May 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

ABAROLI yatoa elimu ya umuhimu wa uhuru wa kujieleza kwa wabunge wa Tanzania

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

TAASISI ya ABAROLI (American Bar Association Rule of Law Initiative) imetoa elimu kuhusu umuhimu wa Uhuru wa kujieleza (Freedom of Expression) kwa maendeleo ya tansia ya habari nchini kwa baadhi ya wabunge wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akifungua warsha hiyo jijini Dodoma,Hakimu Mkazi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (Dodoma),Florah Mhelela amesema ibara ya 18 ya Katiba inatoa haki ya Uhuru wa kujieleza hivyo ni vyema kufanyiwa kazi kama ilivyoelekezwa.

“Bila kuathiri sheria ya nchi kila mtu yupo huru kuwa na maoni yoyote  na kutoa nje mawazo yake,kutafuta habari na ana uhuru wa mawasiliano yake kutoingiliwa kati hivyo ni lazima twende moja kwa moja kujua sheria inasema nini na Katiba inavyotaka,”amesema.

Kwa upande wake mwakilishi wa kundi hilo la Wabunge, Nusrat Hanje amepongeza hatua ya taasisi hiyo kuendelea kupambania ustawi wa tasnia ya habari.

Nusrat ameongeza kuwa hatua hiyo itawawezesha wabunge kuwa katika nafasi nzuri ya kujadili masuala yanayohusu uhuru wa kujieleza,hata hivyo ameshauri taasisi hiyo kuongeza wigo ili waweze kuwafikia wabunge wengi zaidi.

Naye meneja wa mradi huo Violah Ajok amesema ABAROLI imeendelea kutoa elimu hiyo kundi la wabunge kutoka nchi za Afrika Mashariki  ili kuboresha sheria zinazosimamia haki hiyo hususani katika tasnia ya habari.