November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

MIAKA 61 YA UHURU, sekta ya barabara ilivyo kichocheo muhimu kwa maendeleo ya uchumi na kijamii

Judith Ferdinand, Times Majira Online

Barabara nchini ni nguzo muhimu katika sekta ya usafiri na usafirishaji ambayo kwa kiwango kikubwa utumiwa na watu wote kuanzia wenye vipato vya chini,kati na juu.

Mtandao wa barabara za umma Tanzania Bara una jumla ya kilometa 180,792,kama ilivyo kwa nchi nyingine, rasilimali ya barabara ndiyo rasilimali ya umma yenye thamani kubwa zaidi ambayo inakadiriwa kuchangia asilimia 16 ya Pato la Taifa.

Rasilimali barabara ndiyo njia kuu ya usafiri na usafirishaji ambapo zaidi ya asilimia 90 ya wasafiri na zaidi ya asilimia 80 ya mizigo hutumia njia hiyo.

Usafiri na usafirishaji kwa njia ya barabara ni ya uhakika na ni moja ya vichocheo muhimu vya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Nini umuhimu wa barabara katika sekta ya usafiri na usafirishaji.

Jiografia ya Tanzania, ukubwa wake na mtawanyiko wa makazi ya watu hufanya barabara kuwa ni mchango wa kipekee katika kuleta utengamano wa kijamii na kiuchumi.

Usafiri na usafirishaji kwa njia ya barabara ndio pekee unaotegemewa na unaotumiwa kwa asilimia kubwa katika maeneo ya mjini pamoja na vijijini ambako hakuna njia nyingine ya usafiri kama reli na anga.

Asilimia kubwa ya usafiri na usafirishaji kati ya miji mikubwa na vijiji unatumia zaidi miundombinu ya barabara zaidi ambayo ndio iliopo.

Muunganiko unaoletwa na barabara ni nyenzo muhimu sana inayochangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi huku ufanisi wa mipango ya Serikali inayolenga maendeleo ya vijijini, uzalishaji wa ajira pamoja na maendeleo ya viwanda kwa kiasi kikubwa unachangiwa na ubora wa huduma za usafiri kwa njia ya barabara.

Ambapo ndio njia pekee na rahisi inayosaidia kuwaunganisha wazalishaji na masoko, wafanyakazi na ajira, wanafunzi na shule pamoja na wagonjwa na hospitali, barabara zinatoa mchango muhimu katika kutimiza malengo ya Serikali ya kuaharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi.

Kupitia barabara wazalishaji wanaweza kufikisha bidhaa zao hadi kwenye masoko yaliyo katika maeneo ya vijijini jambo ambalo si rahisi kwa kutumia njia nyingine za usafiri kama reli, anga na usafi kwa njia ya maji.

Nini umuhimu wa matengenezo ya barabara katika kuboresha huduma za usafiri

Kama ilivyo kwa rasilimali nyingine, barabara zinaharibika kutokana na muda wa matumizi, wingi wa magari yanayotumia barabara na wakati mwingine kutokana na athari za kimazingira pamoja na kufanyika shughuli za kijamii kando kando ya barabara.

Hivyo ili kuendelea kulinda thamani ya barabara na kuzifanya zitumike wakati wote, hakuna budi kuzifanyia matengenezo kikamilifu na kwa wakati.

Miundombinu ya barabara isipotunzwa na kufanyiwa matengenezo kwa wakati inaweza kuharibika kabisa kiasi cha kuhitaji kujengwa upya.

Ambapo matokeo ya tafiti yanaonesha gharama ya ujenzi mpya huwa zaidi ya mara tatu ya gharama ya matengenezo stahili ya barabara husika.

Inakadiriwa kuwa gharama za matengenezo huongezeka mara sita ya gharama kama barabara isipofanyiwa matengenezo kwa miaka mitatu na kama isipofanyiwa matengenezo kwa miaka mitano gharama huongezeka mara kumi na nane hivyo ni muhimu kufanya matengenezo
ili kuepuka gharama hizo.

Pia barabara isipofanyiwa matengenezo stahili na kamilifu husababisha madhara mengi kwa watumiaji wake ikiwa ni pamoja na gharama kubwa za uendeshaji wa vyombo vinavyotumia njia hiyo.

Ambapo gharama hizo ni kama vile matengenezo ya magari, matumizi ya mafuta na vilainishi, kuongezeka kwa muda wa safari,hivyo husababisha ongezeko la gharama za usafiri na usafirishaji huku ubovu wa barabara husababisha ajali kwa watumiaji wa barabara.

Hata hivyo kuchelewa kufanya matengenezo au kufanya matengenezo yasiyokidhi mahitaji kuna athari kubwa zaidi kwa madaraja na makalvati kwani yanapoharibika husababisha njia kutokupitika na hivyo kuathiri matumizi ya barabara kwa muda.

Matengenezo ya barabara yakifanyika kwa muda sahihi husogeza mbele au kuahirisha kwa muda kipindi ambacho barabara ingepaswa kujengwa upya.

Vile vile hupunguza gharama kwa mtumiaji wa barabara na kupunguza idadi ya ajali za barabarani.

Faida nyingine za kufanya matengenezo ya barabara ni pamoja na:

Kuongeza kiwango cha faida iliyokusudiwa ambapo matengenezo ya barabara huongeza kipindi ambacho barabara itatumika na hivyo kuongeza faida iliyokusudiwa wakati inajengwa.

Kupunguza gharama za ujenzi.

Barabara inayofanyiwa matengenezo kwa wakati huchukua muda mrefu kuharibika na hivyo kupunguza gharama za ukarabati mkubwa unaosababishwa na barabara kuchelewa kufanyiwa matengenezo.

Matokeo ya tafiti yanaonesha kuwa kwa kila dola moja isiyotumika kufanya matengenezo, husababisha gharama za ukarabati kuongezeka kwa dola 5 za Marekani.

Kupunguza gharama za uendeshaji magari.

Tafiti kuhusu gharama za uendeshaji magari zinaonesha kuwa kila dolla moja ya Marekani ambayo haikutumika kufanya matengenezo ili kuzuia uharibifu, inamgharimu mtumiaji dolla 3 za Marekani zaidi kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya mafuta.

Uharibifu wa vyombo vya usafiri,kupunguza muda wa matumizi wa matairi na kupunguza muda wa maisha ya gari.

Pia faida nyingine ni kuwezesha barabara kutumika muda wote ambapo barabara inayofanyiwa matengenezo kulingana na mahitaji na kwa wakati sahihi huzuia uwezekano wa kuchakaa haraka kwa miundombinu yake.

Hivyo inachangia ongezeko la usafiri wa uhakika na wa bei nafuu kwa wasafiri na wasafirishaji wa bidhaa mbalimbali.

Usimamizi wa Matengenezo ya Barabara

Kwa mantiki hiyo, ili kuhakikisha watumiaji wa barabara wananufaika na kulinda thamani ya uwekezaji wa Serikali, mtandao wa barabara unatakiwa kufanyiwa matengenezo kikamilifu na kwa wakati.

Uwezo wa kitaasisi, kiufundi na kifedha ni vigezo muhimu katika kufikia matengenezo ya uhakika, endelevu na yanayofanywa kwa wakati.

Kwa msingi huo Serikali ilifanya mageuzi makubwa kuanzia mwishoni mwa miaka 1990 kwenye usimamizi wa sekta ndogo ya barabara ili kutatua changamoto ya uharibifu wa barabara kutokana na kutofanyiwa matengenezo kikamilifu kwa muda mrefu.

Mageuzi hayo yalilenga kuoanisha majukumu ya kitaasisi katika kusimamia rasilimali ya barabara kama ifuatavyo:-

Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi:
Usimamizi wa sera, sheria, kanuni, miongozo na viwango pamoja na ufuatiliaji na tathmini wa kazi za barabara.

Wakala za Barabara:
Kusanifu, kujenga na kufanya matengenezo ya miundombinu ya barabara.

Bodi ya Mfuko wa Barabara:
Kukusanya fedha za kugharamia matengenezo ya barabara, kugawa fedha kwa Wakala wa Barabara na kufuatilia matumizi yake.

Wizara ya Fedha:
Kutafuta fedha za kugharamia kazi za ujenzi wa barabara.

Ambapo kabla ya mageuzi hayo, matengenezo ya barabara yalikuwa yanagharamiwa kupitia Mfuko Mkuu wa Serikali na kutekelezwa na Wizara ya Ujenzi hivyo Kutokana na mahitaji makubwa ya kibajeti, kiasi kidogo cha fedha kilikuwa kinatengwa kwa ajili ya kugharamia matengenezo ya barabara.

Hii ilisababisha sehemu kubwa ya mtandao kuwa na hali mbaya na sehemu nyingine kutopitika kabisa.mathalani asilimia ya barabara zilizokuwa kwenye hali nzuri ilishuka kutoka asilimia 85 miaka ya 1960 na kufikia asilimia 15 na asilimia 10 kwa barabara za Kitaifa na Wilaya na mtawalia.

Lengo la kuundwa kwa Mfuko na Bodi ya Barabara.

Mfuko na Bodi yake ya Barabara viliundwa mwaka 2000 kupitia Sheria ya Tozo za Barabara na Mafuta, Sura ya 220 kwa lengo kubwa la kuhakikisha uwepo endelevu wa fedha za kutosha kwa ajili ya kugharamia matengenezo ya barabara.

Ugharamiaji wa matengenezo ya barabara.

Matengenezo ya barabara hugharamiwa na watumiaji wa barabara kupitia malipo ya tozo ya matumizi ya barabara (road user charges),hii ni kwa mujibu wa kanuni ya “user-pay ambayo mtumiaji wa barabara uhitajika kufidia uharibifu wa barabara unaosababishwa na gari lake.

Mtumiaji hutakiwa kulipa tozo inayolingana na gharama ya kufidia uharibifu huo,hivyo chini ya utaratibu huu, Serikali hugharamia tu ujenzi wa barabara mpya na jukumu la kugharamia matengenezo huwa la mtumiaji wa barabara.

Vyanzo vya Mapato vya Mfuko wa Barabara.

Vyanzo vikuu vya mapato ya Mfuko ni tozo mbalimbali ikiwemo tozo mafuta (fuel levy),tozo ya magari ya kigeni (transit charges) na tozo ya kuzidisha uzito wa magari (Overloading charges).

Tozo ya mafuta huchangia zaidi ya asilimia 97 ya mapato ya Mfuko kwa kupitia vyanzo hivyo watumiaji wa barabara kuchangia matengenezo ya barabara na kufidia uharibifu unaosababishwa na magari yao.

Uzoefu kutoka baadhi ya nchi za Kiafrika unaonyesha tozo ya mafuta ndicho chanzo kikuu cha kugharamia matengenezo ya barabara. Aidha, kwenye baadhi ya nchi, matengenezo ya barabara yanagharamiwa na bajeti kuu ya serikali.

Mafanikio ya kuundwa kwa Mfuko wa Barabara na Bodi yake.

Kuundwa kwa Mfuko na Bodi yake kumewezesha kuwepo na mfumo imara wa ugharamiaji na usimamizi wa kazi za matengenezo ya barabara ikiwemo
Uhakika wa fedha za kugharamia matengenezo ya barabara kila mwaka.

Ambapo fedha za Mfuko zimetengwa mahususi kisheria (ring-fenced) kwa ajili ya kugharamia matengenezo ya barabara na makusanyo ya Mfuko yamekuwa ya wastani wa Tsh. bilioni 807.5 kwa mwaka.

Hivyo bajeti ya kugharamia matengenezo pamoja na mtiririko wa fedha kwa ajili hiyo ni wa uhakika na hii inawezesha Wakala kuwa na mipango madhubuti ya matengenezo kila mwaka.

Kuimarika kwa mtandao wa barabara,kuanzia mwaka 2016/17 hadi 2021/22, sehemu ya barabara za Kitaifa na Wilaya zilizo kwenye hali nzuri na wastani imekuwa ni asilimia 88 na asilimia 56, mtawalia kutoka wastani wa asilimia 15 mwishoni mwa miaka ya 1990.

Kuimarika kwa mifumo ya fedha na ufuatiliaji,ambapo ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za Mfuko umeimarika na mifumo ya usimamizi wa fedha imeimarishwa,hii imepunguza matumizi mabaya ya fedha na kuongeza ubora wa kazi za barabara.

Wajibu wa Wananchi Katika kutunza Barabara.

Watumiaji wa barabara wanao wajibu mkubwa wa kuzitunza barabara ili kuhakikisha zinatumika kwa muda mrefu na kulinda thamani yake. Hatua ambazo watumiaji wa barabara na wananchi kwa ujumla wanaweza kuchukua ni pamoja kuhakikisha maji hayapiti au kutuama barabarani.

Kwani maji ni adui namba moja wa miundombinu ya barabara ambapo yanapopita au kutuama barabarani husababisha barabara kuharibika haraka, hasa barabara za changarawe na udongo.

Pia matabaka ya chini ya barabara za lami uharibika na kusababisha hasara kubwa,hivyo ni kosa kisheria mwananchi kutiririsha maji barabarani.

Kutozidisha uzito wa magari,kila barabara inapojengwa huwa ina ukomo wa uzito wa magari yanayoruhusiwa kutembea juu yake.

Endapo magari yenye uzito uliozidi uzito uliowekwa kisheria yatapitishwa juu ya barabara husika uharibika kabla ya muda wake na kugharimu fedha nyingi kuifanyia ukarabati na kuongezeka kwa gharama za uendeshaji.

Hivyo ni kosa kisheria kuzidisha uzito na adhabu zimeoanishwa kwa kila kiwango cha uzito unaozidi.

Hata hivyo kutunza samani za barabara ni jukumu la kila mwananchi ikiwemo taa na vibao ili zisiharibiwe au kuibiwa kwani kutokuwepo kwa samani hizo kunaweza kusababisha ajali na kuleta hasara kubwa za kijamii na kiuchumi.

Kutopitisha mifugo barabarani,kutembea kwa mifugo barabarani husababisha barabara kuharibika kabla ya muda wake,hivyo wananchi wanahimizwa kupitisha mifugo yao mbali na barabara ili kuepusha uharibifu huo.

Kutokutengenezea magari barabarani,utengenezeaji wa magari barabarani husababisha uharibifu wa barabara kutokana na kumwagika kwa mafuta na vilainishi barabarani hivyo wenye magari wanahimizwa kuzingatia sheria kwa kutotengenezea magari barabarani.

Aidha Wananchi wanapaswa kutoa taarifa za hali ya barabara kutoa taarifa za uharibifu wa barabara kwa Wakala wa Barabara kutawezesha kufanyiwa matengenezo kwa wakati ambapo taarifa hizo ni pamoja na barabara kujifunga au mashimo makubwa katikati ya barabara.

Bodi ya Mfuko wa Barabara imeunda Mfumo wa Kielektroniki wa kufuatilia hali ya barabara (e-Monitoring Application) ambapo mfumo huo umeundwa mahsusi kuwawezesha wananchi hasa watumiaji wa barabara, kushiriki katika kusimamia na kutunza miundombinu ya barabara katika maeneo wanayopita kwa kutuma taarifa muhimu za hali ya barabara. Mwananchi anaweza kutuma taarifa kwa kutumia utaratibu ufuatao:

Meneja Mfuko wa Barabara nchini,Eliud Nyauhenga
Matengenezo ya moja ya barabara nchini yakiendelea