May 3, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Miaka mitatu ya Rais Samia mapato yaongezeka TANAPA

*Idadi ya watalii yazidi kumiminika nchini

Na Hamisi Miraji, Timesmajira Online

SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), limesema katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kumekuwepo na ongezeko la mapato kutoka shilingi 174,715,158,494 (2021/2022) hadi kufikia shilingi 337,424,076,896 (2022/2023).

Ongezeko hilo ni sawa na shilingi 162,708,918,402 ambayo ni asilimia 94%, kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watalii.

Hayo yamesemwa leo na Kamishna wa Uhifadhi kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Juma Juma Kuji kwenye kikao kazi kati ya TANAPA na Wahariri wa vyombo vya habari chini.

Kikao kazi hicho kimeratibiwa wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR), ili kueleza mafanikio ya utekelezaji wa shughuli za TANAPA katika kipindi cha miaka mitatu ya serikali ya awamu ya sita.

Akizungumzia hilo Kamishina Kuji amesema, idadi ya watalii nchini imeongezeka kutoka watalii 997, 873 kwa mwaka wa fedha 2021/2022 hadi kufikia 1,670,437 kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Amesema, kwa mwaka huu wa fedha 2023/2024 kuanzia Julai 2023 hadi Machi 19, 2024 idadi ya watalii walikuwa 1,514,726.

Aidha, amesema watalii wa ndani ni 721,543, uku watalii kutoka Mataifa mbalimbali wakiwa 793,183.

Amefafanua kuwa, watalii waliotembelea Hifadhi za Taifa ni sawa na ongezeko la asilimia 5 ikiwa ni zaidi ya lengo la kupokea watalii 1,387,987 (wa nje 827,713 na watalii wa ndani 726,676) katika kipindi husika.

Hata hivyo amesema, idadi ya watalii wanaotarajiwa kutembelea Hifadhi za Taifa kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ni 1,830,081 (watalii wa nje 963,413 na watalii wa ndani 866,667).

Ameeleza kuwa, kipindi cha miaka mitatu kumekuwepo na ongezeko la siku za kukaa wageni kutoka wastani wa siku 1,749,194 katika mwaka wa fedha 2021/2022 hadi kufikia wastani wa siku 2,669,586 kufikia Februari 2024.

Pia, amesema katika mwaka wa fedha 2023/2024 kuanzia mwezi Julai 2023 hadi Machi 19, 2024 Shirika limefanikiwa kukusanya shilingi 340,101,108,465 ukilinganisha na matarajio ya kukusanya shilingi 295,466,811, 506 mpaka Machi 2024.

Kamishna Kuji amesema mapato ya sasa yanazidi mapato ya shilingi 282,450,446,103 yaliyokusanywa mwaka 2018/2019 kabla ya janga la UVIKO – 19, ambayo yalikuwa ndio kiwango cha juu cha mapato katika Shirika hilo.

“Ongezeko la watalii na mapato yanakwenda pamoja na malengo ya Ilani ya Chama Chama cha Mapinduzi (CCM) mwaka 2020 – 2025 inayoelekeza idadi ya watalii nchini kufikia milioni 5 na mapato ya dola za kimarekani Bilioni 6 kwa mwaka ifikapo mwaka 2025.

“Kumekuwa na ongezeko la masoko mapya ya Utalii yenye idadi kubwa ambayo inatoa uhakika wa kuendelea kupokea watalii wengi kuja kutembelea Hifadhi za Taifa,” amesema Kamishna Kuji.

Amesema, masoko hayo mapya ni pamoja na China, Urusi, Ukraine, Poland, Jamhuri ya Czech na Israeli, pamoja na kutambulika kimataifa na kupata Tuzo mbalimbali ikiwemo “Best Practice Award” ambayo hutolewa kila mwaka na taasisi ya “European Society for Quality Research – ESQR”.

“Tuzo hii ya utoaji wa huduma bora kimataifa hutolewa na taasisi hiyo baada ya kutambua taasisi za Serikali na zisizo za Kiserikali pamoja na watu binafsi wanaotoa huduma za ubora wa viwango vya hali ya juu kimataifa” amesema

Mbali na hivyo pia, amesema kumekuwa na ongezeko kwa Uwekezaji wa maeneo ya malazi na wawekezaji katika Hifadhi za Taifa ambao umelenga kuboresha huduma za malazi katika Loji, kambi za kudumu (Permanent Tented Camps – PTC), Kambi za Muda (Seasonal Camps), Kambi za Jumuiya (Public Camp Sites), Mabanda (cottages) pamoja na Hosteli.

Hata hivyo amesema, uwekezaji huo umeongeza idadi ya vitanda kutoka vitanda 5,755 mwaka 2021 hadi vitanda 10,094 mwaka 2024, huku akieleza kuwa ujenzi wa malazi unaendelea wenye uwezo wa vitanda 1,148 ambapo ukikamilika kutakuwa na vitanda 11,242.

Kamishana huyo amesema, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wakiwemo Benki ya Ujerumani (KfW), Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) imeendelea kufanya maboresha (kujenga na kukarabati) miundombinu ya barabara na viwanja vya ndege vilivyopo katika Hifadhi za Taifa.

Shirika pia, lina mtandao wa barabara ambao umeongezeka kutoka urefu wa kilometa 7,638 mwaka 2021 na kufikia urefu wa kilometa 16,471 mwaka 2024.

“Tumekarabati barabara ya wastani wa kilometa 3,938, tumetengeneza njia za kutembea kwa miguu zenye urefu wa kilomita 334, kuna ujenzi wa madaraja 14, kukarabati vivuko 399 na viwanja vya ndege (Airstrips) 11 katika maeneo ya barabara za kuruka na kutua ndege (runway) na viungio vyake pamoja na maegesho ya ndege kwa kiwango cha changarawe katika hifadhi” amesema

Shirika limeendelea kufanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha kuwa linabuni vyanzo mbalimbali vya mapato ambavyo vitaliingizia Shirika fedha na kuongeza ukusanyaji wa mapato.

Miongoni mwa vyanzo bunifu vya mapato ambavyo vimeendelea kuibuliwa na Shirika ni pamoja na; Kuanzishwa kwa Kampuni Tanzu ya Uwekezaji ya Shirika (TANAPA Investment Limited – TIL) inayolenga kuimarisha usimamizi na utekelezaji wa miradi ya kimkakati na pia kuwa chanzo kikubwa cha mapato kwa Shirika kwa kutekeleza miradi mbalimbali.