March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Miaka minne ya mageuzi chini ya Rais Dkt. Samia

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Dar

CHINI ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Tanzania imepitia mabadiliko makubwa katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake.

Katika kipindi hicho, mabadiliko makubwa yamefanyika katika karibu sekta zote ikiwemo, sekta uchumi, elimu, afya, usafiri na miundombinu ya mawasiliano , demokrasia na mahusiano ya
Kimataifa, wakati huo huo yakitengenezwa mazingira rafiki ya uwekezaji kwa wawekezaji wapya pamoja na fursa za Maendeleo.

Hata hivyo, mafanikio makubwa ya Rais Samia ambayo yatabaki kwenye kitabu cha historia ya nchi ni mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya Nishati .

Bila shaka, Watanzania ambao walikuwa wakifuatilia kwa karibu jinsi nchi ilivyokuwa haifanyi vizuri katika sekta ya nishati kwa vipindi vya Serikali zilizopita, sasa watakuwa mashahidi wazuri wa mabadiliko ambayo yamefanywa na yanaendelea kufanya na Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dokta Samia.

Hadi kufikia Mwezi wa pili 2025, uzalishaji wa Umeme umeongezeka hadi kufika megawatts 3,796.71 ukiwa umeongezeka mara mbili zaidi ya megawatts 1,889.84 ambazo zilirekodiwa Januari mwaka
2024.

Hivyo basi, utekelezaji wa Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) wenye uwezo wa kuzalisha umeme wa kiwango cha megawatts,2,115 hivi sasa umefikia asilimia 99.8 ili uweze kukamilika kwa kuwa tayari mashine nane kati ya tisa zimeanza kufanyakazi
zikizalisha jumla ya Megawatts 1,880.

Mradi huu sio tu umeondoa upungufu wa umeme bali pia umeondoa mitambo ya uzalishaji umeme inayotumia mafuta ya dizeli ambayo ni ya
gharama kubwa na hivyo kuongeza upatikanaji wa umeme katika maeneo ya mijini na vijijini, lakini pia kuwezesha usafiri kupitia Reli ya Kisasa (SGR) na kupita umeme katika maeneo ambayo awali hayakuwa na umeme .

Kutokana na umuhimu wa sekta ya nishati kwa maendeleo ya nchi, Serikali iliahidi kwamba itaimarisha upatikanaji wa nishati nchini, hasa kwa kukamilisha ujenzi wa Bwawa hilo la Kufua Umeme la Mwalimu
Nyerere na kufikisha umeme kwenye vijiji vyote.

Msukumo uliotolewa na Serikali ya awamu ya sita umewezesha ongezeko kubwa la uzalishaji wa umeme kutoka MW 1,601.84 mwaka 2020 hadi MW 4,031.71 kwa sasa na hali hii imechangiwa na ukamilishaji wa miradi mbalimbali ya uzalishaji na usambazaji umeme
ikiwemo mradi wa kielelezo wa Kuzalisha Umeme kwa Kutumia Maji wa Julius Nyerere (JNHPP) wenye MW 2,115.

Vilevile, miradi mingine iliyokamilishwa katika kipindi hiki ni Mradi wa Kuzalisha umeme wa Kinyerezi I Extension MW 185 kwa kutumia gesi asilia na Mradi wa Rusumo ambao umetekelezwa katika Mto Kagera
kwa ushirikiano wa nchi tatu za Tanzania, Burundi na Rwanda kwa mgawanyo sawa wa umeme (MW 26.67).

Juhudi za Rais Samia katika kufanya mabadiliko kwenye Sekta ya Nishati zimeenda mbali zaidi nchini Tanzania wakati ambapo pia yeye ni kinara wa kampeni ya matumizi ya Nishati safi ya kupikia Barani
Afrika.

Mbali na kuja na mkakati wa matumizi ya nishati safi kitaifa pia ameendelea kuitangaza kampeni hiyo katika ngazi za Kimataifa akijitahidi kuhakikisha kuwa suala la kupika linafanyika kwa njia zenye kuzingatia afya lakini pia kwa njia rafiki kimazingira.

Katika kipindi cha uongozi wake, Rais Samia ameweza kuandaa Mkutano wa Nishati Barani Afrika ambao ulihudhuriwa na viongozi wakubwa kutoka mataifa 22.

Mkutano huo ulilenga kutengeneza mikakati itakayosaidia kufikisha huduma ya umeme kwa watu wapatao milioni 300 waliopo Afrika hadi kufikia mwaka 2030 na nikipindi ambacho nchi hizo 12 ikiwemo mwenyeji Tanzania ziliwasilisha pia
makubaliano ya Mataifa yao katika Nishati kwa Mwaka 2025-2030.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, .Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa safarini kutoka Dar es Salaam kuelekea Jijini Dodoma Juni 26, 2025. Pamoja na mambo mengine Rais Dkt. Samia alihutubia na kuhitimisha shughuli za Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Lakini pia chini ya uongozi wake Rais Samia Tanzania ilirekodi historia ya kuvunja rekodi kwa kuzindua huduma ya treni ya SGR kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma Agosti 1, 2024, ikipanua mtandao wa reli
kutoka kilomita 722 hadi kilomita 2,102, ambapo zaidi ya abiria milioni mbili hadi sasa wamenufaika na huduma za SGR mradi ambao umetengeneza mapato yapatayo bilioni 54 kuanzia siku ulipozinduliwa
hadi mwezi Machi mwaka huu 2025.

Katika kipindi kama hicho pia Serikali chini ya Rais Samia iliweza kupata ufadhili wa kujenga laini ya SGR kutoka Tabora hadi Kigoma ili uimarisha biashara na nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Serikali pia, imekamilisha miradi ya usambazaji umeme ikiwemo mradi wa ujenzi wa njia za kusafirisha umeme yenye urefu wa kilomita 414 kutoka Singida – Arusha – Namanga; kilomita 144 kutoka Geita – Nyakanazi; njia ya Julius Nyerere hadi Chalinze; njia ya Nyakanazi hadi
Kigoma; njia ya kilomita 115 kutoka Tabora – Urambo na njia ya kilomita 94 kutoka Rusumo-Nyakanazi.

Bwawa la Mwalimu Nyerere

Mafanikio hayo yameongeza upatikanaji wa nishati ya umeme ya uhakika katika maeneo mbalimbali nchini. Aidha, Mama Samia na Serikali yake wamefanikiwa kuiunganisha mikoa ya Kigoma na Katavi kwenye Gridi ya Taifa ya umeme.

Katika Sekta ya Ndege, Shirika la Ndege Tanzania limepata ndege mpya saba, na kuongeza idadi yake
hadi ndege 14 za abiria na ndege moja ya mizigo, na hivyo kuongeza idadi ya abiria wanaotumia ndege za shirika hilo kwa kiwango kikubwa.

Lakini pia Serikali imeendelea kuwekeza katika kupanua Bandari pamoja na kuzifanyia maboresho Bandari zilizopo ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa bandari ya Dar es Salaam mradi unaogharimu dola
milioni 421 za Marekani ili kuongeza uwezo na ushindani.

Hivi karibuni Serikali ilisema inajenga bandari nyingine nje ya Manispaa ya Mtwara Mikindani itakayotumika kusafirisha bidhaa chafuzi kwa mazingira na afya kama vile saruji na makaa ya mawe, kwa ajili ya magari yote yanayobeba makaa ya mawe kupita nje ya manispaa
kuelekea bandarini. 

Nihitimishe Makala hii naomba nikukumbushe kwamba Serikali ya awamu ya sita iliahidi na imefikia hatua kubwa na ya kistoria kwenye usambazaji, kwa kuweza kupeleka umeme kwenye vijiji vyote 12,318 vya Tanzania Bara kama alivyoahidi.

Kwa sasa, Serikali inaendelea na kazi ya kupeleka umeme kwenye vitongoji, ambapo tayari vitongoji 33,657 kati ya 64,359 vimeshafikiwa, sawa na asilimia 52.3.

Nimemsikiliza Pia Rais wakati akizungumza Bungeni,
alisema kwamba Serikali pia ina mpango wa kuzalisha nishati mbadala kupitia vyanzo jadidifu lakini pia wakati anmuapisha Mkurugenzi Mtendaji wa sasa wa Tanesco alimwelekeza kuona umuhimu wa
kuanza kuzalisha nishati ya nyuklia.

Lakini pia kama ambavyo imekuwa ni kilio cha Watanzania wengi hivi sasa kwa mujibu wa Rais Dkt.
Samia wanapanga kuweka ushindani kwenye sekta hii ya nishati kwa kualika sekta binafsi kushiriki ili kuongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika na nafuu.

Nashusha chini kalamu yangu kwa leo, lakini nikuhakikishie kwamba tutaziangalia sekta zote ambazo nimezitaja hapo juu wakati nikianza.