Na mwandishi wetu, TimesMajira online
Ndani ya miaka miwili ya utawala wa Serikali ya Awamu ya Sita, ufanisi wa utekelezaji wa kazi za matengenezo ya barabara zinazosimamiwa na Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Mtwara umekuwa mkubwa.
Akizungumzia mafanikio ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania madarakani, Meneja wa TARURA Mkoa wa Mtwara, Mhandisi Zuena Mvungi anasema hatua hiyo inatokana na kuongezeka kwa vyanzo vya mapato kwa ajili ya fedha za kazi ya matengenezo ya barabara.
TARURA Mkoa wa Mtwara unasimamia mtandao wa barabara wenye jumla ya kilomita 6,133.83, ambazo zimegawanyika katika makundi makuu matatu, barabara kuu za Wilaya zenye urefu wa kilomita 2,666.06, barabara za mjazio zenye urefu wa kilomita 2,932.93 na barabara za jamii zenye urefu wa kilomita 534.81.
Mtandao huo wa barabara, kilomita 117.83 ni za kiwango cha lami, kilomita 1,090.97 ni za kiwango cha changarawe na kilomita 4,925 ni za udongo wa kawaida, jumla ya madaraja 22 na kalavati aina mbalimbali 2,583.Aidha, katika mtandao huo kilomita 1874.07 za barabara sawa na asilimia 31 ziko katika hali nzuri, kilomita 3585.64 sawa na asilimia 58 ziko katika hali ya wastani na kilometa 674.09 sawa na asilimia 11 ziko katika hali mbaya.
Akizungumzia hali ya utekelezaji kabla ya kuongezeka kwa bajeti, Mhandisi Zuena anasema utekelezaji wa kazi za matengenezo ulitegemea chanzo kimoja cha fedha ambapo ni Mfuko wa Barabara.
“Tulitekeleza kazi za matengenezo ya barabara kwa kutumia chanzo kimoja cha fedha cha mfuko wa barabara ambacho kiukweli kilikuwa kinatosheleza kufanya matengenezo ya mtandao kwa asilimia 40 tu ya mtandao mzima sawa na kilomita 2,453.53 kwa mwaka.”
Anasema kuwa mwaka 2021/22, bajeti iliongezeka baada ya kuongezeka vyanzo vya mapato na kuwa vyanzo vitatu ambavyo ni Mfuko wa barabara, Tozo za mafuta na Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo.
Mhandisi Zuena anasema katika mwaka huo, TARURA Mkoa wa Mtwara umeongezewa fedha kutoka chanzo cha Mfuko wa maendeleo ya jimbo Sh bilioni 5, fedha za nyongeza zinazotokana na tozo za mafuta Sh bilioni 8 na kufanya jumla ya Sh bilioni 13 zilizoongezwa kati ya zaidi ya Sh bilioni 8.494.“Ongezeko hilo limefanya bajeti ya TARURA Mkoa wa Mtwara kuongezeka kutoka shilingi bilioni 8.494 hadi kufikia shilingi bilioni 21.981.”
Aidha Mhandisi Zuena anasema katika utekelezaji wa miradi kwa mwaka wa fedha 2021/2022 TARURA Mkoa wa Mtwara imetekeleza ujenzi wa barabara za lami zenye jumla ya kilomita 23, barabara za changarawe zenye jumla ya kilomita 172, barabara za udongo zenye jumla ya kilomita 2388.85, makalavati ya kawaida 113, na maboksi kalavati 27.
Anasema kwa mwaka 2022/23, TARURA Mkoa wa Mtwara umeongezewa fedha kutoka Mfuko wa maendeleo ya jimbo Sh bilioni 5 na fedha za nyongeza zinazotokana na tozo za mafuta Sh bilioni 10.15 na kufanya jumla ya Sh bilioni 15.15 zilizoongezwa kati ya Sh bilioni 8.494.Anasema kuwa ongezeko hilo limefanya bajeti ya TARURA Mkoa wa Mtwara iongezeke kutoka Sh bilioni 8.494 hadi kufikia Sh bilioni 24.131.
Aidha katika utekelezaji wa miradi kwa mwaka wa fedha 2022/2023 TARURA Mkoa wa Mtwara unatekeleza ujenzi wa barabara za lami zenye jumla ya kilomita 19.33, barabara za changarawe zenye jumla ya kilomita 232.8 barabara za udongo zenye jumla ya kilomita 2,587.1, makalvati ya kawaida 73, na maboksi kalavati 33.
Akizungumzia ufanisi wa utekelezaji wa miradi, Mhandishi Zuena anasema tangu kuongezeka kwa bajeti ufanisi wa utekelezaji wa kazi za matengenezo ya barabara umekuwa mkubwa.
Anasema pia hali ya mtandao wa barabara katika Mkoa wa Mtwara umeendelea kuimarika kwa kipindi hiki cha miaka miwili ambayo bajeti iliongezwa.
Mhandisi Zuena anasema kabla ya ongezeko la bajeti uwezo wa TARURA Mkoa wa Mtwara ulikuwa ni kujenga kilomita 2 za lami kwa mwaka lakini kwa sasa inajengwa wastani wa kilomita 20 hadi 25 za lami kwa mwaka.“Pia kabla ya ongezeko la bajeti tulikuwa tunajenga barabara za changarawe kuanzia kilomita 60 hadi 80 kwa mwaka lakini baada ya ongezeko la bajeti tuna uwezo wa kujenga wastani wa kilomita 150 hadi 200 za changarawe kwa mwaka.”
Aidha, Mhandisi Zuena anasema hali ya utekelezaji wa miradi katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Rais Samia, barabara za lami zilizojengwa ni kilomita 42.33, barabara za changarawe ni kilomita 404.8, barabara za udongo ni kilomita 4,975, makalavati 246 na daraja moja.Akizungumzia miradi ya kimkakati, Mhandisi Zuena anasema TARURA Mkoa wa Mtwara kwa mwaka wa fedha 2021/22 imejenga barabara mbalimbali kwa kiwango cha lami ambazo zimeleta taswira mpya kwenye Mkoa wa Mtwara.
Anatolea mfano wa baadhi ya miradi ya kimkakati kuwa ni Barabara ya Ndanda-Miyuyu yenye urefu wa kilimita 3, barabara ya Mangaka-Nachingwea Border kilomita 1.8, barabara ya Ziwani-Msangamkuu yenye urefu wa kilomita 1, barabara ya Nanguruwe-Namahyakata-Mkunwa ya kilomita 1.
Kuhusu mikakati waliojiwekea Mhandisi Zuena anasema TARURA Mkoa wa Mtwara wataendelea kuboresha miundombinu ya barabara kwa kuendelea kuimarisha barabara zilizoko katika hali nzuri kuendelea kuwa nzuri.Anasema pia watahakikisha barabara zilizo katika hali mbaya zinakuwa kwenye hali nzuri na kujenga madaraja na makalavati sehemu zenye mito mikubwa ili kuwezesha barabara zote kupitika katika kipindi chote cha mwaka.
“TARURA Mkoa wa Mtwara tunampongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza miaka miwili madarakani. Pia tunamshukuru kwa kuongeza bajeti ya matengenezo ya barabara pamoja na kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa kutupatia magari manne kwa ajili ya kurahisisha usimamizi na ufuatiliaji wa karibu wa matengenezo ya barabara.”
More Stories
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato
Wambura asikitishwa na makundi CCM Nyakato