November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan

Miaka mitatu ya Rais Samia imekuwa chachu ya maendeleo

TimesmajiraOnline,,Dar

LEO Rais Samia Suluhu Hassan, ametimiza miaka mitatu tangu alipoapishwa kushika wadhifa huo, mwaka 2021.

Rais Samia aliapishwa kushika wadhifa huo kufuatia kifo cha Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano, Hayati John Magufuli. Rais Samia akiwa mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo, ameweza kuongoza Serikali ya Awamu ya Sita kwa mafanikio makubwa.

Tangu Rais Samia ashike wadhifa huo, kila sekta imepata mafanikio ambayo ni kipimo tosha, kwamba kiongozi huyo anatosha kwenye kiti hicho.

Sisi kama chombo cha habari tunaungana na Watanzania kumpongeza Rais Samia, kwani tunaona kila kinachofanyika hapa nchini ili kuwaletea maisha bora Watanzania.

Ni vigumu kuainisha mambo yote ambayo kiongozi amefanya, lakini kwa uchache mno, tumeshuhudia Rais Samia akiboresha mazingira ya ufanyaji biashara, ambapo aliweka wazi kwamba katika kipindi cha uongozi wake hataki kodi za dhuluma.

Tunashukuru kwa hilo, kwani maelekezo yake yamefanya Tanzania kuwa kimbilio la wawekezaji na inaongoza kwa mazingira mazuri ya uwekezaji barani Afrika.

Ukienda sekta ya elimu, leo hii Tanzania ina sera mpya ya elimu ambayo italeta mapinduzi makubwa ya elimu hapa nchini.
Tumeshuhudia wanafunzi wote wanaomaliza darasa la saba wakianza kwa pamoja kidato cha kwanza, kinyume na ilivyozoeleka, elimu bure kwa sasa ni kuanzia shule za msingi hadi kidato cha sita, hii haikuwa kutokea ndani ya nchi yetu.

Lakini pia, Rais Samia ameongeza kiwango cha mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na kuanza kutoa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vya kati, hivyo kumaliza kilio cha muda mrefu cha vijana na wengi nchini.

Lakini pia ameanzisha Programu ya Ufadhili iitwayo SAMIA SCHOLARSHIP kwa masomo ya shahada ya kwanza kwa wanafunzi waliopata ufaulu wa juu katika mitihani ya kidato cha sita.

Programu hii imeanza tangu mwaka 2023 na wanufaika ni wanafunzi wa katika Tahasusi za Sayansi (PCB, PCM, PGM, CBG, CBA, PMC na CBN).

Kwa upande wa Wizara ya Afya amefanya mageuzi makubwa ikiwemo uwekezaji kwenye miundombinu, vifaa tiba, kwa wataalam wa sekta hiyo na kutoa ufadhili kwa ya udaktari bingwa na bobezi.

Kimsingi hakuna sehemu ambayo mkono wa Rais Samia haujagusa katika uongozi wake. Mfano, katika medani ya siasa, wakati anaingia madarakani, alikuta hali ya kisiasa hapa nchi sio nzuri, ambapo baadhi ya Watanzania walikimbia nchi kwa kile walichodai kuhofia usalama wao.

Lakini chini ya uongozi wa Rais Samia, wote wamerejea nchini na wanaendelea na shughuli zao za kisiasa kama kawaida. Aidha, ile mikutano ya kisiasa na maandamano yaliyokuwa yamezuiwa tangu mwaka 2016, baada ya kuingia madarakani alifuta zuio la mikutano hio.

Lakini pia kupitia falsafa yake ya R4 tunashuhudia jinsi alivyoweza kuunganisha Taifa letu pamoja, wanasiasa wanaendesha siasa kwa uhuru, wanaandamano na kufanya mikutano kwa amani na uhuru.

Haya yote hakuna aliyetarajia kuyaona kama asingekuwa Rais Samia. Sisi kama chombo cha habari tunamuahidi kwamba tutaendelea kumuunga mkono ili aweze kutimiza azma yake ya kuwaongoza Watanzania na kuwaletea maendeleo kama alivyokusudia.

Kama alivyoahidi kwamba Watanzania hawana sababu ya kutazama mbele mashaka, na hilo linaoneka wazi wazi na kilichobaki ni sisi kufanyakazi ya ili kuunga mkono juhudi zake.