Na Damiano Mkumbo, TimesMajira Online
JUMLA ya mifugo 6987 yenye thamani ya shilingi bilioni 1.05 imechinjwa na kutolewa sadaka kwa wahitaji mbalimbali wakati wa kutekeleza ibada ya Eid El Adha mkoani Singida kama inavyoelekezwa katika dini ya Kiislam.
Taarifa iliyotolewa na Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) mkoani Singida, Buruhani Mohhamed Mlau ilieleza kuwa, mifugo hiyo ambayo ni ng’ombe 1067, jondoo na mbuzi 5,920 zilitolewa na taasisi sita za kiislam kutoka mataifa wahisani duniani.
Alizungumza juu ya zoezi hilo lililofanyika kwa siku tatu kulingana na madhehebu ya dini hiyo, lilikuwa ni kutekeleza Ibada ya kuchinja na kutoa sadaka kwa maskini, wasiojiweza, wagonjwa,wanyonge, vilema na wengine wasiojiweza na jamii kwa ujumla ili washereheke siku hiyo kwa furaha iliyofanyika kwenye vituo mbalimbali vya mawakala mkoani Singida.
Akitoa mawaidha wakati wa sala ya sikukuu hiyo iliyofanyika uwanja wa shule ya Msingi ya Ipembe mjini hapa na utekelezaji wa ibada katika kituo kimoja kilichopo Unyankindi, shehe wa mkoa huo, Issa Nassoro aliwashukuru wahisani wote na mawakala wao kwa msaada huo ambao unaoongeza baraka katika shughuli zao kutochelewa zoezi hilo.
Shehe Issa Nassoro alibainisha kuwa, ibada hiyo iliagizwa katika dini ya kiislamu ilifanya kama maelekezo yalivyo ambayo mara ya kwanza Ibrahimu alitaka kuchinja mwanae, lakini mwenyezi Mungu alimpa kondoo badala yake amtolee sadaka kutokana na imani yake,na kuwataka watekelezaji kuonyesha uaminifu na uadilifu kama ilivyokuwa katika badhi ya maeneo aliyotembelea kutumia mifugo mizuri yenye kukubalika, na kuonya mawakala wa taasisi hizo wanaodanganya kununua ng’ombe waliodhaifu na kukonda.
“Pamoja na misaada ya wanyama hao tunaopewa kila mwaka, sisi pia tukiwa waumini wa dini yetu inatupasa kuendeleza moyo wa kujitolea, vile vile tunaomba wahisani waweze kufikiria aina zingine za shughuli zenye manufaa zaidi kwa jamii zikiwemo sekta za maji, elimu,afya na uchumi ambazo zinahitajika kuinua maendeleo ya Taifa la Tanzania,”alisema kiongozi huyo.
Alitumia wakati huo kuwaomba waislamu waendelee kujenga umoja upendo na amani miongoni mwao na madhehebu ya dini zingine pamoja na kushukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kuonyesha kujali wananchi wake, pale alipoagiza kuangaliwa upya zoezi la gharama za miamala katika makampuni ya simu ili kuwapa nafuu wananchi ya kutuma na kupokea fedha kwa kutumia njia hii.
Kiongozi huyo alisisitiza kutekeleza maelekezo ya serikali kupitia idara ya afya kuzingatia kwa makini jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa COVID-19 kwa kuwa bado ni tishio kwa maisha ya watu hapa nchini na dunia nzima ikiwepo kunawa mikono kwa maji yanayotiririka, kuvaa barakoa, kuepuka misongamano na kutoa taarifa juu ya watu wanaoonyesha dalili ili hatua za kiafya ziweze kuchukuliwa.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Taasisi ya Islamic Foundation Mkoa wa Singida, Shehe Zuberi Nkoko alieleza umuhimu wa kila mtu kutambua umuhimu wa kutambua suala zima la kuwasaidia wahitaji kwa kutoa chakula, mavazi, malazi na matibabu ili waweze kuishi katika hali nzuri ya ustawi wao wakati wanapokuwa na hali hiyo kama walivyojaliwa na mola wao kupewa nafasi ya maisha yaliyo nafuu zaidi kuuliko kundi la wahitaji.
Akizungumza wakati wa kutekeleza ibada ya kuchinja wanyama 890 katika kituo chake kilichopo karibu mtaa wa stendi mpya ya Misuna mjini Singida alisema, misaada hiyo siyo ya kutoa chakula tu, bali ni kuendeleza ushirikiano, undugu na upendo katika imani kwa mataifa mengine duniani na kufanya waislamu kuwa ni wamoja walio chini ya Mwenyezi Mungu.
More Stories
Kongamano la Uwekezaji kati ya Tanzania na Ubelgiji lafanyika Dar
CCM kuhitimisha kampeni kwa kishindo
Walimu elimu ya lazima watatakiwa kuwa wabobezi kwenye masomo wanayofundisha