Na Mwandishi Wetu,Timesmajira
MWENYEKITI wa Baraza la Taasisi ya Elimu Tanzania Profesa Maulid Mwatawala amezindua kampeni ya upandaji miti katika kuelekea Maadhimisho ya Miaka 50 ya TET yanayotarajia kufanyika mwishoni mwa mwezi Juni 2025.
Profesa Mwatawala aliongoza zoezi hilo Mei 10, 2025 katika Ofisi za TET Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wajumbe wa Baraza pamoja na menejimenti ya taasisi hiyo.
Akiongoza tukio hilo, Profesa Mwatawala amesema, kampeni hii ya upandikizaji miti ni sehemu ya jitahada ya kuunga mkono maono ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya utunzaji mazingira hasa kutokana na uchapaji vitabu vinavyotumia karatasi ambazo zinatokana na miti.
“Sisi ni watumiaji sana wa miti katika kuandaa vitabu, kwahiyo tunapenda miti kwasababu miti ndio inayotoa bidhaa karatasi ambayo inatumika katika vitabu. ” Amesema Profesa Mwatawala.
Aidha, Profesa Mwatawala ameiomba Serikali kuendelea kuisaidia TET kwa kutoa fedha hasa katika kipindi hiki ambacho utekelezaji wa Mtaala ulioboreshwa unaendelea nchini, hasa katika maeneo ya uwekezaji wa teknolojia ya Tehama.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania Dk. Aneth Komba, amesema TET imejipanga kuendelea na kampeni hii kwa kupanda miti bustani katika maeneo mbalimbali ikiwemo katika shule na taasisi mbalimbali ili kuendelea kuhifadhi mazingira na kuunga mkono juhudi za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
More Stories
Kapinga:Serikali inaboresha miundombinu ya umeme kibiti kuondoa changamoto ya umeme
Mwili wa Hayati Msuya wawasili Uwanja wa Ndege wa (KIA)
Dkt. Biteko avutiwa mwitikio Tulia marathon