December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Miaka 3 ya Dkt. Samia na hali ya mtandao wa barabara nchini

Na Mwandishi Wetu

Mtandao wa barabara nchini una jumla ya Kilometa 181,602.2 zikijumisha kilometa 37,225.7 za barabara za Kitaifa na kilometa 144,376.5 za barabara za Wilaya.

Barabara za Kitaifa zinasimamiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na barabara za Wilaya zinasimamiwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).

Kutokana na hali ya jiografia ya nchi ya Tanzania usafiri wa barabara ndiyo njia inayotumiwa zaidi kwa usafiri na usafirishaji.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Barabara Mhandisi Rashid Kalimbaga

Inakadiriwa kuwa zaidi ya asilimia 90 na 80 ya abiria na mizigo, mtawalia hutumia barabara hivyo ufanisi wa mipango ya Serikali inayolenga maendeleo ya vijijini, uzalishaji wa ajira, maendeleo ya viwanda, kwa kiasi kikubwa unachangiwa na ubora wa huduma za usafiri wa barabara.

Miundombinu ya barabara ndiyo rasilimali ya umma yenye thamani kubwa inakadiriwa kufikia Trilioni 39.5 sawa na asilimia 23 ya Pato la Taifa.

Juhudi za Serikali katika kuboresha hali miundombinu ya barabara nchini kwa kutambua thamani na umuhimu wa barabara kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi imekuwa ikiimarisha uwezo wa kifedha na kitaasisi ili kuzilinda barabara kwa lengo la kuziwezesha kutumika kwa muda uliopangwa.

Katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake, Rais Dkt Samia Suluhu Hassan serikali imekuwa ikitenga wastani wa bilioni 850 kila mwaka kwa ajili ya kugharamia matengenezo ya barabara hapa nchini.

Fedha hizi zimewezesha utekelezaji wa wastani wa miradi 620 ya matengenezo ya barabara za Kitaifa na miradi 850 kwa barabara za Wilaya kila mwaka.

Aidha Serikali imekuwa ikiimarisha uwezo wa taasisi zinazosimamia kazi za barabara hususani TANROADS, TARURA na Bodi ya Mfuko wa Barabara kwa kuziongezea vitendea kazi pamoja na wataalam.

Kuimarika kwa uwezo wa kifedha na kitaasisi kumewezesha matengenezo ya barabara kufanyika mara kwa mara.

Hivyo kufanyika kwa matengenezo hayo kumesaidia zaidi ya asilimia 90 ya mtandao wa barabara za Kitaifa uko kwenye hali nzuri na wastani.

Aidha zaidi ya asilimia 60 ya mtandao wa barabara za Wilaya uko kwenye hali nzuri na wastani.

Hivyo sehemu kubwa ya mtandao wa barabara unapitika kipindi chote cha mwaka hali hii imeiwezesha Tanzania kuwa moja ya nchi za Afrika zenye mtandao bora wa barabara ambao sehemu kubwa inapitika majira yote.

Hata pale mawasiliano ya barabara yanapokuwa yamekatika kutokana na mafuriko, serikali imekuwa ikitoa fedha mara moja ili kurudisha mawasiliano kwa wakati na hivyo kuwawezesha wananchi kuendelea na shughuli zao za kijamii na kiuchumi.

“Mfano ni kazi za dharura zilizofanyika maeneo ya Hanang (Manyara), Liwale (Lindi) na Ununio (Dar es Salaam), ambapo kwa kuboresha miundombinu ya barabara, wananchi wamewezeshwa kuzifikia huduma za kijamii na kiuchumi ikiwemo elimu, afya, masoko, ajira na fursa nyingine za kujipatia kipato,”.

Usimamizi na ugharamiaji wa matengenezo ya barabara

Barabara zikishajengwa zinahitaji kufanyiwa matengenezo kikamilifu ili kulinda thamani yake na uwekezaji wa Serikali pamoja na kuziwezesha kutumika kwa muda uliopangwa.

“Hii ni kwa sababau ubora wa barabara hupungua kutokana na kuzeeka, uzito wa magari na athari za mabadiliko ya tabianchi ambapo matengenezo yasipofanyika kikamilifu, barabara uharibika mapema na hivyo kupoteza thamani yake na thamani ya uwekezaji wa serikali na kuongeza gharama za usafiri na usafirishaji,”.

Matengenezo ya barabara hapa nchini yanasimamiwa na kugharamiwa chini ya Sheria ya Tozo za Barabara na Mafuta, Sura 220.

Chini ya Sheria hiyo Serikali iliunda Mfuko wa Barabara na Bodi yake mwaka 2000 ili kuhakikisha uwepo wa kutosha na endelevu wa fedha za kugharamia matengenezo ya barabara.

Serikali ilianzisha Mfuko wa Barabara kama moja ya mifuko maalum chini ya Ibara ya 135(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pia ilianzisha Mfuko na Bodi yake kama njia ya kutatua changamoto kubwa ya ubovu wa mtandao wa barabara kati ya miaka ya 1980 na 1990 kutokana na kutofanyiwa matengenezo kikamilifu.

Hata hivyo nchi nyingi za Afrika zilianzisha mifuko ya aina hii na hadi sasa kuna nchi 34 zenye mifuko hiyo na kwa mujibu wa Sheria, majukumu makuu ya bodi ni kuhakikisha upatikanaji wa fedha za kutosha za kugharamia matengenezo, kugawa fedha kwa Wakala wa Barabara na kufuatilia matumizi yake.

Tozo ya mafuta ni chanzo kikuu cha mapato ya Mfuko kwani huchangia wastani wa asilimia 96 ya mapato yote huku tozo ya mafuta kwa ajili ya kugharamia matengenezo ya barabara ni TZS 263 kwa kila lita ya petroli na dizeli.

Muonekano wa Daraja la Ngira mkoani Kilimanjaro lililojengwa kwa fedha za Mfuko wa Barabara.,katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia zaidi ya madaraja 160 yamejengwa kwa kutumia teknolojia mbadala ya mawe na matofali ya kuchoma ambapo madaraja hayo ni imara na yanauwezo wa kupitisha magari yenye uzito wa hadi tani 40

Vyanzo vingine ni ushuru wa magari ya kigeni (transit charges) na Tozo ya uzidishaji wa uzito,kwa mujibu wa Kifungu cha 4(2) cha Sheria ya Barabara na Mafuta, Sura ya 220, makusanyo yote ya Mfuko wa Barabara yanatakiwa yawekwe kwenye akaunti ya mfuko huo inayosimamiwa na bodi.

Hii ni kwa sababu mapato hayo yametengwa mahususi (ring-fenced) kwa ajili ya kugharamia matengenezo ya barabara za Kitaifa na Wilaya zinazosimamiwa na TANROADS na TARURA, mtawalia.

Moja ya mafanikio ya kuanzishwa kwa Mfuko wa Barabara na Bodi yake ni kuimarika kwa ubora wa mtandao wa barabara hapa mchini.

Barabara za Kitaifa zilizo kwenye hali nzuri zimeongezeka na kufikia wastani wa asilimia 90 kutoka wastani wa asilimia 13 mwaka 2000.

Aidha barabara za Wilaya zilizo kwenye hali nzuri na wastani zimeongezeka na kufika asilimia 60 toka asilimia 10 mwaka 2000.

Bodi ya Mfuko wa Barabara itaendelea kufanya kazi kwa juhudi na umahiri ili kutoa mchango unaotarajiwa ili kufikia malengo ya serikali.