Na Hamisi Miraji, Timesmajira Online
UNAPOZUNGUMZIA dawa za kulevya ni kitu hatari sana kwa binadamu na jamii kwa ujumla kwa kuwa husababisha magonjwa kama mapafu na kuharibu utindio wa ubongo. Mfano wa madawa hayo ni kama Cocaine, heroin, bangi na mirungi.
Wapo watu wengi walioathiriwa na dawa za kulevya, lakini yanazidi kuenea kwa sababu ni biashara kubwa inayoingiza pesa nyingi.
Serikali inatakiwa kutoa elimu kuhusiana na madhara yatokanayo na matumizi ya dawa za kulevya, kwani ni hatari kwa maisha ya binadamu na kwa jamii.
Katika kuhakikisha Serikali inakabiliana na janga hilo Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imejikita katika kutathmini hatua zilizofikiwa na serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini Tanzania.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania awamu ya sita, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameongoza nchi tangu Machi 2021, na katika kipindi chake cha uongozi, amekuwa na mkakati wa kweli wa kupambana na tatizo la dawa za kulevya, ambalo ni janga kubwa la kijamii na kiuchumi.
Hata hivyo kuna baadhi ya mafanikio na hatua alizochukua katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya katika kipindi chake cha miaka minne:
1.Kuimarisha Sheria na Sera, 2. Kuhamasisha wananchi, 3.Kuanzisha mifumo ya kutoa misaada, 4. Kujumuisha wadau wa kimataifa,5. Kupambana na uuzwaji wa dawa za kulevya 6. kuwa na Mpango Mkakati.
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), hivi karibuni ilifanya kikao kazi na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, ambapo walizungumzia mafanikio ya Mamlaka hiyo chini ya Rais wa awamu ya Sita Dkt. Samia Suluhu Hassan katika miaka minne ya uongozi wake.
Kikao hicho kiliandaliwa na Kamishna wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo katika Makao Makuu ya Mamlaka jijini Dar es Salaam.
DCEA, imepata mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka minne ya utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan katika juhudi zake za kupambana na waharifu wa dawa za kulevya. Serikali imeimarisha mikakati ya kisiasa na kiuchumi ili kudhibiti na kukabiliana na tatizo la biashara hiyo haramu.
Kwa kipindi cha miaka minne, DCEA imeshirikiana na taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi ili kuboresha upelelezi, kukamata, na kuwafilisi waharifu wa dawa hizo.
Aidha, Wizara husika imeongeza rasilimali za kifedha na vifaa kwa ajili ya operesheni za kupambana na dawa za kulevya, ikiwa ni pamoja na mafunzo ya kitaalamu kwa maafisa.
Katika hatua nyingine, Rais Samia pia ameongeza mwamko wa jamii juu ya athari za matumizi ya dawa za kulevya, kupitia kampeni za elimu na uhamasishaji. Hii imeongeza uelewa miongoni mwa wananchi na kuhamasisha ushirikiano katika kutoa taarifa kuhusu shughuli za waharifu.
Juhudi hizo zinaongeza uwezo wa DCEA, katika kufanya kazi zao na kupunguza ukubwa wa tatizo la dawa za kulevya nchini. Hata hivyo, bado kuna kazi kubwa ya kufanyika ili kuhakikisha kuwa nchi inakuwa salama kutokana na ushawishi wa biashara hiyo haramu.

Akizungumzia hilo Kamishna wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo anasema katika kipindi cha awamu ya sita ambayo miaka minne ya Rais wa Jamhuri ya Muungao wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuna mafanikio makubwa katika kupambana na vita dhidi ya dawa za kulevyo.
Anasema, Katika kipindi cha miaka minne kadri siku zinavyodi mafanikio yamekuwa makubwa zaidi kulinganisha na kipindi cha nyuma.
Pia, anasema sasa hivi wananchi wamekuwa na imani na serikali ya awamu ya sita kupitia Mamlaka ya udhibiti wa Dawa za Kulevya (DCEA), kutokana na kuona baadhi ya mafanikio yanayopatikana dhidi ya dawa za kulevya.
Hiyo imekuja baada ya kuona baadhi ya watuhumiwa wakubwa ambao walikuwa hawashikiki wanakamatwa katika kipindi hiki cha awamu ya sita.
1.Kupambana na uuzwaji wa dawa za kulevya
Katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, Serikali imeimarisha juhudi za kuzuia na kupambana na mitandao ya uuzaji dawa za kulevya, kupitia operesheni maalum ambazo zimepelekea kukamatwa kwa wafanyabiashara wakubwa wa dawa hizo.
Akiweka wazi hilo Kamishna Lyimo anasema, kipindi cha nyuma kulikuwa na watu wanaitwa Zungu la Unga ambao mitaani walikuwa wakiwajua lakini walikuwa hawakamatwi na hata ukitoa taarifa, mtoa taarifa ndio wa kwanza kushughurikiwa na maisha yao yanakuwa hatarini. Lakini sasa hao watu hawapo.
Kamishna Jenerali Lymo anasema katika kipindi cha awamu ya sita kwa mara ya kwanza wamekamata wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya, ambapo kilogram 3,500 zilikatwa Kigamboni mkoani Dar es Salaam.
Anasema, dawa hizo zilikamatwa Desemba 2023, kwa mara ya kwanza haijawai kutokea kukamatwa kwa dawa hizo za kulevya, jambo hilo Mamlaka kupitia serikali ya awamu ya sita inajivunia.
Aidha, anasema Kiwango hicho hakijawahi kukamatwa katika kipindi chochote tokea mamlaka hizi zianzishwe na hata kabla ya Tanzania ijulikane. Kwa hiyo inaonekana ukishamkuta mtu wa kiwango kikubwa kama kile ambacho ni mabilioni ya hela kwenye zile dawa ni mafanikio ya awamu ya sita.
“Mafanikio ya awamu ya sita yanatokana na kwamba kwa mara ya kwanza Tanzania kuwa na Rais mwanamke, siku zote mzazi huwa hapendi kumuona mtoto wake anaharibikiwa ndio maana unaona mafanikio haya yamekuwa makubwa zaidi kwa sababu Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameonesha kwa vitendo namna ya kupambana na dawa za kulevya kwa sababu anajua athari zake kwa jamii, anajua athari zake kwa vijana pamoja na watoto.
“Kutokana na kutambua hilo ndio maana Rais Samia ameweka msisitizo mkubwa sana katika kipindi chake anataka aone kuwa Tanzania sio watumiaji wa dawa za kulevya, isiwe na usambazaji mkubwa wa dawa za kulevya.” anasema Kamishna Lyimo.
Vilevile, anasema awali Tanzania ilikuwa ndio mlango mkuu wa kupitisha dawa za kulevya na dunia nzima ilikuwa inajua hilo, hata watanzania wengi waliokuwa wakienda nje wakifika uwanja wa ndege wakiangaliwa hati zao za kusafiria wakigundua ni mtanzania lazima uwekwe pembeni kwanza kwa kutaka kujua unakotokea.
Lakini pia, anasema ukiangalia watanzania wengi waliopo nje maeneo mbalimbali kama vile Afrika Kusini, Asia, Indonesia NK, wengi wao wasafirishaji wa dawa za kulevya lakini kwa sasa hivi hali hiyo imepungua kwa asilimia kubwa sana.
Kwa nini imepungua baada ya kufanya kazi kubwa katika kipindi hiki chwa awamu ya sita kuwakamata wale waliokuwa wakiwawezesha kusafirisha dawa za kulevya nje ya nchi.
“Hiyo imekuja baada ya operation zilizofanyika kipindi hiki zimeleta mafanikio makubwa sana kutokana na msukumo wa Rais Samia kuiamsha mamlaka lakini pia, kuongeza nguvu kubwa katika kutuongezea vifaa hasa rasilimali mipango,” anesema Kamishana Jenerali Lyimo.
Vilevile anasema kwa mwaka wa jana na juzi walikamatwa watu takribani 29, 187 wakiwemo wale wa kigeni ambao mali zao limetaifishwa huku akiweka wazi kuwa mpaka sasa kesi zilikuwa 2001 na serikali imeshinda asilimia 80.
Hata hivyo anasema, katika kuhakikisha mitandao ya dawa za kulevya inakufa, mpaka sasa wameshakamata mitandao mitano ya ndani na nje miwili.
Pia, katika kipindi cha miaka minne ya mafanikio ya Raisa Samia, DCEA imekata madawa ya kelevya Kilogram 38,342.53 mwaka 2021, mwaka 2022 kilagram 43,596.101, mwaka 2023 1,964,028.14 na mwaka 2024 ilikua kilogram 2,411,267.221.
Kamishna Jenerali Lyimo anasema, mafanikio mengine ya awamu ya sita kukabiliana na waharifu wa dawa za kulevya ni rasilimali mipango, Rais amewanunulia magari mapya ndio maana operation nyingi zinafanyika mpaka vijijini kwani mwanzoni kulikuwa hakuna magari ya kufika huko vijijini.
Mbali na hivyo, pia Rais amewaongezea rasilimali fedha kwa sababu ili ufanye zile operation lazima utumie gharama hivyo amesaidi kuweza kukabiliana na waharifu wa dawa za kulevya mitaani, pia amewaongezea rasilimali watu kwenye hizo kazi.

“Mwanzo tulikuwa na watumishi wachache huwezi kufanya operation nchini nzima kwa sababu ya uchache
wa watu tuliokuwa nao, kwa mfano wakati Mamlaka inaanza ilikuwa na watumishi 102, lakini sasa hivi wameongezwa na kufikia zaidi ya watu 200 na kuendelea, kwa muda mfupi tu wa kipindi hiki na ndio maana mafanikio yamekuwa makubwa zaidi kutokana na hizi Operation za dawa za kulevya,” anasema Kamishna Lyimo.
Aidha, anasema katika kuhakikisha dawa za kulevya zinadhibitiwa kuingia nchini au kutoka, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupamba na Dawa za Kulevya (DCEA), imewezesha kuanzisha kanda tano.
Anasema, hapo awali kulikua hakuna kanda hizo zaidi ya Makao Makuu ya ofisi kwa hiyo hata Operation ilikuwa ngumu sana kufanya kutokana na gharama kubwa kwa sababu mtu anatoka dar anakwenda mtwara lakini baadae inamlazimu kurejea dar kukamilisha kazi zake jambo ambalo lilikuwa likichangia ufanisi mdogo.
Kamishna Jenerali Lyimo anasema, kupitia serikali ya awamu ya sita wameweza kuanzisha kanda tano ambazo ni;
- Kanda ya Kaskazini
Kanda hiyo ya Kaskazini inajumuisha Mikoa ya Manyara, Arusha, Kilimanjaro pamoja na Tanga.
Kamishna Jenerali Lyimo anasema mikoa hiyo yote ofisi zake za DCEA zipo mkoani Arusha, wameweka Maofisa, magari pamoja na vifaa kwa ajili ya kudhibidi mipaka ya Namanga, Horohoro, Tarakea na mengine kuhakikisha maeneo hayo uvushaji wa dawa za kulevya unadhibitiwa.
Anasema, baada ya kuanzisha Kanda ya Kaskazini hususani mkoa wa Arusha, mafanikio makubwa yamepatikana katika kipindi hiki cha awamu ya sita kwa sababu ni mkoa ambao ulikuwa unaongoza kwa kilimo cha bangi, ilikuwa inasafirisha ndani ya nchini na hata nje ya nchi.
Vile vile, anasema baada ya ile Kanda kuwepo katika Mkoa wa Arusha na operation iliyokuwa ikifanywa mara kwa mara bangi pamoja na kilimo chake kimepungua sana.
Hata hivyo anasema, baada ya operation nyingi kufanyika katika mkoa huo watu sasa hivi wamegundua mbinu nyingine ya kulima bangi ndani ya nyumba.
“Mtu anajenga hall lake ndani ya nyumba na kulima bangi mfano mzuri kama jamii ilivyoona hivi karibuni tulivyokamata mtu akilima kilimo hicho ndani,” anasema Kamishna Jenerali.
Anasema, moja ya mafanikio katika miaka minne ya Rais Samia ni hiyo ya kudhibiti kilimo cha bangi mkoani Arusha jambo ambalo pia limepunguza uharifu.
- Kanda ya Ziwa
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupamba na Dawa za Kulevya (DCEA), imeanzisha ofisi pia, Kanda ya Ziwa ambayo inahudumia Kagera, Geita, Mwanza yenyewe, Simiyu, Shinyanga pamoja na Mara, mkoa ambao umekithiri kwa ulimaji wa bangi.
Kamishna Jenerali wa Mamlaka hiyo, Aretas Lyimo anasema wameiweka Kanda ya Ziwa ambapo Ofisi zake zipo Mwanza kwa ajili ya kufanya Operation ya kupambana na dawa za kulevya katika mikoa iliyopo kanda hiyo.
Anasema, mafanikio makubwa yaliopatikana katika Kanda hiyo ni kupunguza dawa za kulevya kwa sababu jiji la Mwanza hali ya dawa za kulevya ilikuwa kubwa sana hasa matumizi ya heroine.
“Kutokana na hali hiyo kukithiri mkoani Mwanza, tukaanzisha Mat-Klinic kwa ajili ya kuwahudumia Warahibu wa dawa za kulevya ambao walikuwa wengi sana, kutokana jiji hilo kuwa na mchanganyiko wa watu.
“Wengine wanakuja kwa njia ya Ziwa, kutoka nchi tulizopakana nazo wanauza dawa za kulevya pale, lakini operation zilizofanyika kwa sasa hali ya dawa za kulevya jiji la Mwanza zimepungua, sio kama zimeisha kabisa,” anasema Kamishna Jenerali Lyimo.

Aidha, anasema operation ya kwanza kufanyika tokea Tanzania ifahamike kwa sababu Mara kule ni walimaji wakubwa sana wa bangi na kulikuwa hakuna mtu yoyote yule anayeweza kufanya kule kutokana na watu wa kule kuwa wakatili.
Anasema, kuna kipindi kuliwahi kufanyika operation na vyombo vingine lakini kulitokea mapigano kwa kuwapiga Maofisa wa serikali waliotaka kwenda kuona mashamba ya bangi wameshindwa hata kufika.
Lakini baada ya Mamlaka kuanzisha Ofisi kule na kufanya uchunguzi wa kina wakabainika wale wakulima na kuwatiwa nguvuni na mashamba yao kufyekwa kwa mara ya kwanza Mamlaka ilitekeza hekali nyingi za mashamba ya bangi.
“Mwaka jana tumeteketeza hekali zaidi ya 3000 kwa miaka miwili zaidi ya hekali 4000 ni hekali kubwa sana haijawahi kutokea, wamelima eneo kubwa sana katika mto Mara, na ule mto Mara ndio Ikolojia ya kupeleka maji katika Mbuga ya srengeti.
“Kwa hiyo lile eneo baada ya Rais Samia kuona kwamba uharibifu unaendelea kufanyika, watu hawana uthubutu wa kufanya zile Operation, tulienda kufanya operation ya kutosha kupitia kwa Maofisa wenye weledi waliopitia mafunzo pamoja na kuwa na vifaa vya kisasa kwa sababu bila ya vifaa huwezi kufika kule ni mbali sana.
“Ni eneo ambalo unatembea zaidi ya masaa mawili, unaenda na gari unaliacha baadae ndio ufike ni eneo moja ambalo kubwa sana na tambalale ambalo wananchi walilitawala hilo eneo kama vile lakwao.Lakini kipindi hiki cha awamu ya sita hilo limewezekana kutokana uwezeshaji wa Rais Samia,” anasema Kamishna Jenerali Lyimo.
- Kanda ya Kati Dodoma
Hili ni eneo ambalo pia, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupamba na Dawa za Kulevya (DCEA), iliamua kuanzisha kwa kuhudumia Dodoma enyewe, Singida, Tabora pamoja na kigoma.
Dodoma ni eneo ambalo ni Makao ya nchi, Mamlaka imefungua Ofisi kuhakikisha Makao Makuu ya nchi hakuna matumizi ya dawa za kulevya lengo ni kutokomeza uharifu katika sehemu muhimu ya nchi.
Kamishna Jenerali Lyima anasema asilimia kubwa wanaofanya uharifu ni wale wanaotumia dawa za kulevya, Wabakaji, vibaka, wauaji, wanaolawitiana. Kwa sababu mtu mwenye akili timamu hawezi fanya vitu kama vile.
“Wengi tuliowakamata hata hapa Dar es Salaam wale Panya Road asilimia 96 wengi wao walikuwa wanatumia dawa za kulenya na asilimia kubwa walikuwa wanatumia bangi na ndio maana unaona bangi inapigwa marufuku dunia nzima kwa sababu bangi ina madhara makubwa sana.
“Kwanza ukivuta bangi unajiamini sana unaona mtu mwengine hawezi kukufanya chochote ndio maana wanavunja majumba, wanaingia wanaiba na wenginea wanabaka au kukukata mapanga, hii si akili ya kawaida kwa sababu unapovuta bangi inaharibu uwezo wako wa kufikiri kama mwanadamu,” anasema Kamishna.

Kamishna Lyimo anasema lengo la kuanzisha Kanda ya Kati ni kuhakikisha mji Mkuu wa serikali shughuri ziweze kufanyika pale na kupunguza uhalifu, pale mjini kulikuwa na waharifu wengi sana lakini baada ya kuanzisha Kanda kulifanyika operation kubwa.
Anasema, kutokana na kufanya Operation kubwa walifanikiwa kumkamata muuzaji wa dawa za kulevya maarufu alikuwa akijulikana kwa hina la Zungu la Unga ambaye alishindikana na watu wote na hakuna aliyekuwa anamgusa.
“Hawa wauzaji wa dawa za kulevya ni wafadhiri wakubwa sana kwenye taasisi za dini, taasisi za serikali pamoja na kwenye vyama vya kisisa ili kujenga dhamana linapotokea amekamatwa wengi wao watamtetea.
“Lakini kipindi hichi cha awamu ya sita chini ya Rais Samia kinasema mtu akikamatwa na dawa za kulevya akiwa na kidhibiti hakuna msamaha hata awe na jina kubwa kiasi gani ndio maana sasa hivi hawa wanaokamatwa hakuna hata mmoja anayejitokeza kumtetea.
“Rais amesisitiza katika awamu yake kila tunayemkamata na ushahidi upo ili asije akatumia udhaifu wa Operation zile akajitetea kuwa huyu amekamatwa katika mazingira ambayo hakuwa na dawa za kulevya, ndio maana kila anayekamatwa lazima akamatwe tena akiwana na kiwango kikubwa cha dawa kwa sababu mtu anayekamatwa na kiwango kidogo cha dawa ni rahisi kulalamika,” anasema Kamishna Jenerali Lyimo.
Aidha, anasema mtuhumiwa yoyote anapokamatwa na mzigo mkubwa kwanza adhabu yake haina dhamana na kifungo chake kuanzia miaka 30 mpaka kifungo cha maisha
Anasema, Wanokamatwa na mizigo midogo wana dhamana lakini pia kifungo chake chini ya miaka 30, kwa mfano dawa za viwandani kuanzia gramu 200 hazina dhamana na kifungo chake miaka 30 lakini kuanzia gramu 500 kifungo chake maisha.
Lakini pia, anasema dawa za kulevya aina ya mirungi kuanzia kila 20 haina dhamana na kifungo chake kinaanzia miaka 30, kuanzia kila 100 kifungo chake maisha. Hiyo ni dawa za kulevya aina ya bangi na mirungi.
Mafanikio makubwa yaliopatokana pale baada ya kuanzisha Kanda ya Kati, DCEA walikuta shamba kubwa la bangi katika maeneo ya Chamwino lenye hekali 14 lakini pia, wale walimaji walikuwa na silaha za moto
wanalinda lile shamba
Kwa hiyo waliteketeza yale mashamba yote na hayajirudii, lakini pia walifanya Operation maeneo ya Kondoa mwezi wa pili mwaka huu waliteketeza hekali 300 na bado operationa inaendelea mpaka sasa hivi kuna hekali zingine zimeteketezwa zinafika hekali 500 ambazo hazijatangazwa.
Kamishna Jenerali Lyimo anasema, sio Kondoa tu hata Mkoa wa Tabora katika misitu ya Nzega ilifanyika Operation ya nguvu pamoja na Mkoa wa Singida kuhakikisha dawa za kulevya zinapungua kwa kiasi kikubwa ijapokuwa hazijaisha kabisa.
- Kanda ya Pwani
Kanda ya Pwani inajumuisha mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Pwani yenyewe pamoja na Morogoro. Baada ya kuanzishwa Kanda hii, awali dawa za kulevya zilikua zinapitishwa ukanda wa Bahari zinapitia Mtwara baadaye zinaletwa Dar es Salaam, na kusambazwa maeneo mengine kwa hiyo Kanda hiyo ilianzishwa makusudi kuhakikisha wanaziba mianya ya upitishaji wa dawa kupitia katika njia mbalimbali.
- Kanda ya Nyanda za Juu Kusini
Kamishna Jenerali Lyimo anasema Kanda hiyo inahudumia Mikoa ya Rukwa, Songwe, Mbeya, Njombe pamoja na Iringa. Kanda hii haipo vizuri katika mipaka yake ikiwemo Tunduma na maeneo mingine
Anasema, mara baada ya kuanzisha Kanda hiyo kwa mara ya kwanza ilisaidia kukamata zile Cocaine ambazo zinatoka huko lakini pia walifanikiwa kumkamata mfanyabiashara na pusha mkubwa wa dawa za kulevya katika Kanda hiyo aliyejulikana kwa jina la Horohoro, ambaye alikuwa akisambaza sana dawa za kulevya.
Mfanya biashara huyo ndio alikuwa akisafirisha vijana wanaomeza dawa hizo tumboni ambapo kwa wiki alikuwa akisafirisha watu 18 kuelekea nchi mbalimbali. Hatua hiyo ni mafanikio makubwa sana kipindi cha awamu tya sita kwa sababu huyo mtu alikuwa akitafutwa tokea miaka ya 2000 na vyombo dola na hata nchi ya Marekani.

Lakini pia, anasema walianza kukamatwa bangi za kusindika zinazojulikana kwa jina la ‘Sikanka’ ni bangi kali kuliko hata ya kawaida. Haina hiyo ya kilevi ni kikali kikiingia mwilini na kusababisha urahibu uliokithiri jambo ambalo linachangia kupoteza nguvu ya Taifa.
Anasema, shida kubwa bado jamii haijaelelewa mazara makubwa ya bangi lakini ni dawa ambazo zinamfanya mwanadamu kutenda mambo ambayo hayapendezi ikiwemo uharifu wa hali ya juu kwa Rais aliliona hilo ndio maana wanafanya Operation ya hali ya juu kuhakikisha hali hiyo inapungua na mafanikio yameonekana.
Mafunzo
Katika kuhakikisha wafanya Operation wa dawa za kulevya wanakuwa na weledi mkubwa, Rais Samia amewawezesha watumisha wa Mamlaka hiyo kupata mafunzo mbalimbali ndani na je ya nchi.
Watumishi wameweza kupata mafunzo kwa ufadhili wa nchi mbalimbali kutokana na mahusiano mazuru ya Rais Samia aliyojenga kwenye mataifa mbalimbali.
“Watumishi wameenda kujifunza Singapore, Marekani, Uingereza, Ujerumani, Viena, Austria pamoja na nchi zingine ambazo zimetoa mafunzo kwa Tanzania kwa ajili ya operation ya dawa za kulevya,” anasema Kamishna Jenerali Lyimo.
Kamishna Jenerali Lyimo anasema, kutokana na mafunzo hayo na uwezeshaji huo pia Rais Samia ametoa pesa ambapo kwa mara ya kwanza mwaka 2023 wameweza kujenga maabara ya kisasa ya kupima dawa za kulevya ambayo ilikamilika mwaka 2024 na 2025 ndio imeanza kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa.
Anasema, vifaa vya kupima dawa za kulevya zinauzwa kwa bei kubwa sana ambapo kifaa kimoja kinauzwa milioni 200 cha kupima tu dawa za kulevya, kwa hiyo katika kipindi kiki Rais Samia ameweza kuiwezesha Mamlaka kuwa na maabara.
Hata hivyo anasema, bila ya kuwa na maabara ya kisasa wasingweza kufanya kazi viwanja vya ndege pamoja na bandarini kwa sababu unapokamata dawa mtu anasafiri yupo na ndege unamkamata unahisi kama huna kifaa inakulazimu uwende kwa mkemia ndio upate majibu huku ndege inamuacha kwa hiyo Rais kupitia maabara hiyo amenunua vifaa vya kisasa ambavyo vinapima ndani ya sekunde mbili unapata majibu kwa kutambua aina ya dawa.

“Kuna vifaa vitatu Rais Samia ametununulia ambacho kifaa kimoja kina uwezo wa kupima aina ya 12,000 ambazo ni nyingi sana karibia dawa zote za kulevya, lakini pia, kuna vifaa vingine vya kisasa ametununulia kwa mfano mtu ana begi lake amebeba dawa za kulevya huitaji kufungua begi kuna kifaa unagusisha kwenye kile kifurushi hapohapo kinakusomea ni aina gani ya dawa.
“Lengo ni kujenga mahusiano mazuri na wananchi, wasafiri, mataifa mengine na serikali kwa ajili ya kutokera watu, kuchukiza unakuta mtu ameleta dawa zake unazifungua unaenda kupima ameshachelewa ndege unarudi unamwambia hizi sio dawa za kulevya kwa hiyo unaweza kuendelea na ndege ishamuacha.
“Kwa hiyo ndio maana tumeona tuboreshe hilo ili kazi zetu pia zilete mafanikio kwa sababu Rais anataka serikali inayokuwa kiuchumi lazima uingie uwekezaji, lazima uvutie wasafiri, watalii na watu mbalimbali waingie nchini,” anasema Kamishna Lyimo
- Kuwahamasisha Wananchi
Rais Samia katika kipindi chake cha awamu ya sita amekuwa akisisitiza umuhimu wa elimu na uhamasishaji kuhusu hathari za dawa za kulevya, akishirikiana na wadau mbalimbali wa jamii, ikiwemo shule na taasisi za kidini, ili kuzuia vijana kuingia katika matumizi ya dawa hizo.
Akizungumzia kuhusu elimu, Kamishna Lyimo anasema eneo lingine ambalo Rais Samia katika kipindi hiki cha awamu ya sita alitoa msisitizo kuhusu Elimu, licha ya kufanya Operation lakini jamii inatakia ipewe elimu ili kujua madhara ya dawa za kulevya kwa sababu watu watakamatwa na kujikuta wakijaa gerezani na kukosa pa kuwaweka.
“Kwa kipindi hiki tumeweza kufikia watu milioni 28, watu hawa ni wengi sana ukiangalia Tanzania ina watu takribani milioni 62 kwa hiyo angalau tumekaribia nusu ya Watanzania ambao wanajua dawa za kulevya ni nini.
“Zamani hakuna mtu aliyekuwa anajua Cocaine, heroine, bangi na mirungi lakini sasa hivi hata wanafunzi wanatambua dawa hizo, tumeamua kutengeneza vipeperushi ili kutoa elimu ya kutosha kuhusu dawa za kulevya,” anasema Kamishna Lyimo.
Anasema, kutokana na hilo katika Kanda zote tano wamepeleka waelimishaji kuwaelimisha, kwa sababu zipo program nyingi sana zinaendele huko shule za msingi ambapo wengi wanaaribikiwa kuanzia pale.
Kwa hiyo wamenunua vifaa mbalimbali vya kuelimisha ikiwemo Spika kubwa za matangazo na hata wanapoenda kwenye mashule hayana umeme zinafanya kazi zaidi ya masaa sita kuhakikisha watu wanapata elimu ya kutosha kuhusu dawa za kulevya.
Pia, anasema wameungana na TAKUKURU katika uelimishaji kwa sababu Takukuru walikua washaanzisha klabu mbalimbali kuhusu madhara ya rushwa katika shule za msingi, sekondari na vyuo, kwa hiyo wameingia makubaliano nao sasa zinaitwa klabu za kupinga Rushwa na dawa za kulevya.
Mafnikio mengine kutunga kitabu cha muongozo kitabu hicho ndicho kinachotoa muongozo wa uelimishaji kuhusiana na dawa za kelevya kuanzia shule ya msingi, sekondari, vyuoni, mitaani hadi kwa wanahabari, viongozi wa dini, walezi, wazazi yaani kina Categori 12 mafunzo ya kufundishia.
“Kitabu tumewapa watu wa TAKUKURU ambao tuliwapa elimu waelimishaji nchi nzima, Dodoma tuliwagawia vitabu kwa hiyo tunapokwenda kuelimisha shule ya msingi kuhusiana na maswala ya rushwa anaelimisha pia kuhusiana na dawa za kulevya
“Na sisi tunapokwenda kwenye shule nyingine kwenda kuelimisha dawa za kulevya na wao wanatupa muongozo wao kuelimisha pia na rushwa, lengo ni kufikia watu wengi kwa pamoja kwa kutumia rasilimali chache tulizonazo kuweza kutoa hiyo elimu,” anasema Kamishna Lyimo.
Kamishna Lyimo anasema, kasi kubwa zaidi imeongezeka kuanzia mwaka 2023 mpaka sasa hivi na kufanya watu wote hao kuweza kupata elimu.
Pia, anasema mafanikio mengine ambayo Rais Samia alielekeza kwamba kwenye mtaala wa ufundishaji wa shule za msingi kuwepo na mada za dawa za kulevya kwa hiyo kwenye lile somo la maadili tayari wizara ya elimu ilishaelekezwa kila kitu kuwa kutakuwa na somo la dawa la kulevya.
Kwa hiyo wanafunzi kutoka shule ya msingi wataelewa sasa aina ya dawa za kulevya, madhara yake na vitu vingine, hivyo kizazi kijacho kitajikuta kwamba kina uelewa mkubwa zaidi kuhusiana na dawa za kulevya na kupunguza athari kubwa hapa nchini.
- Kuanzisha Mifumo ya Kutoa Msaada
Serikali imetambua umuhimu wa msaada kwa watumiaji wa dawa za kulevya na imeanzisha vituo vya kusaidia na kurekebisha tabia za watu walioathirika na tatizo hili. Hii ni pamoja na huduma za afya ya akili na matibabu ya kuacha kutumia dawa.
Akielezea kuhusu Matibabu ya waathirika wa dawa za kulevya, Kamishna Jenerali Lyimo anasema katika kipindi cha awamu ya sita chini ya Rais Samia, Mamlaka imeboresha zaidi eneo la matibabu kwa wale ambao wameathiriwa na dawa za kulevya,
Anasema, kwenye eneo hilo Rais Samia wakati anaingia madarakani vituo vya Mat-clinic vilikuwa 11, lakini kwa kipindi chake kifupi amejenga vituo 16 ambavyo vinafanya kazi na tayari vimepewa zana za kazi zote.
Vituo hivyo kwa sasa vinahudumia warahibu 18170 kwenye Mat-Clinic, ni wengi sana ambao wanapata matibabu na wamejiondoa kwenye matumizi ya dawa za kulevya.
Vilevile, anasema kuna vituo vingine vitano sasa hivi, kwa mwaka huu vitano vinajengwa kwa wakati mmoja. Viwili tayari vimeshakamilika vinasubiri kununuliwa Fanicha na mashine ya kupima dawa.
“Kuna mashine inapima dozi kulingana na umri wako, kulingana na athari kwa maana umeathirika kiasi gani, kwa hiyo kuna mashine ukiingiza dole gumba lako inakupimia dawa gani na milimita ngapi unatumia, bila ya hiyo mashine utachukua muda mrefu sana,” anasema Kamishna Lyimo.
Anasema, vituo vitatu vimeshaanza kujengwa, ambapo vingine vinajengwa Mkuranga, Kilimajaro na Kahama na tayari fedha zishapelekwa na wakandarasi wapo site kwa ajili ya ujenzi, kwa hiyo ni mafanikio makubwa sana katika kutibu ili waathirika wanaweza kurudi kwenye jamii na kuleta maendeleo.
Lengo kubwa la awamu sita, Rais Samia anataka kujenga uchumi endelevu hivyo hakuna budi kuwa na watu wenye afya njema na akili timamu, na nchi yoyote yenye warahibu wa dawa za kulevya haiwezi kuendelea kwa sababu athari inakuwa kubwa sana
Mafanikio mengine katika kutibu Warahibu ni Soba House, kipindi hiki cha awamu ya sita, chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, wakati anaingia madarakani kulikuwa na Soba House 42 sasa hivi zipo 62, hiyo ni kwasababu ya uhamasishaji kwa jamii na watu wenye uwezo.
Soba House zilianzishwa za kutosha kwa kipindi kichache tu zimeanzishwa 20 kwa hiyo uwezeshaji wa serikali wamewasaidia kupata maeneo hayo, kutoa elimu, kuratibu namna ya uanzishaji na kusimamia.
Anasema, kule Soba House mpaka sasa hivi kuna watu 17,000 Soba House zote, lakini pia Rais ameelekeza kwenye Hospitali zote Rufaa, Mikoa pamoja na zile za kikanda zitoe matibabu bure kwa wale Warahibu wa dawa za kulevya na vilevi vingine.
Kwa hiyo kwa kipindi hiki tayari watu 900000, wameshatibiwa kwa hospitali zote nchi nzima, lengo ni kuwasaidia ili warejee katika jamii na kujenga uchumi imara.

Mbali na hivyo pia sasa hivi kuna ujenzi umeanza wa kitua kikubwa cha Taifa cha Utengamavu kinaitwa Rehabitation Center, kimeanza kujengwa eneo la Itega, mkoani Dodoma.
Hata hivyo, Kamishna Lyima anasema kituo hicho kinajengwa kwa fedha za serikali, ambapo Rais amepitisha bajeti na tayari kuna fedha zitatoka zaidi ya milioni 800 na ujenzi umeanza mara moja.
Aidha, anasema kitiuo hicho kitakuwa kikubwa na kitakuwa kinabeba warahibu wote kutoka kwenye Soba House mara baada ya kupata nafuu anapelekwa pale na wakishapelekwa wataendelea kupata elimu namna ya kuacha dawa za kulevya, lakini pia watapata mafunzo ya ufundi satadi wa aina zote.
“Kutakuwa na karakana kubwa anayetaka kushona atafundishwa, Makenika, Compute nk. mwisho wa siku ukishamaliza utapewa vifaa vya kazi, hilo ni eneo moja wapo la awamu ya sita imesema, hawa watu tunawatibu ukishawatibu wanarudi mtaani wanakuwa hawana cha kufanya.
“Sawa amepona hana shughuri ya kufanya na kuanza kupata msongo wamawazo jambo ambalo litamchangia kurejea kwenye dawa za kulevya kwa hiyo tutajikuta tunatibu lakini wanarudia kwa hiyo kimeanzisha kitua hichi watakusanywa watu wote wakihitimu mafunzo wanapewa zana za kazi.
“Lakini pia kama kuna project mbalimbali za serikali zinazoendelea wataunganishwa ili kupata pesa za kujikimu na kwa kuanzia wale waliopo kwenye kitua pale Dodoma watafanya kazi ndogondogo za vibarua,” anasema Kamishna Lyimo.
“Kwa kasi hii tukienda nayo nina uhakika dawa za kulevya mtaani zitapungua sana na hii ndio dhamira ya Rais kuhakikisha zinapungua na ikiwezekana zinaisha kabisa,” anaongeza Kamishna Lyimo.
- Kuwajumuisha Wadau wa Kimataifa
Katika eneo hili, Rais Samia ameshauriana na nchi mbalimbali na mashirika ya kimataifa ili kupata msaada wa kiufundi na rasilimali katika kupambana na dawa za kulevya.
Ushirikiano huo unasaidia katika kuboresha uwezo wa vyombo vya dola na kuimarisha mikakati ya kupambana na biashara haramu ya dawa.
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupamba na Dawa za Kulevya (DCEA),inafanya kazi kwa karibu na mataifa mengine katika juhudi za kukabiliana na tatizo la matumizi na biashara haramu ya dawa za kulevya. Ushirikiano huo unajumuisha vitu mbalimbali kama vile:
Kushirikiana Katika Utekelezaji wa Sheria: Mamlaka hizi zinashirikiana kwa kubadilishana taarifa na kuanzisha operesheni za pamoja ili kukamata wahalifu wa dawa za kulevya.
Mikataba ya Kimataifa: Mataifa yanashirikiana kupitia mikataba mbalimbali kama vile Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Dawa za Kulevya, ambao unalenga kudhibiti uzalishaji, usambazaji, na matumizi ya dawa za kulevya.
DCEA, tayari imeshaingia makubaliano na Zambia kwa sababu ni njia mojawapo inayopitisha dawa za kulevya zikitokea Afrika Kusini, wameingia makubaliano ili kufanya operation kwa pamoja hususani kwenye ile eneo la mpaka wa Tunduma, ambalo lilikuwa likitumika sana kuingiza dawa za kulevya nchini.
Lakini pia, kuna nchi nyingi wanaendelea kufanya nayo mazungumzo kwa ajili ya kuingia nao makubaliano kufanya Operation mbalimbali ikiwemo India, ambao wao ndio wazalishaji wakubwa wa Kemikali Bashirifu, asilimia kubwa ya Makampuni yanayoagiza Kemikali Bashirifu yanatoka India.
Kwa hiyo wanajenga makubaliano kuhakikisha kwamba kila anayeagiza Kemikali Bashirifu zinakuja Tanzania lazima taarifa zifahamike.
- Mpango Mkakati kupambana na dawa za kulevy
Mpango mkakati wa kupambana na dawa za kulevya ni mchakato wa kupanga na kutekeleza hatua mbalimbali ili kudhibiti na kupunguza tatizo la matumizi na biashara ya dawa za kulevya.
Hata hivyo, serikali imeweka mikakati ya muda mrefu katika kupambana na tatizo la dawa za kulevya, ikijumuisha ushirikiano kati ya wizara mbalimbali na vyombo vya usalama kama polisi na forodha.
Kuongeza uelewa kuhusu madhara ya dawa za kulevya kupitia kampeni za elimu, semina, na vikundi vya usalama katika jamii.
Kuimarisha sheria na kanuni zinazohusiana na biashara ya dawa za kulevya, pamoja na kuanzisha mikakati ya kukabiliana na uhalifu wa dawa za kulevya.
Hatua hizo ni danguro katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya, lakini bado kuna changamoto nyingi, ikiwa ni pamoja na mfumo wa kiuchumi, uelewa wa jamii, na mtazamo wa baadhi ya watu kuhusu tatizo hili. Ni muhimu kwa serikali kuendelea kuimarisha juhudi hizo ili kuweza kufikia malengo yaliyowekwa
More Stories
Tanzania yaadhimisha siku ya hali ya hewa,kwa kuhakikisha uwekezaji wa miundombinu ya hali ya hewa na usambazaji wa huduma zake.Â
TMDA kuendeleza mikakati katika kukomesha uingizwaji wa dawa na vifaa bandia nchini
Sakaya;Mungu,ujasiri na kujiamini ndio siri ya mafanikio safari ya siasa/ kutetea wananchi-sehemu ya mwisho