March 19, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Miaka Minne ya Rais Samia Madarakani,Tanzania mlango wa mataifa mengine kujifunza uchimbaji mdogo

Na Mwandishi wetu, Timesmajira


Tanzania imefanikiwa kuwa kivutio cha mataifa mengine Barani Afrika kujifunza kuhusu shughuli za uchimbaji mdogo na usimamizi wa Sekta ya Madini kwa ujumla. Jambo hili halikutokea tu kwa bahati mbaya bali ni kutokana na hatua kadhaa zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita ikiwemo usimamizi madhubuti wa Sekta ambapo pamoja na mambo mengine, imefanya maboresho ya Sheria na Kanuni zinazosimamia shughuli za uchimbaji mdogo, kurasimisha shughuli za wachimbaji wadogo, kusogeza huduma za uchimbaji na biashara ya madini ambayo imeleta mageuzi makubwa katika Sekta ya Madini nchini.

Hatua hiyo imeyavuta mataifa kadhaa kutoka Barani Afrika kujifunza Tanzania kuhusu usimamizi wa Sekta ya Madini na hususan eneo la shughuli za uchimbaji mdogo wa madini. Nchi hizo ambazo zimefika nchini na nyingine zaidi ya mara moja ni pamoja na Uganda, Kenya, Zimbabwe, Burundi, Malawi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na Zambia.

Matokeo hayo yametokana na Serikali kuendelea kusogeza huduma muhimu kwa wachimbaji wadogo kama vile masoko ya madini, mitambo ya uchorongaji, nishati ya umeme, barabara, programu maalum za uchimbaji wenye tija, kuwaunganisha na taasisi za fedha pamoja na kuwapatia leseni za uchimbaji. Makala hii fupi inajaribu kuanisha matokeo ya juhudi hizo za serikali ambazo zimeifanya Tanzania kuwa mfano kwa mataifa mengine.

Masoko ya Madini
Serikali ilianzisha masoko ya madini kuwaondolea adha wachimbaji wadogo na wafanyabiashara wa madini ili wapate sehemu ya kukutana kufanya biashara bila kificho. Uwepo wa Masoko ya madini na vituo vya ununuzi vimeongeza uwazi, uwepo wa bei elekezi, uhakika wa masoko na bidhaa zinazopita sokoni na yameongeza mapato yanayotokana na madini, mathalan, katika Mwaka wa Fedha 2021/22 mauzo ya Madini katika masoko ya madini yameongezeka kutoka shilingi bilioni 2.361.80 hadi bilioni 2.597 Mwaka wa Fedha 2023/2024. Hadi sasa kuna jumla ya masoko ya madini 43 na vituo vya ununuzi 109 Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2019.

Leseni za uchimbaji madini
Wizara kupitia Tume ya Madini imetoa jumla ya leseni 41,424 kati ya 37,318 zilizopangwa kutolewa katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita ambayo ni sawa na asilimia 111. Leseni hizo zinajumuisha leseni za uchimbaji mkubwa, uchimbaji wa kati na uchimbaji mdogo.

Maeneo ya uchimbaji
Ili kuhakikisha watanzania wengi wanashiriki katika uchumi wa madini na wachimbaji wadogo wanapata maeneo ya kuchimba, Wizara kupitia Tume ya Madini imetenga maeneo 58 kwa ajili ya uchimbaji mdogo ikiwemo mazingira rafiki kwa ajili ya kuchimba.

Nishati ya Umeme Yawafikia Wachimbaji Wadogo
Kama inavyofahamika, umuhimu wa nishati ya umeme katika shughuli za kila siku. Kadhalika, kwenye Sekta ya Madini ili shughuli za madini zifanyike kwa ufasaha kwa matokeo, nishati ya umeme ni kiungo muhimu katika kufanikisha masuala hayo. Katika kipindi cha miaka Minne ya Serikali ya Awamu ya Sita Serikali imeendelea kuhakikisha kuwa miundombinu mbalimbali katika shughuli za uchimbaji inaboreshwa ili kuongeza mapato na tija kwa wachimbaji. Hadi kufikia mwaka 2023 zaidi ya migodi 350 ya wachimbaji wadogo imeunganishwa huduma ya nishati ya umeme.

Mitambo ya Uchorongaji Miamba
katika kuwawezesha wachimbaji wadogo kuchimba kwa tija, Oktoba 21, 2023, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu alizindua Mitambo Mitano (5) ya uchorongaji kwa ajili ya wachimbaji wadogo pamoja na vifaa kazi vingine vya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) vyenye thamani ya jumla ya shilingi 9,178,559,128. Mitambo hiyo ni msaada mkubwa kwa wachimbaji wadogo kwani inawasaidia kupata taarifa za kijiolojia katika maeneo yao hivyo kuondokana na uchimbaji wa kubahatisha, inawawezesha kupata taarifa sahihi za uwepo wa madini katika maeneo yao kwa kutambua umbali na kiwango cha madini kilichopo na hivyo kuchimba kwa tija. Hadi sasa wachimbaji 23 wamefanyiwa uchorongaji na zaidi wa mita Elfu Sita Mia Tisa Ishirini na Tisa (6929) zimechorongwa. Aidha, Serikali inatarajia kuongeza mitambo mingine 10 itakayotengwa kwa ajili ya wachimbaji wanawake na vijana.

Vituo vya Mfano Vyaongeza Mapato, Hamasa kwa Watanzania Kuchimba
Serikali ilianzisha Vituo vya Mfano kwenye maeneo yenye shughuli za uchimbaji ili kutoa mafunzo ya uchimbaji na uchenjuaji bora. Vituo hivyo vimewawezesha wachimbaji kupata elimu huku Serikali ikinufaika na mapato kutokana na kodi mbalimbali. Kutokana na uwepo wake, vimewahamasisha watanzania na wachimbaji kuchimba na baadhi kuanzisha mitambo ya uchenjuaji Mathalan, Mkurugenzi wa Kampuni ya Hexad, Fortunatus Luhemeja ni moja ya wachimbaji ambao wamekiri waziwazi kunufaika na vituo vya Lwamgasa na Katente Geita vilivyopelekea kuongeza uzalishaji katika mgodi wake na kuanzisha kiwanda cha uchenjuaji.

Aidha, Christopher Kadeo, mchimbaji mwenye uzoefu wa takribani miaka 40 kwenye uchimbaji mdogo, anakiri manufaa ya uwepo wa vituo hivyo kwenye shughuli zake kwa namna vilivyombadilisha. Aidha, uwepo wa Kituo cha Ketente kimewezesha kuongeza maduhuli katika Mkoa wa Kimadini Mbogwe ambapo baada ya kusogezwa kwa huduma hizo Kituo hicho katika Mwaka wa Fedha 2021/22 Mkoa huo ulikusanya shilingi bilioni 21.3, Mwaka wa Fedha 2022/23 shilingi bilioni 22.4 na Mwaka wa Fedha 2023/24 shilingi bilioni 27.1 zilikusanywa.

Taasisi za fedha Zajenga Imani kwa Sekta ya Madini
Miongoni mwa changamoto zinazowakabili wachimbaji wadogo ni pamoja na ukosefu wa mitaji. Kwa kuliona hilo, Wizara kupitia STAMICO ilisaini hati za makubaliano na baadhi ya taasisi za fedha ikiwemo CRDB, KCB na NMB ili kutoa mikopo kwa wachimbaji wadogo kuwawezesha waongeze uzalishaji na kuchimba kwa tija. Katika kipindi cha Julai 2023 hadi Machi 2024, jumla ya shilingi bilioni 187 zilikopeshwa kwa wachimbaji ikilinganishwa na shilingi bilioni 145 zilizokopeshwa mwaka 2022. Aidha, STAMICO imechukua hatua kadhaa ikiwemo kuandaa mpango kutoa elimu kwa kuzunguka nchi nzima, kusaini makubaliano na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania GST kuwezesha kupatikana wa taarifa za kijilojia zitakazowezesha taasisi za fedha kujenga Imani na wachimbaji.

Ongezeko la Maduhuli ya Serikali kutokana na shughuli za uchimbaji mdogo
Jitihada za Serikali kuboresha shughuli za uchimbaji mdogo nchini zimetengeneza fursa za kiuchumi kwa wachimbaji wadogo na hivyo kupelekea kuongezeka kwa maduhuli ya Serikali yanayotokana na shughuli hizo kufikia asilimia 40 ya sasa kutoka 4 kabla ya maboresho ya Sheria ya Madini.

Program Maalum ya Mining For Brighter Tomorrow
Katika kuhakikisha watanzania wengi zaidi wanashiriki uchumi wa madini, Wizara ya Madini iko kwenye mchakato wa kuandaa Program ya Mining For Brighter Tomorrow-MBT, inayolenga kuwainua wachimbaji wanawake na vijana huku kipaumbele kikiwekwa kwenye utoaji wa leseni katika maeneo ya uchimbaji, na kunufaika na vitendea kazi ikiwemo magari, vifaa na mitambo ya uchimbaji. Program hiyo inalenga kuchochea ukuaji wa sekta ya madini, uchumi wa Taifa na kuongeza ajira kwa watanzania.


Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuboresha sekta ya uchimbaji mdogo kupitia hatua kama vile kuboresha miundombinu, huduma za kisheria, hivyo kusaidia wachimbaji wadogo kuongeza tija na mapato.

Mitambo ya uchorongaji, vituo vya mfano, na ushirikiano na taasisi za fedha vimewezesha wachimbaji wadogo kuchangia zaidi katika uchumi na kuongeza mapato ya Serikali. Tanzania imekuwa mfano bora wa kuigwa, na mataifa mengine yanaendelea kujifunza kutokana na mafanikio haya.