December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Miaka miwili uongozi wa Samia ilivyounganisha Tanzania kidijiti

Na Joyce Kasiki,TimesMajira,Online Dodoma

MACHI 21, mwaka huu Rais Samia Suluhu Hassan anatimiza miaka miwili tangu aapishwe kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Machi 21, 2021 .

Kama ilivyo kwa wakuu wa nchi wengine duniani, Rais Samia aliposhika wadhifa huo aliweka vipaumle vyake kwa ajili ya kufanikisha dhamira yake ya kuwaletea Watanzania maendeleo katika nyanja za kiuchumi na kijamii.

Aidha msisitizo wake umekuwa ni kuzitaka mamlaka zinazotoa huduma kwa Watanzania kuhakikisha zinatoa huduma bora na za haraka kwa wananchi.

Mfano, wakati akifungua mkutano wa faragha wa mawaziri, manaibu waziri, makatibu wakuu na manaibu makatibu wakuu wiki iliyopita jijini Arusha miongoni mwa mambo aliyosisitiza Rais Samia ni kutaka viongozi hao kuhakikisha wanaongoza wizara zao na taasisi zilizo chini ya wizara hizo kuwaletea maendeleo wananchi.

Miongoni mwa taasisi zinazoguswa moja kwa moja na maelekezo hayo ya Rais Samia ni pamoja na Mamlaka Serikali Mtandao.

Dhamira ya Rais Samia pamoja na mambo mengine ni kuhakikisha anajenga Serikali ya Kidijiti.

Agizo hilo Rais Samia la kujenga Serikali ya kidijiti limeendelea kutekelezwa kwa vitendo na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), ambayo inatekeleza kwa vitendo dhamira ya Rais Samia tangu aingie madarakani.

Agizo hilo la Rais limesaidia huduma nyingi za Serikali kupatikana haraka na mahali popote chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao.

Serikali Mtandao ni matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika utendaji kazi wa Taasisi za Umma na utoaji wa huduma kwa wananchi.

Lengo la Mamlaka ya Serikali Mtandao ni kuongeza ufanisi wa utendaji kazi katika Taasisi za Umma pamoja na kuboresha utoaji wa huduma kwa umma ili huduma hizo zipatikane kwa urahisi, haraka na kwa gharama nafuu kupitia TEHAMA.

Hatua hiyo inalenga kupanua uwezo wa Mtandao wa Mawasiliano Serikalini na kuufikisha katika Wilaya zote nchini ili kurahisisha utekelezaji wa jitihada za Serikali kama ambavyo Rais Samia amedhamiria.

Kutokana na umuhimu wa maelekezo ya Rais Samia, Mamlaka haya imeendelea kutekeleza dhamiranya Rais Samia.

Katika makala haya, Mwandishi Wetu, anaelezaji jinsi taasisi hiyo iliyoweza kutekeleza wajibu wake kwa kuzingatia maelekezo ambayo yamekuwa yakitolewa na Rais Samia kama ambavyo inaelezwa na Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Serikali Mtandao, Benedict Ndomba.

Ndomba anaeleza kwamba Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) ilianzishwa kwa Sheria ya Serikali Mtandao Na. 10 ya mwaka 2019, ikiwa na majukumu ya kuratibu, kusimamia na kukuza jitihada za Serikali Mtandao, pamoja na kusimamia uzingatiaji wa Sera, Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao katika Taasisi za Umma. Hivyo basi, Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) ndiyo yenye dhamana ya kusimamia Serikali Mtandao nchini.

Ndomba anasema Mamlaka imekuwa ikitekeleza jitihada mbalimbali za Serikali Mtandao katika Taasisi za Umma tangu kuanzishwa kwake mwaka 2012.

Awali Taasisi hii ilijulikana kama Wakala ya Serikali Mtandao na baada ya kutungwa kwa Sheria ya Serikali Mtandao No. 10 ya mwaka 2019, ilipewa hadhi ya Mamlaka.

Chini ya uongozi wa Rais Samia ambaye Machi 21 anatimiza miaka miwili tangu aapishwe kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Watanzania tumeshuhudia Serikali yake ikiongeza kasi ya utengenezaji wa mifumo ambayo inapunguza kwa kiasi kikubwa gharama za uendeshaji Serikali anayoiongoza.

Ipo mifano mingi ambayo ni kielelezo cha hayo, mfano tumeshudia Mamlaka ya Serikali Mtandao inasimamia uendeshaji na uendelezaji miundombinu ya pamoja ya TEHAMA
inayotumiwa na Taasisi mbalimbali za Umma kwa pamoja, hivyo kupunguza gharama kwa Serikali.

Tumeshuhudia chini ya uongozi wa Rais Samia utengenezaji wa mifumo ambayo imepunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ya karatasi Bungeni na kwenye Baraza la Wawakilishi, hivyo kupunguza gharama za uendeshaji.

Aidha, tumeshuhudia uanzishwaji Mfumo unawawezesha wananchi kuwasiliana moja kwa moja na Taasisi za Umma kwa njia ya kidigitali, ili kuwasilisha maoni, mapendekezo, maulizo, pongezi au malalamiko yao sambamba na kufuatilia utekelezaji wake ndani ya Taasisi husika. Taasisi za Umma 398 zinatumia Mfumo huu.

Mamlaka hiyo imekuwa kinara cha kusimamia utekelezaji na uzingatiaji wa Sera, Sheria, Kanuni, Viwango, Taratibu na Miongozo ya Serikali Mtandao kwa kutengeneza Miongozo na Viwango vya Serikali Mtandao inayopatikana.

Rais Samia Suluhu Hassan

Pili, Ndomba anasema imekuwa ikipitia na kupitisha Miradi ya TEHAMA ya Taasisi za Umma. Katika kipindi hiki miradi 340 imepitiwa na kuthibitishwa.

Aidha, anasema imejengea uwezo taasisi za umma kutekeleza Jitihada za Serikali Mtandao.

Taasisi mbalimbali za Umma zimewezeshwa kutekeleza jitihada za Serikali Mtandao kwa kutoa Mafunzo mbalimbali kama vile, Usimamizi wa Mtandao wa Mawasiliano wa Serikali kwa Taasisi 240, kutoa mafunzo ya mfumo wa Baruapepe kwa Taasisi 611, kutoa mafunzo ya usimamizi wa tovuti kwa Taasisi 492.

Kwa mujibu wa Ndomba, Mamlaka hiyo imekuwa ikishirikiana na Wadau wa utekelezaji wa Serikali Mtandao.

“Mamlaka inashirikiana na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi, zikiwemo Taasisi za Elimu ya Juu na Utafiti, Sekta binafsi pamoja na Kuandaa Vikao Kazi vya Mwaka vya Serikali Mtandao ili kuwakutanisha wadau mbalimbali, ambapo katika kikao kazi kilichofanyika Februari mwaka huu (2023) ambapo jumla ya washiriki 1,624 walihudhuria, ambao ni Wakuu wa Taasisi za Umma, Wataalamu wa TEHAMA na watumiaji wa TEHAMA katika Taasisi za Umma,” anasema.

Aidha, Ndomba anafafanua kwamba Mamlaka inashirikiana na Wakala ya Serikali Mtandao Zanzibar (eGAZ) kwa lengo la kuhakikisha Serikali Mtandao inaimarika kote Bara na Visiwani.

“Kupitia ushirikiano huu, Mifumo kadhaa imeboreshwa na inatumiwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ). Mifumo hii ni pamoja na Mfumo wa Barua Pepe Serikalini, Mfumo wa Masjala, Mfumo wa Malipo Zanzibar (ZanMalipo), Mfumo wa Ajira (ZanAjira), e-Wawakilishi na Mfumo wa Ankara za Maji (MAJIIS) kwa ajili ya Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA).

Pia, Mamlaka inashirikiana na eGAZ katika utoaji wa huduma ya miundombinu ya Serikali mtandao,” anasema Ndoma.

Anaendelea kwamba imekuwa ikitoa Ushauri wa Kiufundi kwa Taasisi za Umma katika utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao na matumizi sahihi na salama ya huduma za Serikali mtandao.

Aidha, Mamlaka imekuwa ikitambua matishio ya kiusalama mitandaoni na kuainisha hatua za kuchukuwa ili kukabiliana nayo.

Anasema Mamlaka imeandaa ripoti za usalama wa Mifumo ya TEHAMA ya Taasisi za Umma na kufuatilia utekelezaji wake, imetoa mafunzo mbalimbali kwa Taasisi za Umma kuhusu usalama wa kimtandao, na imeandaa na kutoa miongozo ya kiufundi ya usalama wa Mifumo ya TEHAMA.

Imekuwa ikifanya shughuli za Kufanya Shughuli za Utafiti, ubunifu na Kutoa Mafunzo ya Huduma za Serikali Mtandao. Mamlaka inaratibu tafiti mbalimbali za maendeleo ya jitihada za Serikali mtandao na kubuni Mifumo inayoendana na mahitaji yetu na itakayosaidia kuboresha utendaji kazi katika Taasisi za Umma na utoaji wa huduma kwa Umma, pamoja na kujengea uwezo na kukuza vipaji vya vijana wa kitanzania katika eneo la Serikali mtandao.

Aidha, anasema imejenga Mifumo na Miundombinu Shirikishi na ya Kisekta ya TEHAMA katika Taasisi za Umma.

Ndomba anasema Mamlaka imeendelea kusanifu, kujenga na kusimamia uendeshaji wa Mifumo tumizi inayotumiwa katika Taasisi za Umma kwa pamoja (shirikishi). Baadhi ya Mifumo hiyo ni pamoja na Mfumo wa baruapepe Serikalini (GMS).

Mfumo huu unaziwezesha Taasisi za Umma kuwasiliana na kubadilishana taarifa kwa usalama, haraka na kwa gharama nafuu ambapo jumla ya Taasisi 616 zinatumia Mfumo huu.

“Mfumo wa Ofisi Mtandao jumla ya Taasisi 200 zinatumia Mfumo huu. Aidha Mfumo wa Ofisi Mtandao mbali na kurahisisha utendaji kazi katika Taasisi za Umma pia umesaidia kupunguza matumizi ya karatasi na kwa upande mwingine umesaidia kutunza mazingira na kuokoa fedha za Serikali,” anasema Ndomba na kuongeza:

“Mfumo wa Utoaji Huduma za Serikali kwa Simu za Mkononi (MGov) Mfumo wa mGOV umeunganishwa na watoa huduma wote wa simu za mikononi nchini Tanzania.

Hadi sasa, Taasisi zaidi ya 275 zimeunganishwa na kuutumia Mfumo wa mGOV kutoa huduma. Baadhi ya huduma hizo ni jumbe fupi yaani SMS za ununuzi wa umeme (LUKU), SMS za huduma za malipo ya Serikali (GePG), Ankara za maji, malipo ya Ardhi.”

Kuhusu Mfumo wa Ubadilishanaji Taarifa Serikalini ‘Government Enterprise Service Bus’ (GovESB), Ndomba anasema Mfumo huu unawezesha Mifumo mbalimbali ya Serikali kuwasiliana na
kubadilishana taarifa.

Kwa mujibu wa Ndomba Taasisi zaidi ya 50 zimewezeshwa Mifumo yake kubadilishana taarifa kupitia Mfumo huu.

Anatoa wito kwa Taasisi za Umma ambazo hazijaunganisha Mifumo yake katika Mfumo huu, kuunganisha ili ziweze kubadilishana taarifa na Taasisi
nyingine pale inapohitajika.

“Mfumo wa e- Mikutano Mfumo huu unaziwezesha Taasisi za Umma kufanya vikao na mikutano kwa njia ya mtandao hadi kufikia Januari 2023, Taasisi za Umma 192 zimekuwa zikitumia Mfumo huu,”anasema Ndomba.

Anaongeza kwamba Mamlaka kwa kushirikiana na Taasisi mbalimbali za Umma, imefanikiwa kutengeneza Mifumo
mbalimbali ya kisekta inayotumika katika Taasisi hizo.
Baadhi ya Mifumo hiyo ni pamoja na Mfumo wa Ukusanyaji wa Malipo ya Serikali Kielektroniki (GePG) (umetengenezwa
na Mamlaka kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango).

“Mfumo huu unaimarisha uwazi na udhibiti katika ukusanyaji mapato ya Serikali. Kupitia Mfumo huu,
Serikali inao uwezo wa kufahamu mapato yanayoingia kila siku.

Mpaka sasa kuna Taasisi na vituo vya kutolea huduma 948 zinatumia Mfumo huu. Mfumo wa Pamoja wa Utoaji Ankara kwa Mamlaka za Maji Nchini (MAJIIS) (umetengenezwa na Mamlaka kwa kushirikiana na Wizara ya Maji).

Anasema Mfumo huu unarahisisha uendeshaji na usimamizi wa shughuli za Mamlaka za maji na Bodi za maji
za Mabonde nchini Tanzania.

Mamlaka za maji 94 zimeunganishwa kwenye Mfumo huu. Mfumo wa Pamoja wa Uondoshaji wa Shehena Maeneo ya Forodha (TeSWS) (umetengenezwa na Mamlaka kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) pamoja na Taasisi mbalimbali
za udhibiti wa shughuli za forodha.

Mfumo huu umelenga kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji. Mpaka sasa unatumiwa na zaidi ya Mawakala wa forodha 800.

Kwa Bunge Mtandao , anasema umetengenezwa na Mamlaka kwa kushirikiana na Ofisi ya Bunge. Mfumo huu hutumika kuendesha shughuli za Bunge na kuhifadhi taarifa za Bunge kama vile Miswada na Sheria, Hotuba, Kumbukumbu za vikao vinavyofanyika katika vipindi vya Bunge.

Anasema Mfumo huu umewezesha kupunguza kwa kiasi kikubwa sana matumizi ya karatasi Bungeni na kwenye Baraza la Wawakilishi, hivyo kupunguza gharama za uendeshaji.

Aidha, anasema Mfumo huu unawawezesha wananchi kuwasiliana moja kwa moja na Taasisi za Umma kwa njia ya kidigitali, ili kuwasilisha maoni, mapendekezo, maulizo, pongezi au malalamiko yao sambamba na kufuatilia utekelezaji wake ndani ya Taasisi husika.

Mfumo wa Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (MUVU).
Nodomba anasema mfumo huu umetengenezwa na Mamlaka kwa kushirikiana na Tume ya Maendeleo ya Ushirika) Mfumo huu unarahisisha Ukaguzi, Usimamizi, na Uendeshaji wa vyama vya ushirika ili kuongeza Ufanisi, Uwazi na Uwajibikaji utakaoboresha utendaji na kuchochea mabadiliko ya Kiuchumi.

Anasema Mikoa 26 imeunganishwa na vyama vya ushirika Zaidi ya 3740 vimeandikishwa kwenye Mfumo.

Anaongeza kwamba Mfumo wa Uendeshaji Shughuli za Wakala wa Ununuzi Serikalini (GIMIS). Umetengenezwa na Mamlaka kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma ya Ununuzi
Serikalini (GPSA).

Anaeleza kuwa Mfumo huu unarahisisha uendeshaji na usimamizi wa shughuli za Wakala, pia unaziwezesha Taasisi kupata huduma za ununuzi wa vifaa, mafuta na magari kutoka kwa wakala pamoja na huduma ya ugomboaji na uondoshaji wa mizigo.

Ndomba anasema Usanifu na Ujenzi wa Tovuti katika Taasisi za Umma, Mamlaka imesanifu na kutengeneza Tovuti zaidi 350 za Taasisi za Umma, ikiwemo Tovuti Kuu ya Serikali na
Tovuti Kuu ya Ajira.

Aidha, baada ya Mamlaka kutengeneza Tovuti hizo, ni jukumu la Taasisi husika kuhuisha taarifa za kwenye tovuti zao, Mamlaka inasimamia masuala ya kiufundi katika tovuti hizo.

Aidha, anasema Mamlaka inasimamia uendeshaji na uendelezaji miundombinu ya pamoja ya TEHAMA inayotumiwa na Taasisi mbalimbali za Umma kwa pamoja, hivyo kupunguza gharama kwa Serikali.