Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki (Mb) amesema Wizara na Taasisi zake imejipanga kuongeza wigo wa kutangaza vivutio vya utalii ndani na nje ya nchi kupitia michezo.
Mashindano mbalimbali katika michezo yana wafuatilia wengi zaidi, hivyo yataongeza idadi kubwa ya watalii watakaoitembelea Tanzania na kuongeza mapato kwa Taifa.
Waziri Kairuki ameyasema hayo Mei 31, 2024, alipokuwa akitaja vipaombele hivyo wakati wa kuwasilisha Bajeti ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa fedha 2024/2025, Bungeni jijini Dodoma.
“Wizara imejipanga kuongeza wigo wa kutangaza utalii ndani na nje ya nchi kupitia Mashindano mbalimbali ya michezo, ambayo yamekuwa na wafuatiliaji wengi zaidi Duniani ili kuongeza idadi ya watalii wengi nchini.”
“Tutambue kuwa Ligi zinazofuatiliwa sana duniani ni za mpira wa miguu, huku Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ikifuatiliwa na watu zaidi ya bilioni 4.7 duniani, ikifuatia “LALIGA” ya nchini Hispania na “BUNDESLIGA” ya Ujerumani. Hivyo mipango na mikakati ya wizara kutumia Ligi na Mashindano makubwa kama hayo yataongeza kasi ya ukuaji wa soko la utalii nchini,” amesema Kairuki.
Amesema, Ili kuwa na ushindani chanya katika soko la utalii kwa mataifa yenye Maliasili na vivutio vinavyofanana na Tanzania Waziri Wizara itaendelea kushiriki katika maonesho na matukio ya utalii pamoja na kutangaza vivutio vya utalii kupitia mashirika ya ndege ya Kimataifa yakiwemo Qatar Airways, Emirates na Turkish Airlines.
Kwa mwaka wa fedha 2022/2023 Shirika la ndege la Kimataifa la Emirate lilisafirisha takribani watalii milioni 43.6, hivyo kuweka matangazo ya vivutio vyetu vya utalii katika mashirika hayo kutaongeza kasi ya ukuaji wa utalii na kufungua masoko mapya ya utalii.
Hata hivyo, kwa kipindi cha mwaka ulioisha Disemba 2023, wizara ilishirikiana na Epic Tanzania Tour kuandaa mchezo wa Tennis ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti, mchezo ulihudhuriwa na watalii na wawekezaji takribani 80 kutoka mataifa mbalimbali.
Kupitia mchezo huo wa Tennis uliomuhusisha mchezaji tennis maarufu Veteran, John McEnroe uliitangaza Tanzania hususani Hifadhi ya Taifa Serengeti katika jarida maarufu la World Tennis, tovotu ya Forbe na gazeti la The Times la Uingereza, ambayo ni miongoni mwa masoko makubwa ya utalii wa Kimataifa.
Aidha, Waziri Kairuki amesema jitihada za kutangaza utalii zimeendelea kuzaa matunda na kupelekea kuongeza kwa mapato yanayotokana na utalii kutoka Dola za Kimarekani bilioni 1.3 mwaka 2021 hadi kufikia Dola za Kimarekani bilioni 3.4 mwaka 2023. Kuongezeka kwa mapato hayo kumeongeza kasi ya maendeleo nchini.
Wizara ya Maliasili na Utalii licha ya kuchangia asilimia 21.5 katika pato la Taifa pia ni miongoni mwa wizara ambayo imeajiri watu wengi takribani milioni 3.6 zikiwa ni ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa