March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Midahalo mingi kwa vijana chachu ya kuwapa fursa ya kugombea uongozi

Na Penina Malundo,Timesmajira

IMEELEZWA kuwa uwapo wa midahalo mingi kwa vijana na viongozi wenye umri mkubwa katika nafasi mbalimbali za uongozi unaweza kuwapa fursa vijana wa kitanzania kujiamini na kupata uzoefu wa kujifunza mambo mbalimbali ya Uongozi.

Midahalo hiyo itaweza kuwapa fursa vijana kuona wanauwezo wa kushika nafasi hizo kwa kuona namna ya viongozi wenye umri mkubwa kuwa karibu nao na kuwapa elimu.

Akizungumza hayo jana jijini Dar es Salaam,wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo vijana na wanawake kutoka sehemu mbalimbali, Mkufunzi wa Masuala ya Vijana na Wanawake,Judith Ngusa amesema uwepo wa midahalo kati ya vijana na viongozi hao inauwezo mkubwa wa kutoa uzoefu kwa vijana kujua nini wanatakiwa kufanya ili wawe viongozi wenye tija katika jamii.

Amesema vijana wanatakiwa kupata elimu kwasababu viongozi ambao wanaumri mkubwa tayari wao wamepata uzoefu wa kutosha na kujua mambo mengi katika nafasi zao sio kama wanavyokuwa vijana kuwa na woga pamoja na Mihemko.

”Vijana wanapaswa kukaa chini na kujifunza yale yote yanayofanywa na viongozi ambao wanaumri mkubwa katika nafasi mbalimbali na kukubali kufundishwa kujua uongozi ni nini na unakazi kazi katika jamii.

”Tunaona sasa hivi vijana namna wanavyokuwa hawawezi kusema,wamekuwa waoga wanaona wakigombea nafasi yoyote wanaona haziwafahi hivyo kuona kufanya mambo mengine na kuwaachia watu wenye umri mkubwa kuendelea kuongoza,”amesema


Amesema hii yote inatoka na vijana wengi kuwa na hofu pamoja na woga uliojengeka katika fikra zao kuona wanapoweza kujitokeza wanaweza kukosolewa au kuona hawawezi kuongoza kwa kuofia kuharibu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Miradi wa Shirika la Mazingira ,Haki za Binadamu na Jinsia (Envirocare),Eng.Amos Mbwambo amesema takribani vijana na wanawake wasipungua 500 kutoka Mkoa wa Dar es Salaam,taasisi yao chini ya Mradi maalum wa ushiriki wa wanawake pamoja na vijana katika masuala ya uongozi,unafadhiliwa na shirika la Forum CIV la nchini Sweden.

Amesema mradi huo unatekelezwa chini ya Wilaya Tatu Kinondoni,Ubungo pamoja na Kigamboni.”Mafunzo hayo yamejumuisha vijana na wanawake kutoka taasisi za dini,Ofisi za Serikali za Mitaa,Wanafunzi kutoka elimu ya vyuo vikuu,wawakilishi kutoka asasi za kiraia,Wawakilishi kutoka Asasi za kiraia kujadili ushiriki wa wanawake na vijana katika nafasi za uongozi,”Alisema.

Amesema lengo la mradi huo ni kusaidiana kuwajengea vijana uwezo ili waweze kupata nafasi na kuweza kujiamini katika kuigia kwenye nafasi za uongozi.

Mmoja wa washiriki katika Mafunzo hayo,Suma Mulungu ameishukuru taasisi hii kuwakutanisha pamoja na kupata bahati ya kujifunza vitu vingi na kuelewa kuwa katika vijana na wanawake wote ni kuonyesha uwezo wao katika uongozi.

”Niwasihi wenzangu kutosita kuonyesha uwezo wetu pale unapohitajika na kutoa majibu katika changamoto kwenye jamii zetu,kutosita kutoa ushauri kwa viongozi wetu,kuonyesha nia ya kushiriki na kugombea nafasi mbalimbali za uongozi,”amesema