January 24, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Michezo imechangia kwa kiasi kikubwa kudumumisha Muungano

Na Mwandishi Wetu

LEO Aprili 26, 2019, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaadhimisha miaka 56 ya Muungano, tangu kuungana kwa iliyokuwa Jamhuri ya watu wa Zanzibar na ile ya Tanganyika, na kupata jina moja la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Muungano huo ulisimamiwa kwa madhubuti, chini ya viongozi wawili marehemu Abeid Karume na hayati Mwalimu Julius Nyerere, ambapo Aprili 26, 1964 walichanganya udongo kuashiria kuungana kwa nchi hizo na kupata jina moja la Tanzania.

Hii ni fahari kubwa sana, kwa miaka hii tunathubutu kusema muungano huu ni lulu kwetu, kwani hadi sasa tumekuwa tukishuhudia nchi mbali mbali zikivunja muungano wa nchi zao, lakini sisi tunajivunia mpaka sasa kufikisha miaka 56 ambayo si haba.

Kwa hakika yapo mambo mengi ambayo hadi leo tunaendelea kunufaika nayo kama sehemu ya Muungano huo, kwenye masuala mbali mbali yanayogusa maisha ya binadamu.

Ikiwa leo tunaadhimisha miaka 56 ya muungano wacha nielezee mambo yanahusu michezo ambayo bado yamekuwa kielelezo tosha cha kuenzi na kudumumisha Muungano huu.

Kuna michezo mbalimbali ambayo hadi leo bado inachezwa kwa ushirikiano mkubwa baina ya wanamichezo wa Zanzibar na wale wa Tanzania bara, ambayo yanaendeleza udugu uliopo ndani ya muungano huo.

Ligi ya Muungano

Ligi ya Muungano ilianza rasmi mwaka 1982 lengo ni kudumisha Muungano wetu na kutoa usawa wa kiuwakilishi nchi, katika michuano ya kimataifa ya vilabu.

Hii ni kutokana na Tanzania bara kuwa na ligi yake na Zanzibar ligi yake, huku upande wa pili (Zanzibar) ukiwa sio mwanachama wa shirikisho la soka barani Africa caf.

Kukosa sifa ya timu zake kushiriki michuano ya Klabu Bingwa Africa na kombe la washindi (ilijulikana hivyo miaka hiyo).

Huwepo wa ligi ya Muungano ambayo ilikuwa inajumlisha timu 3 zilizomaliza nafasi za juu kwenye ligi husika, timu kutoka Zanzibar nazo zilipata nafasi ya kuiwakilisha Jamhuri ya Muungano kwenye michuano ya CAF.

Kwa kawaida mashindano mbali mbali ya ligi ya Muungano hufanyika kwa michezo mingi, ambayo hujumuisha wachezaji kutoka Tanzania bara na Zanzibar na kutafuta bingwa wa Tanzania ambaye huwakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa.

Mpira wa Miguu (Soka)

Mpira wa miguu ni mchezo unaopendwa zaidi Tanzania na hata duniani kote, na hapa kwetu ndio mchezo nambari moja kwa kuwa na mashabiki na wapenzi wengi zaidi kulinganisha na mchezo mwengine wowote.

Kwa miaka mingi Tanzania ilikuwa ikipata washiriki wa mashindano ya kombe la klabu bingwa na kombe la Shirikisho, ambayo yanaandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa kucheza ligi ya Muungano.

Ligi hii ilishirikisha timu nne za Zanzibar na nne za Tanzania bara, ambapo huchezwa mfumo wa ligi na bingwa huiwakilisha Tanzania katika ligi ya mabingwa na mshindi wa pili huwakilisha nchi katika kombe la shirikisho.

Kwa miaka mingi ushirikiano huo uliendelea hadi pale Zanzibar ilipopata uanachama shiriki wa CAF, ambapo hivi sasa kila upande hutoa wawakilishi wake kushiriki mashindano hayo, ambapo Zanzibar ilipata uanachama huo mwaka 2004.

Kombe la Mapinduzi

Ni mashindano ambayo yalianzishwa mwaka 2007 ambayo hufanyika kila ifikipo mwezi Disemba na kilele chake hufanyika Janauri 13, mashindano haya maalum kwa ajili ya kusherehekea maadhimisho ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Mashindano haya ni kielelezo dhahiri cha kuuenzi na kuendeleza Muungano huu, kwani timu mbali mbali za Tanzania bara hushiriki na kuungana na wenzeo wa Zanzibar.

Michezo ya Pasaka

Kwa muda mrefu wananchi wa Zanzibar wamekuwa na utamaduni wa kutembeleana kimichezo ifikapo sikukuu ya Pasaka, jambo ambalo linaleta mahusiano mazuri baina ya Zanzibar na Tanzania bara, hivyo kuzidi kudhihirisha kuwa dhana ya Muungano katika michezo bado inapewa kipaumbele kikubwa.

Michezo ya Pasaka hufanyika kwa wanamichezo wa upande mmoja kuwatembelea wanamichezo wenzao, ambapo mashindano ya michezo mbali mbali hufanyika, jambo ambalo linaleta umoja na mashirikiano mazuri baina ya pande mbili hizi.

Miaka 55 ya Muungano mashindano ya Pasaka mwaka huu yalifanyika Kisiwani Zanzibar, ambapo takribani wanamichezo 1000 kutoka Tanzania Bara, walipata fursa ya kuwatembelea wenzao wa Zanzibar na kucheza michezo mbali mbali,katika kudumisha Muungano wa Zanzibar na Tanganyika.

Ujenzi wa uwanja wa Amaan ambao ndio Uwanja mkubwa Kisiwani Zanzibar,ulianza kujengwa Novemba 1969, na Januari 12, 1970, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere aliufungua uwanja huo na kuupa jina la ‘AMAAN’. hiyo inadhihirisha jinsi gani Muungano ulivyochukua nafaasi yake.

Miaka 21 ya Ligi ya Muungano

Michuano hii ilifanyika kwa miaka 21 mfululizo na ikishuhudia timu 9 zikiibuka na kombe hilo katika miaka tofauti tofauti.

Licha ya ligi hiyo kuwa na timu 6 kila mwaka, bado ni hizo timu 9 tu ndio ziliibuka kidedea kila mmoja kwa wakati wake.

Timu zilizochukua ubingwa huu, zikiwa pia ni bingwa wa ligi, lakini vile vile zipo zilizochukua ubingwa huu bila kuwa bingwa kwenye ligi anapotokea.
Kwa umri wa miaka 21 ya michuano hii imeshuhudia mabingwa wafuatao:-

  1. Pan Afrika. 1982

Hii ilikuwa timu tishio sanaa, iliyotoka kwenye ubavu wa Yanga kutokana na migogoro ya wenyewe kwa wenyewe, ilikuwa timu tishio kutokana na kuwa na idadi kubwa ya wachezaji waliohama Yanga na kuunda timu hii.

Wakiwa katika ubora wake walichukua ubingwa wa bara na ule wa Muungano mwaka 1982 na kuweka rekodi ya kumbukumbu kwa kuwa timu ya kwanza kubeba kombe hilo mara tu lilipoanzishwa mwaka 1982 rekodi ambayo itabaki kwa muda wote.

  1. KMKM: 1984

Mwaka huu ulikuwa wa mafanikio kwa timu ya KMKM inayoshiriki Ligi Kuu Zanzibar, licha ya kuchukua ubingwa wa Muungano pia walikuwa ni mabingwa wa ligi ya Zanzibar.

  1. Majimaji: 1985, 1986 na 1998.

Timu ya Majimaji ilikuwa na bahati ya mtende hasa inapokuwa na namba 8?, ni timu ambayo ilikuwa na historia kubwa katika soka la Tanzania.

Tangu kuanzishwa kwake na jitihada za watu wa songea na mfanikio hayo waliyoyapata ni dhahiri ni timu iliyokuwa na maono makubwa.

Haijawahi kuchukua makombe mawili kwenye mwaka mmoja kama timu zingine kwani mwaka 1985 wakati wanachukua kwa mara ya kwanza kombe hili la Muungano bingwa wa bara alikuwa Yanga.

Mwaka 1986 alipochukua kwa mara ya pili mfululizo kombe la Muungano bingwa wa bara alikuwa Tukuyu stars na mwaka 1998 alipochukua kwa mara ya mwisho bingwa wa bara alikuwa ni Yanga.

  1. African Sports: 1988.

Mwaka huu ulikuwa wa mkoa wa Tanga, Coastal union walifanikiwa kuwa mabingwa wa Bara, huku African Sports wakibeba la Muungano, makombe yote yalihamia Tanga wakitoka mikononi mwa Yanga iliyokuwa imeyaweka kabatini kwake. African sports chini mwalimu (Marehemu)Mziray walibeba ndoo hiyo 1988.

  1. Malindi: 1989 na 1992.

Malindi ni kati ya klabu zilizowahi kufanya vizuri kwenye michuano ya CAF, lakini miaka hii miwili ilikuwa ya neema kwao, kwani walibeba vikombe viwili kwa kila mwaka, 1989 walibeba kombe la ligi ya Zanzibar na Muungano, hivyo hivyo mwaka 1992.

Timu hii ilikuwa moja ya timu tishio sana kwa miaka hiyo wakati soka la Zanzibar lilipokuwa juu, jambo lililofanya klabu hiyo kukumbukwa mpaka leo.

  1. Pamba: 1990

Unapozungumzia timu tishio katika miaka ya nyuma huwezi kuisahau Pamba ya Mwanza, ni timu iliyokuwa ikicheza soka la kuvutia kutokana na kuwa na wachezaji wenye vipaji vya hali ya juu.

Pamba walifanikiwa kuchukua Kombe la Muunga mwaka 1990, lakini ilikuwa timu yenye kuvutia katika michuano hiyo kutokana na kusheheni wachezaji mahiri.

  1. Tanzania Prisons: 1999.

Nu mwaka ambao kikosi cha Tanzania Prison kilikuwa bora, hasa baada ya kufanikiwa kulitwaa Kombe la Muungano na kulitua katika Jiji la Mbeya, huku Tukuyu stars ikifanikiwa kunyakuwa Kombe la Ligi 1986.

  1. Simba: 1993, 1994, 1995, 2001 na 2002.

Simba ndio ilikuwa timu pekee kunyakuwa Kombe la Muungano mara 3 mfululizo, tangu kuanzishwa kwa michuano hii 1982 Simba ilihangaika zaidi ya miaka 10 bila mafanikio yoyote hadi ilipofika mwaka 1993 ndipo walipoingia rasmi na kuanza kujimilikisha kombe hili.

Simba wangenyakuwa mara 6 Kombe hilo, kwa staili ya aina yake sababu walibeba 2001 na 2002 kabla ya 2003 michuano hiyo kupotea kabisa.

Katika mara 5 ambazo Simba imebeba ubingwa huu mara tatu kati hizo walikuwa ni mabingwa wa bara pia, yaani 94, 95 na 2001, isipokuwa 93 na 2002 ambapo bingwa wa bara alikuwa mtani wake Yanga.

  1. Yanga: 1983, 1987, 1991, 1996, 1997 NA 2000.

Yanga wana sifa 3 pekee, moja wao wametwaa kombe la Muungano mara nyingi kuliko vilabu vyote vya Jamhuri ya Muungano (mara 6).

Sifa ya pili ni kati ya hizo mara 6, mara moja tu 2000 ndio alikuwa bingwa wa Muungano lakini sio bingwa wa bara, ila mara 5 alikuwa akichukua kotekote.

Kutokana na hilo mpaka sasa hakuna aliyevunja rekodi hiyo na historia itaendelea kubaki hivyo kwamba wao ndio vinara wa michuano hiyo.

Sifa ya 3 sio nzuri kwa Yanga, wao ndio chanzo cha michuano hii kufa. Lakini iliwafungua macho Wazanzibar kuomba uanachama CAF, ili vilabu vyake vishiriki michuano ya kimataifa.

Mpaka sasa miaka 16, tangu michuano ya ligi ya Muungano ife, michuano ambayo ilifanyika kwa miaka 21 mfululizo.