Na Mwandishi Wetu,Timesmajira
Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imesema maandalizi ya Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), maarufu kama Sabasaba, yamekamilika huku maadhimisho ya mwaka huu yakitarajiwa kuwa ya kipekee kutokana na kutimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwa maonesho hayo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Juni 24, 2026, Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Dkt. Ratifa Mohamed Khamis, alisema maonesho hayo yatafanyika kuanzia Juni 28 hadi Julai 13, 2026, yakilenga kukuza biashara, uwekezaji na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi.
Amesema TanTrade, kwa niaba ya Wizara ya Viwanda na Biashara, imeendelea kushirikiana kwa karibu na sekta binafsi pamoja na wadau mbalimbali wa biashara kuhakikisha maonesho hayo yanakuwa na tija kubwa kwa washiriki.
“Madhumuni makuu ya maonesho haya si burudani pekee, bali ni kutoa jukwaa linalowawezesha wafanyabiashara kukutana, kujenga mitandao ya kibiashara, kutangaza bidhaa na huduma zao pamoja na kufungua masoko mapya,” amesema Dkt. Ratifa.

Amebainisha kuwa moja ya matukio makubwa yatakayobeba sura ya kipekee mwaka huu ni Usiku wa Jubilei ya Dhahabu, utakaofanyika Julai 6, 2026, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Sabasaba.
Kwa mujibu wa Dkt. Ratifa, hafla hiyo itajumuisha maonesho ya kumbukumbu mbalimbali yanayoeleza historia ya Sabasaba tangu kuanzishwa kwake, uzinduzi wa filamu maalum ya kumbukumbu pamoja na utambuzi wa wadau waliotoa mchango mkubwa katika ukuaji na mafanikio ya maonesho hayo kwa kipindi cha nusu karne.
Aidha, amesema washiriki na wadau mbalimbali watatunukiwa tuzo maalum katika hafla hiyo, huku baadhi ya tuzo ambazo kwa kawaida hutolewa wakati wa ufunguzi wa maonesho zikihamishiwa kwenye usiku huo maalum ili kuongeza hadhi ya maadhimisho ya Jubilei ya Dhahabu.
Dkt. Ratifa pia ametambua mchango wa vyombo vya habari katika maendeleo ya maonesho ya Sabasaba, akisema waandishi wa habari wamekuwa nguzo muhimu katika kuyatangaza na kuyafikisha kwa wananchi kwa miaka yote.
“Waandishi wa habari ni sehemu ya mafanikio ya maonesho haya. Wamekuwa mstari wa mbele katika kuyatangaza kwa miaka yote, hivyo nao watatambuliwa kwa mchango wao katika usiku huu maalum wa Jubilei ya Dhahabu,” alisema.
Akizungumzia mafanikio ya maonesho hayo, Dkt Ratifa amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuyaimarisha maonesho ya Sabasaba na kuyapa hadhi kubwa zaidi kimataifa, jambo lililochochea ongezeko la ushiriki wa wafanyabiashara na wawekezaji kutoka mataifa mbalimbali duniani.
Amesema hadi sasa nchi 23 zimethibitisha kushiriki katika maonesho hayo, huku matarajio yakiwa ni kuongezeka kwa idadi hiyo kutokana na nchi nyingine, zikiwemo Burundi, Kenya na Algeria, kuendelea na maandalizi ya ushiriki wao.
Dkt. Ratifa ametoa wito kwa Watanzania, wafanyabiashara, wawekezaji na wadau wa maendeleo kutoka ndani na nje ya nchi kujitokeza kwa wingi kushiriki maonesho hayo, akisisitiza kuwa Sabasaba 2026 itakuwa fursa muhimu ya kukuza biashara, kuvutia uwekezaji na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi katika kipindi ambacho Tanzania inaendelea kujiimarisha kwenye ramani ya biashara za kimataifa.
“Sabasaba 2026 si maonesho ya kawaida; ni maadhimisho ya miaka 50 ya mafanikio, ubunifu na mchango mkubwa wa biashara katika maendeleo ya uchumi wa Tanzania,” amesema Dkt. Ratifa.

More Stories
TISEZA Songea kuvutia uwekezaji, ajira zaidi zapatikana
Serikali yajipanga kukabiliana na athari za El Nino
Wadau watakiwa kushirikiana Kuhifadhi Ziwa Tanganyika