November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mhina: Asilimia 70 ya wakazi wa Wilaya ya Muheza wanategemea zao la machungwa kiuchumi

Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online, Tanga

Asilimia 70 ya wananchi wa wilaya ya Muheza Mkoani Tanga wanategemea zao la machungwa kiuchumi hivyo Halmashauri ya wilaya hiyo inaangalia namna ya kuanzisha chombo kitakachosaidia kupambana na magonjwa, walanguzi, lakini pia kuongeza uzalishajo lengo likiwa ni kukifanya kilimo hicho kuwa na tija kwa Mkulima.

Akizungumza mara baada ya kikao maalumu cha kutoa taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka uliopita, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Erasto Mhina amesema kuwa kilimo cha machungwa kimechangia kwa kiwango kikubwa kwenye bajeti hiyo.

Mwenyekiti Mhina amesema kuwa Halamashauri hiyo imekusanya mapato yake kwa zaidi ya asilimia 100 ambapo kimsingi bajeti yao imekamilishwa na mazao ya kilimo ikiwemo machungwa na viungo hivyo mkakati wao ni kuendelea kuimarisha zao la michungwa kwani michungwa mingi ni ya muda mrefu.

“Mkakati wetu ni kuendelea kuimarisha zao hili la, michungwa kwakuwa mingi ni ya muda mrefu inazeeka hivyo lakini sasa tunategemea kutengeneza, chombo maalumu kitakachosimamia zao la chingwa, na mchakato wake umekwisha anza, “alisistiza Mwkt Mhina.

Aliongeza kuwa Tumekusanya zaidi ya asilimia 100 maana yake ni kwamba kila kilichopangwa kwenye bajeti kwa kutumia mapato ya ndani imeweza kupata fedha hatimaye kukamilika

Aidha alisema wameunda kamati maalumu inayohusisha wakulima wenyewe pamoja na wataalamu na wamekubaliana hadi ifikapo mwezi Desemba zoezi hilo liwe limeleta andiko litakalowawezesha kuwa na bodi ya matunda au kuwa na msimamo wa zao hilo katika Wilaya hiyo.

Akizungumzia viungo vinapatikana Wilayani humo ikowemo Iliki, Karafuu, Pilipili manga na Mdalasini Mwenyekiti huyo amesema kuwa viungo hivyo vimeendelea kuwa mkombozi kwa halamashauri hiyo katika mapato yake ya ndani.

“Tunashirikiana na mashirika mbalimbali ya, ndani na nje ya nchi kuhakilosha ubora wa mazao ya viungo katika wilaya yao unaongezeka lakini pia kuwawezesha wananchi kupitia maafisa ugani kwamba viumgo vyetu visitumie madawa na mbolea za kisasa na badala yake tutumie mbolea za asili na madawa ambayo hayana kemikali, “alisema Mwenyekiti Mhina.

Awali akizungumzia changamoto inayolikabili zao hilo la machungwa Mwenyekiti Mhina amesema kuwa ni ugonjwa wa Inzi ambapo matunda mengi yamekuwa yakiharibika pamoja na ukosefu wa kiwanda cha kuchakata machingwa hayo.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashairi hiyo Issa Msumari amesema mpango huo utasaidia kukomesha biashara ya madalali wanaonunua machungwa machanga na kuwalangua wakulima.

Kaimu Mkurugenzi huyo amesema mapato yao yanachangiwa na vyanzo vingi isipokuwa wana vyanzo vikuu viwili ikiwemo mazao ya kilimo, ikiwemo machungwa, mazao ya viungo pamoaja na zao la Mkonge ambalo hivi sasa limeingizwa kwenye mkakati wa kitaifa.

Madiwani wa Halmashauri hiyo akiwemo Asha Shekigenda na Mwanshamba Pashua wamesema mpango huo unapaswa kulenga kuelimisha kilimo bora na kuwabadilisha wakulima.

Halmashairi ya wilaya ya Muheza ilikusanya mapato yake ya ndani kwa asilimia mia moja katika mwaka wa fedha uliopita na kushoka nafasi ya pili kimkoa, bajeti iliyosaidiwa na kilimo cha machungwa na viungo.