December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Migodi yachangia pato la Taifa Shinyanga

Na Suleiman Abeid,TimesMajira Online

MKOA wa Shinyanga ni miongoni mwa mikoa 10 inayoongoza nchini katika kuchangia pato la Taifa (GDP) ambapo kwa takwimu za mwaka 2021 mkoa huo ulikuwa ni wa nne kitaifa katika uchangiaji wa pato hilo.

Mafanikio ya Mkoa huo yanachangiwa kwa asilimia kubwa na uwepo wa migodi mikubwa na midogo ya madini ikiwemo ya dhahabu na almasi pamoja na mazao makuu ya kibiashara ikiwemo pamba na tumbaku.

Tukitupia macho upande wa sekta ya madini tunaona ndani ya kipindi cha miaka miwili chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan mkoa wa Shinyanga umeweza kukusanya kiasi cha bilioni 255 kutoka sekta hiyo ya madini.

Baadhi ya wachimbaji wadogo wa dhahabu wakiendelea na shughuli zao za kila siku katika Mgodi unaomilikiwa na wazawa wa Wachapakazi Goldmine kijiji cha Nyandolwa wilayani Shinyanga.

Mapato hayo yamepatikana kupitia ada za leseni, mrabaha na ada za ukaguzi yanayokusanywa kupitia Wizara ya Madini huku Mkoa ukiwa umetoa leseni mbalimbali za madini hususan upande wa migodi midogo midogo inayomilikiwa na wazawa.

Tunaweza kuona kwamba hatua ya Serikali kuruhusu wazawa kuwekeza katika sekta hii ya madini kwa kumiliki migodi midogo inayotambulika kisheria baada ya kupatiwa leseni ni moja ya mafanikio makubwa katika kuongeza makusanyo ya mapato ya Serikali.

Hatua hiyo ya Serikali imezingatia Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020 – 2025 ambapo chama hicho tawala wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 miongoni mwa ahadi zake ilizozitoa kwa wananchi ilikuwa ni kuboresha sekta ya madini nchini.

Ndani ya Ilani hiyo inaelezwa kuwa, sekta ya madini ni muhimu kutokana na kuchangia kwake mapato ya serikali na kutoa ajira kwa watanzania, hususani wananchi wa kawaida.

Ibara ya 65 ya Ilani hiyo inaelezwa, nanukuu; “….Katika miaka mitano ijayo, Chama cha Mapinduzi kitaendelea kusimamia Serikali kuhakikisha mapinduzi makubwa yaliyofanyika katika sekta ya madini yanaendelezwa,”hususani katika kuwezesha wananchi kuwa sehemu ya umiliki wa raslimali hiyo.

Aidha CCM itahakikisha sekta ya madini inachangia zaidi pato la Taifa na kupunguza umasikini nchini,” mwisho wa kunukuu.

Mchimbaji mdogo wa dhahabu katika mgodi wa Wachapakazi Goldmine, Eliza Juma akionesha moja ya mawe yenye madini ya dhahabu yanayosubiri kusagwa ili kupatikana dhahabu.

Miongoni mwa mikakati inayotekelezwa ili kufikia malengo kusudiwa ni kubuni na kuimarisha utekelezaji wa mipango ya kuwawezesha wachimbaji wadogo waweze kufanya shughuli zao kwa tija kwa kuwatengea maeneo au kuwapatia leseni kwenye maeneo ambayo yana taarifa za msingi za kijiolojia.

Pia kutoa huduma za utafiti kwa gharama nafuu, kuwaendeleza kutoka uchimbaji mdogo kwenda wa kati na hatimaye uchimbaji mkubwa, na kuwapa mafunzo yanayohitajika kuhusu uchimbaji na biashara ya madini.

Ndani ya kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan utekelezaji wa ahadi hizi zilizomo ndani ya Ilani ya uchaguzi ya CCM hivi sasa tayari umeanza kuonekana.

Miongoni mwa wanufaika wa ahadi hizo ni wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu wanaomiliki mgodi mdogo wa dhahabu wa Wachapakazi Gold Mine ulioko kijiji cha Nyandolwa, kata ya Mwenge wilayani Shinyanga.

Wachimbaji wadogo hawa ambao wamejiunga kwenye kikundi na kuanzisha mgodi huo wanaishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia msaada mkubwa na kuweza kumiliki mgodi ambao mbali ya kuwanufaisha wanachama wake pia umeweza kutoa fursa za ajira kwa wananchi wengine zaidi ya 300.

Mwenyekiti wa kikundi hicho, Joshua Sayi anasema hatua ya Serikali kuwapatia wachimbaji wadogo maeneo ya uchimbaji kumefungua fursa kwao ya kuweza kuendesha shughuli zao kwa uhakika tofauti na miaka ya nyuma walipokuwa wakihangaika kupata maeneo ya uchimbaji.

“Kwanza tunamshukuru Mungu kwa sababu tumepata Rais ambaye ana mtizamo wa pekee sana, tangu tulipoanza shughuli zetu hapa mwaka 2021 mpaka sasa ni kama miaka miwili imepita, tunashukuru kwa jinsi Serikali inavyotujali sisi wananchi wake,”.

Mwenyekiti Kikundi cha Wachapakazi Goldmine Nyandolwa Shinyanga, Joshua Sayi.

“Serikali imefanya mabadiliko makubwa tofauti na huko nyuma ambapo kila wananchi walipogundua madini ya dhahabu walifukuzwa kwa madai kuwa eneo husika lina leseni ya mwekezaji mkubwa, lakini Rais Samia ameiondoa hali hiyo kwa sasa ambapo Serikali inatujali pia sisi wachimbaji wadogo,” anaeleza Sayi.

Anaendelea kufafanua kuwa kuanzishwa kwa mgodi wa Wachamapakazi kumefungua pia fursa kwa watanzania wengine zaidi ya 300 kujipatia ajira na kwamba kutokana na uzalishaji wanaozalisha wameweza kutoa misaada mbalimbali ya kijamii katika vijiji vinavyowazunguka kwenye sekta za afya, elimu na miundombinu ya barabara.

Hata hivyo Mwenyekiti huyo ametoa ombi kwa Serikali iweze kuwasaidia kuboresha zaidi shughuli zao kwa kuwapatia wataalam wa masuala ya madini ili waweze kuchunguza maeneo yenye madini ya dhahabu badala ya hivi sasa wanapochimba kwa kubahatisha bahatisha.

“Shukrani zetu nyingine kwa Serikali ni kutokana na maamuzi yake sahihi ya kuanzishwa kwa masoko ya madini hapa nchini, masoko haya yameturahisishia katika kuuza dhahabu tunazopata, na tunapata bei nzuri tofauti na tulivyokuwa tunahangaika kutafuta wanunuzi wenye bei nzuri,” anaeleza Sayi.

Kuhusu uchangiaji wa pato la taifa, Sayi anasema ndani ya kipindi cha miaka miwili mgodi wa Wachapakazi umelipa serikalini mrabaha wa zaidi ya bilioni 2 na kuwezesha mgodi huo kushika nafasi ya tatu kitaifa katika uchangiaji wa pato la Taifa huku kimkoa wakichukua nafasi ya kwanza.

Baadhi ya wachimbaji wadogo wa dhahabu wakiendelea na shughuli zao za kila siku katika Mgodi unaomilikiwa na wazawa wa Wachapakazi Goldmine kijiji cha Nyandolwa wilayani Shinyanga.

Kwa upande wao Katibu wa Wachapakazi Goldmine, Petro Jonathan na Katibu Msaidizi wake Galiangu Yusufu wanasema moja ya mambo ambayo wameyapa kipaumbele katika eneo la mgodi wao ni suala la usalama kwa wachimbaji na utunzaji wa mazingira katika eneo lote na mgodi.

“Kwa ujumla tumejipanga vizuri katika utekelezaji wa shughuli zetu za kila siku hapa mgodini, na kupitia nafasi hii tunaiomba Serikali itusaidie kuturekebishia miundombinu mfano tupate umeme, maji na vyuma kwa ajili ya kuwekea kinga kwenye mashimo tunayochimba badala ya kutumia miti,”.

“Tukipata umeme tutapunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ya miti na mazingira yetu yatakuwa salama maana tutaacha kwa kiasi kikubwa matumizi ya miti, umeme ukiwepo tutaweza kutumia saruji na nondo katika shughuli zetu, tofauti na sasa tunavyotumia jenereta gharama zake ni kubwa,” anaeleza Yusufu.

Baadhi ya wachimbaji wadogo wanaofanya shughuli zao kwenye mgodi huo pia wameipongeza Serikali kwa kuruhusu uwepo wa wawekezaji wadogo na wazawa kwenye sekta ya madini ambapo hatua hiyo imeongeza wigo wa ajira kwa vijana na wanawake ambao sasa wanajiajiri kupitia migodi hiyo.

“Kwa kweli tunaushukuru uongozi wa Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu wazawa kuwekeza kwenye sekta ya madini na kutoa leseni kwa wachimbaji wadogo wanaomiliki migodi midogo ya dhahabu,ombi letu kwake ni kutupatia vifaa vya kuchunguzia maeneo sahihi yenye madini tuweze kuchimba kwa uhakika,” anaeleza Josia Lunegeja.

Diwani wa Kata ya Mwenge, Edward Maganga anasema ndani ya kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan pamekuwepo na mafanikio makubwa kwenye sekta ya madini upande wa wachimbaji wadogo kutokana na kuruhusu watengewe maeneo rasmi ya uchimbaji ambapo pia wamepewa leseni za uchimbaji.

“Rais Samia ndani ya kipindi chake cha miaka miwili amewawezesha wachimbaji wadogo hapa nchini kufanya shughuli zao kwa uhakika, hivi sasa wana uhakika wa kufanya kazi bila kufukuzwa fukuzwa ovyo kama zamani,pia wazawa wameweza kuanzisha migodi midogo ambayo imetoa ajira kwa watanzania,”

“Mfano mzuri ni hapa kwenye kijiji cha Nyandolwa, tuna migodi miwili inayomilikiwa na wazawa, mmoja ni unamilikiwa na wachimbaji ambao wamejiunga na kuanzisha Kikundi cha Wachapakazi Goldmine na wa pili unamilikiwa na mzawa unaitwa, Busolwa Goldmine, hili ni jambo jema sana na la kupongezwa,” anaeleza Maganga.

Anasema kutokana na uwepo wa migodi hiyo miwili mbali ya kutoa ajira kwa wazawa wa vijiji jirani pia imeweza kuchangia misaada mbalimbali katika huduma za kijamii ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa kwenye shule ya msingi Nyandolwa pia ujenzi wa Zahanati ya kijiji cha Nyandolwa.

“Kwa upande wa huduma za kijamii migodi hii miwili iliyopo kwenye kijiji chetu imesaidia kwa kiasi kikubwa, mfano katika shule ya msingi wamesaidia ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa, wametoa vifaa na kusaidiana na TARURA katika ukarabati wa barabara zetu, na pia kukamilisha ujenzi wa Zahanati ya kijiji cha Nyandolwa,” anaeleza.

Mwalimu Mkuu shule ya Msingi Nyandolwa, Leonard Luhende ni miongoni mwa watu ambao wamemshukuru Rais Samia kwa kuruhusu wawekezaji wazawa kuwekeza kwenye sekta ya madini na kwamba mchango wa wawekezaji hao kwa sasa unaonekana baada ya shule yao kujengewa vyumba viwili vya madarasa.