alihoji na kujibiwa na DED huyo kuwa ana miezi 20.
“Kwa hiyo unataka kuniambia wananchi hawajui dhuluma wanayotendewa?”Alihoji Rais Magufuli na kuongeza; ” Lakini jambo la pili kwa nini hukusubiri waziri niliyemtuma?”
Waziri wa TAMISEMI, Suleima Jaffo, amesema kitendo kilichofanywa na Mkurugenzi hakina afya katika utendaji wake. “Malalamiko ya wananchi hayatoi afya nzuri,” amesema Jafo.
Mara baada ya kauli hiyo ya Jafo, DED huyo alipata nafasi ya kuendelea kujitetea na kuomba msamaha kwa Rais Magufuli mara tatu akisema;
“Mheshimiwa Rais kuna kazi nyingine ambazo nimefanya kwa mafanikio, umenipa kazi ya ujenzi ya jengo la upasuaji, nimelijenga kwa mafanikio.”
Mara baada ya kumaliza kuomba msamaha kwa Rais Magufuli, Rais amesema; “Ndugu wana wa Ironga kilio chenu nimekisikia, mkuu wa mkoa nimeshakueleza, waziri wa TAMISEMI nimeshamueleza, saa nyingine matatizo tunayoyapata ni kwa sababu ya watendaji wengine.”
Rais Magufuli alimtaka DED huyo kuandika barua ya kufuta barua hiyo ya kugawa ardhi kwa wananchi na aombe radhi kwa wananchi kwa makosa aliyowafanyia, jambo ambalo alifanya.
“Kilio chenu nimekisikia, Waziri ataleta ripoti yangu na haya yaliyofanywa na mkurugenzi yamefutika yanabaki kama ilivyokuwa zamani hadi majibu yatakapoletwa,”amesema na kuongeza;
“Na atakayewaletea majibu ni mheshimiwa Lukuvi pamoja na Mkuu wa Mkoa,” amesema.
Wakati huo huo, Rais Magufuli aliwataka wakazi wa eneo hilo kulinda mradi huo wa reli na kwamba ujenzi wa reli hiyo ya kisasa Dar es Salaam hadi Morogoro umekamilika kwa asilimia 85 na Morogoro hadi Makutupora umejengwa kwa asilimia 30.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa