March 12, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Miaka minne ya Rais Samia TRA yaongeza makusanyo ya kodi kwa asilimia 78

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

MAMLAKA ya Mapato Tanzania(TRA)imesema
kwa kipindi cha miezi nane mfululizo kuanzia Julai 2024 mpaka Februari 2025 imekusanya kiasi cha Shilingi Trilioni 21.200 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2020/2021 ambapo ilikusanya Sh. Trilioni 11.9.

Hayo yamesemwa jijini hapa leo Machi 12,2025 na Kamishna Mkuu wa TRA,Yusuph Mwenda akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na muelekeo wa Mamlaka hiyo katika kipindi cha miaka minne ya  Serikali ya awamu ya sita ambapo amesema makusanyo hayo ni sawa na ongezeko la asilimia 78 na ukuaji wa asilimia 17.

Mwenda amesema kuwa makusanyo hayo yaliyofanywa katika kipindi cha Serikali ya awamu ya sita yamevunja rekodi ya makusanyo tangu kuanzishwa kwa TRA mwaka 1996 na hayo yote yametokana Mamlaka hiyo kutekeleza maelekezo yanayotolewa na  Rais Dkt.Samia.

Vilevile ametaja mafanikio mengine yaliyopatikana kuwa ni kuwezesha kukua kwa biashara na uwekezaji nchini wakishirikiana na Taasisi nyingine kama TIC katika kuvutia wawekezaji na kwa upande wa marejesho ya Kodi kwa Wafanyabiashara kwa kipindi cha miezi 8 wamelipa Sh. Trilioni 1.171 wakati kipindi kama hicho miaka minne iliyopita ililipwa Sh. Bilioni 92.

Akizungumzia Mifumo inayotumiwa na Mamlaka hiyo Mwenda amesema upo mfumo wa TANCIS ulioboreshwa unaofanya kazi za Forodha na mfumo wa IDRAS unaoshughulikia Kodi za ndani ambao unawezesha Mlipakodi kujihudumia mwenyewe hali iliyopunguza Watumishi wa TRA kukutana na Walipakodi.

“Elimu kwa Mlipakodi ni miongoni mwa vitu vilivyochangia kuongeza kwa makusanyo ya Kodi pamoja na Shukrani kwa Mlipakodi ambapo tumeenda mikoa yote kuwashukuru Walipakodi na kusikiliza changamoto zao pamoja na kuzipatia ufumbuzi,”amesema Mwenda.

Aidha ametaja siri nyingine ya mafanikio ni kuendelea kuimarika kwa nidhamu miongoni mwa watumishi huku akitaja hatua zilizo chukuliwa kwa baadhi ya watumishi waliokiuka taratibu za kazi ambapo amesema  watumishi 15 walifukuzwa kazi kwa makosa mbalimbali ya kinidhamu,watumishi sita wamepunguziwa mishahara,12 wameshushwa vyeo na mishahara na watumishi 22 wamepewa onyo la maandishi.

Akitaja mafanikio mengine Mwenda amesema ni kuongezeka kwa idadi ya watumishi wa TRA kutoka 4749 miaka minne iliyopita na kufikia watumishi 6989 mwaka 2025 ambapo wanatarajia kuajiri watumishi wapya 1596 watakaofanya Mamlaka iwe na watumishi 8585 sawa na ongezeko la asilimia 80.

Pamoja na hayo amesema mwelekeo wa TRA ni kuendelea kutekeleza kwa vitendo maagizo wanayopatiwa na Rais Dkt.Samia ili kuweka mazingira mazuri kwa Walipakodi na kuongeza makusanyo ya Kodi.